Sunday, September 11, 2011

Ajali ya Meli Zanzibar: Maiti 192 zapatikana na 601 waokolewa wakiwa hai



Jumla ya maiti 192 zimepatikana na watu 601 wameokolewa wakiwa hai hadi sasa katika eneo la Nungwi mkoa wa Kaskazini Unguja ikiwa ni kati ya watu 760 waliosajiliwa kusafiri na meli ya MV Spice Islander iliyokuwa ikielekea kisiwani Pemba jana usiku wa Septemba 9, 2011 huku kukiwa na ongezeko la watu 33 hadi sasa na inaaminika kuwapo kwa watu zaidi watakao okolewa.
Baadhi ya Abiria walionusurika walisema kuwa abiria walijaa kupita kiasi katika Meli hiyo kongwe ya MV Spice Islander iliyokuwa ikielekea Pemba.
MV Spice Islander ilianzia safari yake kwenye Bandari ya Dar es Salaam ambapo iliondoka mchana wa Septemba 9, 2011 ikielekea Pemba kupitia Zanzibar.
Ingawa haijafahamika maramoja kuwa Dar es salaam iliondoka ikiwa na abiria wangapi na mizigo yenye tani ngapi, lakini meli hiyo ilitia nanga kwenye Bandari ya Zanzibar na kuondoka kuelekea Pemba usiku wa kuamkia Septemba 10, 2011 ikiwa na abiria 670 waliosajiliwa.
Mnamo majira ya saa 7.30 usiku meli hiyo ikiwa katika eneo la Nungwi mkoa wa kaskazini Unguja ilianza kupinduka polepole na hadi ilipofika saa 9.00 usiku meli hiyo ilipinduka na hatimaye kuzama kabisa kwa kuelemewa na mizigo pamoja na abiria.
Baadhi ya wananchi wameitupia lawama malka ya bandari na Sumatra kwa kushindwa kudhibiti uchukuzi wa abiria na mizigo kupita kiasi.
Kazi ya utafutaji wa watu walio hai na uopoaji wa maiti bado unaendelea na vikosi vya Jeshi la Polisi wanamaji wa JWTZ, KMKM,na JKU wanaendelea na kazi hiyo.
Jeshi la Polisi limetuma timu ya wataalamu wa Upelelezi na Madaktaji pamoja na Meli moja ya uokoaji MV Mamba ikiwa na boti nyingine ndogondogo ziendazo kasi za msaada majiuni.
Serikali ya Zanzibar na ile ya Muungano kupitia marais JK na Dk. Shein wametangaza siku tatu za maombolezo kuanzia kesho Septemba 11, 2011 na bendera zote zitapepea nuzu mlingoti.
Hakutakuwa na sherehe zozote ama mikusanyiko yenye kuonyesha buurudani na michezo.
Mh. Zito Kabwe, yeye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA na Waziri Kivuli wa Fedha, alikuwa ni miongoni mwa viongozi wa vyama vya Siasa waliofika katika viwanja vya Maisala mjini Zanzibar na kutoa Pole kwa wafiwa na kusema Chama chake kimesitisha kwa muda shughuli za kampeni katika jimbo la Igunga mkoani Tabora kutokana na msiba huo mzito.
Hiyo ni meli ya pili kuzama baharini ikiwa safarini kuelekea Pemba na meli ya kwanza ilikuwa ni MV Fatahi iliyozama mwaka jana 2010 ikiwa Bandari ya Zanzibar ikielekea Pemba.
Meli nyingine mbili ziliungua moto zikiwa bandarini Zanzibar na meli nyingine ya MV El- Salaam ilizama Baharini ikiwa na bidhaa mbalimbali ikielekea Songosongo Kilwa kwenye utafiti wa mafuta.

Saturday, September 10, 2011

NANI KATI YA WAREMBO HAWA KULIVAA TAJI LA MISS TANZANIA LEO?


HAWA NDIO WASHIRIKI WA VODACOM MISS TANZANIA 2011 AMBAO USIKU WA LEO WATAINGIA KATIKA KINYANG'ANYIRO CHA KUWANIA TAJI HILO.JE NANI ATAONDOKA NA TAJI HILO KATIKA HAWA??

JK AHUDHURIA MKUTANO WA PEMBE YA AFRIKA

Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na mwenyeji wakeRais Mwai Kibaki wa Kenya muda mfupi kabla ya kuanza kwa mkutano wa siku moja uliojadili tatizo la njaa na ukame linazozikabili nchi za pembe ya Afrika uliofanyika katika kituo cha Umoja wa mataifa uliopo Gigiri, nje kidogo ya jiji la Nairobi,Kenya jana asubuhi.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na Rais wa Somalia Sheikh Sharif Sheikh Ahmed jijini Nairobi kabla ya kuanza kwa mkutano uliojadili jinsi ya kukabiliana tatizo la njaa na ukame katika nchi za pembe ya Afrika.Katikati ni mwenyeji wa mkutano huo Rais Mwai Kibaki wa Kenya.

Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na mwenyeji wakeRais Mwai Kibaki wa Kenya muda mfupi kabla ya kuanza kwa mkutano wa siku moja uliojadili tatizo la njaa na ukame linazozikabili nchi za pembe ya Afrika uliofanyika katika kituo cha Umoja wa mataifa uliopo Gigiri, nje kidogo ya jiji la Nairobi,Kenya jana asubuhi.

Friday, September 9, 2011

GENEVIEVE MPANGALA KUKABIDHI TAJI LA MISS TANZANIA KESHO

Genevieve akiwa kwenye pozi, ambapo anatarajia kulikakabidhi taji la urembo wa Tanzania kesho kwenye ukumbi wa mlimani city kwa mrembo mpya wa mwaka 2011.Blog hii inakupongeza kwa kukaa na taji vizuri na inakutakia kila la heri kwenye maisha yako baada ya kuwa na taji kwa kipindi cha mwaka mmoja.

