Tuesday, September 13, 2011

300 WAFA KATIKA MILIPUKO YA MAFUTA KENYA NA CONGO DRC

ZAIDI ya watu 330 wamefariki dunia  katika matukio mawili ya kulipuka kwa mafuta ambapo tukio la kwanza liliua watu100 nchini Kenya.Habari kutoka Jijini Nairobi zilisema watu hao walifariki baada ya bomba la mafuta kulipuka na kusababisha moto uliosambaa na kuwaunguza watu wengi.

Wakati hali ikiwa ya majonzi nchini Kenya, nayo Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo(DRC), ilipata pigo baada ya watu 230 kuteketea kwa moto kufuatia tukio la lori lililobeba mafuta kulipuka nchini humo.Moto huo uliua watu hao na wengine wengi kujeruhiwa  na kwamba vyombo vya usalama vya nchi hiyo vilikuwa kikiendelea kuokoa watu wengine.
Habari zaidi kutoka Kenya zilisema mlipuko wa bomba la mafuta ulisababisha moto mkubwa  katika eneo la viwanda mjini hapo, na kuwaunguza watu wengi ambao miili yao hadi sasa haijatambuliwa.  Hata hivyo, Jeshi la Polisi nchini humo lilisema idadi ya vifo inatarajiwa kuongezeka na kuwa zaidi ya 100.  Waandishi wa Gazeti  Mama la Mwananchi, Daily Nation, waliokuwapo eneo la tukio, waliwahesabu watu 73 ambao walikuwa wamefariki dunia.

 Mashuhuda walisema, bomba hilo la mafuta  ya petroli linatumiwa kusafirisha mafuta katika nchi za jirani na Kenya.   Habari zinasema, licha ya vikosi vya zimamoto kuendelea kuuzima moto huo kwa kasi, miili ya watu wengi iliharibika vibaya.  Idadi kubwa ya majeruhi walipelekwa hospitalini na magari ya dharura ambayo yalikuja kwa wingi baada ya tukio hilo.  Habari zaidi za matukio hayo soma ukurasa wa 14.

Chanzo: Gazeti la Mwananchi

WAZANZIBAR WAENDELEA KUPOKEA RAMBIRAMBI

CHADEMA NA CRDB WAKABIDHI RAMBIRAMBI ZAO 

 MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akipokea mchango wa Fedha shilingi milioni tano kutoka kwa Mwenyekiti wa Chama cha Chadema Freeman Mbowe, kwa ajili ya Waathirika wa ajali ya Meli iliotokea usiku wa tarehe 9-9-2011 katika bahari ya Nungwi. 
 MAKAMU wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi akitowa shukrani kwa msaada uliotolewa na Chama cha CHADEMA Tanzania.
 MWENYEKITI wa Chama cha Chadema Freeman Mbowe akitowa rambirambi za Chama chake kwa wahanga wa ajali ya meli alipofika Ofisi ya Mamaku wa Pili wa Rais kutowa rambimrambi jana
 MKURUGENZI wa Masoko wa Benki ya CRDB Tanzania Tully Esther Mwambapa akimkabidhi cheki ya shilingi Milioni kumi. Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa ajili ya waathirika wa janga la ajali ya meli ilioyotokea Nungwi
MKURUGENZI wa Masoko wa Benki ya CRDB TanzaniaTully Esther Mwambapa akitowa salamu za rambirambi kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

16 waenda Afrika Kusini katika Mashindano ya Guinness Footabal Challenge

WAKONGWE WA SOKA OKOCHA, DESAILLY, SONG NA BWALYA KUWANAO PAMOJA KATIKA GUINNESS FOOTBALL CHALLENGE

Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) Epraim Mafuru akizungumza katika mkutani na waandishi wa Habari Dar es Salaam juzi juu ya timu nane ambazo zina mashabiki 16 wa mpira wa miguu wanaokwenda nchini Afrika Kusini katika mashindano ya Guinness Football Challenge. Timu hizo zinaondoka Septemba 13, 2011 leo. Pamoja nae anaeonekana Kulia ni Meneja wa Chapa ya Guinness, Maurice Njowoka.
Meneja wa Chapa ya Guinness, Maurice Njowoka (kulia) akifafanua jambo kuhusiano na mashindano hayo. Pamojanae ni Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) Epraim Mafuru.Vijana hao walipatikana katika mchujo maalum wiki iliyopita katika viwanja vya Leaders Club na vijana hao wanatarajia kurejea nchini September 26,2011 na wakiwa huko mbali na kufundishwa soka la kimataifa pia watashiriki katika kuandaa matangazo mbalimbali ya GFC.
Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) Epraim Mafuru (katikati) akizungumza katika mkutani na waandishi wa Habari Dar es Salaam na kuwataja wachezaji wakongwe wa Afrika watakao kuwa na vijana hao kwa nyakati tofauti Afrika Kusini kuwa ni Jay Jay Okocha, Kalusha Bwalya, Marcel Desailly na Rigobert Song.  Pamoja nae Mkurugenzi wa Mahusiano na Mawasiliano wa SBL, Teddy Mapunda na meneja wa chapa ya Guiness,Maurice Njowoka

Monday, September 12, 2011

EWURA YASHUSHA TENA BEI YA MAFUTA


Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imeendelea kushusha bei za mafuta, safari hii petroli katika Jiji la Dar es Salaam yatakuwa yakiuzwa kwa Sh2,031 katika kipindi cha wiki mbili zijazo ikilinganishwa na Sh2,070, bei ambayo iliishia kutumika jana.