WAZIRI NUNDU AMTEUA DKT. KIJAZI KUWA MKURUGENZI MKUU WA HALI YA HEWA

 
Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu amemteua Dk. Agnes Lawrence Kijazi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Taarifa iliyotolewa juzi katika vyombo vya habari na kusainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi Omari Chambo ilisema uteuzi huo umefanyika kwa kuzingatia sheria ya wakala wa serikali Na. 30 ya mwaka 1997 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2009.
Aidha taarifa hiyo iliongeza kuwa kulingana na uteuzi huo Dk. Agnes Lawrence atachukua na kuitumikia nafasi hiyo kuanzia tarehe 06/09/2011 kwa kipindi cha miaka mitatu ambapo kitaisha tarehe 06/09/2014
Kabla ya kuteuliwa kushika wadhfa huo Dk. Kijazi alikuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.

KANALI GADDAFI AKANUSHA KUKIMBILIA NIGER


Kanali Gaddafi (PICHANI) azungumza na televisheni Syria

Aliyekuwa Kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi amekanusha taarifa za uvumi kuwa amekimbilia nchi jirani ya Niger, na kuziita ni uongo na vita ya kisaikolojia.

Alikuwa akizungumza kwa simu kutokea Libya na televisheni moja inayomuunga mkono nchini Syria.

Mapema, Niger ilisema inatafakari cha kufanya iwapo ataomba hifadhi nchini humo.

Maafisa wanasema benki kuu imeuza tani 29 za dhahabu, sawa na dinari milioni 1.7 ($ 1.4 bilioni, £ 875 milioni) wakati bado ikidhibitiwa na na Kanali Gaddafi.

Akiba hiyo iliuzwa kwa wafanya biashara wa wenyeji kati mwezi April na Mei na fedha hizo zilitumika kulipa mishahara, maafisa wa utawala wa muda wa Baraza la Mpito (NTC).

Mazuo hayo yanawakilisha asilimia 20 ya akiba yote ya dhahabu ya Libya, govana wa muda wa Benki hiyo Qassim Azzuz aliwaambia waandishi wa habari mjini Tripoli.

Hakuna mali yoyote isiyohamishika ambayo ‘haionekani au kuibwa’ wakati wa miezi sita ya machafuko na vita ambayo imemuondoa Kanali Gaddafi madarakani, Bw Azzuz alisema, lakini hesabu hiyo haikujumlisha mali iliyokuwa mikononi mwa familia ya Gaddafi.

Baraza la Mpito (NTC) linasema watu walioshuhudia nchini Niger wanaripoti kuona kiasi cha dhahabu na fedha katika msafara uliovuka mpaka na Libya siku chache zilizopita.

"Ikiwa hilo lilitokea, tunataka fedha hizo zirudishwe " Afisa mmoja wa NTC Fathi Badja alisema akinukuliwa na shirika la habari la AFP.

Niger itaambua baadaye iwapo itamkubali Kanali Gaddafi au imkabidhi kwenye mahakama ya kimataifa ya Uhalifu wa Kivita The Hague, waziri wa mambo ya nje ameiambia BBC.

Kumekuwa na uvumi kuwa Kanali Gaddafi anaweza kwenda Niger baada ya kundi linalomuunga mkono kukimbilia huko siku za karibuni.

Baraza la Mpito nchini Libya limeiomba Niger kutomkubali Kanali Gaddafi.

Niger inaitambua mahakama ya ICC, ambayo inatafuta kumkamata Kanali Gaddafi, mwanawe Saif al-Islam, na mkuu wa zamani wa usalama Abdullah Sanussi.

Kanali Gaddafi amekiambia kituo cha televisheni cha Arrai kilichoko Damascus nchini Syria, hakukuwa na kitu kisicho cha cha kawaida kuhusu msafara ulioingia Niger.

Hata hivyo, katika mahojiano na BBC Jumatano, Waziri wa Mambo ya Nje wa Niger Mohamed Bazoum alikiri kuwa maafisa wa serikali ya zamani ya Gaddafi ni kati ya watu waliovuka mpaka kuingia Niger katika misafara mitatu, lakini Kanali Gaddafi wala watoto wake hawakuwemo katika msafara huo

UTEUZI WA BINGU WA MUTHARIKA WAKOSOLEWA



Upinzani wa Malawi umemkosoa Rais Bingu wa Mutahrika (pichani) kwa kumteua mkewe kwenye baraza la mawaziri na kumpandisha cheo kaka yake.

Siku ya Jumatano, Bw Mutharika alimteua mke wake, Callista, kuwa waziri wa masuala ya wanawake na ukimwi.

Amemhamisha kaka yake, Peter, kutoka wizara ya elimu na kumweka kwenye wizara ya mambo ya nje.

Kubadilisha baraza hilo kumefanyika baada ya watu 19 kuuawa kwenye maandamano ya kuipinga serikali mwezi Julai.

Walioandaa maandamano hayo walimpa muda Bw Mutharika mpaka Septemba 21 awe ameshafanya mabadiliko.

Mkuu wa upinzani wa Malawi Congress Party (MCP), John Tembo, alisema anatia shaka uteuzi wa Bi Mutharika na Peter Mutharika kwenye baraza hilo la mawaziri.

Bw Tembo alisema, " Rais bado anahitaji kujieleza kwanini mke wake na kaka yake wako kwenye baraza la mawaziri kabla ya kuanza kumshutumu kwa kupendelea ndugu."

"Pia amewabakiza mawaziri wengi waliotoka kwenye eneo lake la asili ambalo nalo ni kosa."