Ewura imekuwa na utaratibu wa kukokotoa na kutoa bei elekezi ya mafuta kila baada ya wiki mbili na hiyo mpya itaanza kutumika leo.Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo alisema katika mabadiliko hayo bei ya petroli imeshuka kwa Sh38.03 sawa na asilimia 1.84, dizeli Sh45.15 sawa na asilimia 2.26 na mafuta ya taa bei imeshuka kwa Sh46.15 sawa na asilimia 2.33.

Kutoka na mabadiliko hayo, bei ya dizeli kwa Dar es Salaam itakuwa Sh1,954 ikilinganishwa na Sh1,999 na mafuta ya taa yatauzwa kwa ni Sh1,933 yakiwa yameshuka kutoka Sh1,980.“Bei za rejareja kwa aina zote za mafuta zimeshuka ikilinganishwa na bei zilizoanza kutumika kuanzia tarehe 29 Agosti, 2011 kwa viwango mbalimbali,” alisema Kaguo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kushuka kwa bei hizo ni matokeo ya matumizi ya kanuni mpya ya ukokotoaji iliyoanza kutumika rasmi Agosti Mosi, mwaka huu.

Kaguo alisema mabadiliko ya bei yametokana na kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia ambako Petroli imeshuka kwa asilimia 2.54, dizeli asilimia 3.78 na mafuta ya taa kwa asilimia 3.50.

Hata hivyo, Kaguo alisema bei za mafuta katika soko la ndani zingeshuka zaidi iwapo thamani ya Shilingi ya Tanzania isingeendelea kushuka dhidi ya Dola ya Marekani ambayo hutumika kununulia bidhaa za mafuta kutoka soko la dunia. Alifafanua kuwa katika kipindi hicho, thamani ya shilingi ya Tanzania imeshuka kwa asilimia 0.20 ikilinganishwa na Dola.

Faida za kanuni mpya za ukokotoaji
Akizungumzia faida ya matumizi ya kanuni mpya, Kaguo alisema bei za rejareja zingepanda zaidi endapo kanuni ya zamani ingeendelea kutumika.“Kama tungeendelea na mwendo ule, badala ya kushuka hadi Sh2,031 kwa petroli, bei hiyo ingepanda hadi kufikia Sh2,205 na dizeli ingepanda hadi kufikia Sh2,126 badala ya Sh1,954 wakati mafuta ya taa bei yake ingepanda hadi kufikia Sh2,108 badala ya Sh1,933,” alisema.

Agosti 2, mwaka huu Ewura ilitangaza kushusha bei ya mafuta ambayo petroli ilishuka kwa Sh202.37 kwa lita ambayo ni sawa na asimilia 9.17, dizeli ilishuka kwa Sh173.49 ambayo ni sawa na asilimia 8.32 na mafuta ya taa yalishuka bei kwa Sh181.37, sawa na asilimia 8.70.

Uamuzi huo uliibua mvutano kati ya wamiliki wa kampuni za mafuta na Serikali baada ya wafanyabiashara hao kugoma kuuza nishati hiyo muhimu.Lakini Agosti 10, mwaka huu Serikali ilitoa saa 24 kwa kampuni hizo za mafuta kurejea kutoa huduma hiyo mara moja na bila masharti huku ikizitaka kujieleza ni kwa nini zisichukuliwe hatua za kisheria kwa kukiuka agizo halali la Serikali.

Ewura baadaye ilitoa onyo kwa kampuni zilizogoma za Engen, Camel Oil, Oilcom na BP. Kampuni tatu zilitii agizo hilo isipokuwa BP ambayo iligoma hatua ambayo ilisababisha mkurugenzi wake mkuu kushtakiwa kwa kutotii amri hiyo.

Siku kumi na moja baada ya kushusha bei hizo, Ewura ilipandisha tena bei kwa kile ilichoeleza kuwa ni kuporomoka kwa shilingi na kupanda kwa bei ya nishati hiyo katika soko la dunia kabla ya kushusha bei hizo wiki mbili zilizopita hadi kuishia jana

SBL yazindua mpango wa Maombi kwa ajili ya ufadhili wa masomo kupitia EABL Foundation 2011

Mkurugenzi wa Uhusiano na Mawasilino wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) Teddy Mapundaakionesha fomu ambayo wa wanafunzi wanaotaka kupatiwa ufadhili wa kusomeshwa kupitia kampuni hiyo chini ya taasisi ya EABL Foundation kwa mwaka 2011 kwa wanahabari jijini Dar es Salaam leo wakati wa uzinduzi wa mpango huo wa maombi ya ufadhili wa masomo ya elimu ya juu nchini.
Mkurugenzi wa Uhusiano na Mawasilino wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) Teddy Mapunda (katikati) akizungumza katika mkutano na waandishi wa Habari juu ya kuanza mchakato wa kupata wanafunzi ambao SBL itawapa udhamini wa kimasomo katika Vyuo vya elimu ya Juu nchini. Pamoja nae kushoto ni Meneja Mahusiano ya Jamii wa SBL,Nandi Mwiyombela na Meneja Mawasilano ya ndani ya SBL Imani Lwinga.
Mkurugenzi wa Uhusiano na Mawasiliano wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) Teddy Mapunda akifafanua jambo kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo juu ya kutangaza kuanza kwa kupokea maombi ya wanafunzi wasio na uwezo ili kupata ufadhili wa kampuni hiyo katika vyo vya Elimu ya Juu nchini.

Sunday, September 11, 2011

SALHA ISRAEL NDIYE MISS VODACOM TANZANIA 2011


Hatimaye kitendawili cha "Nani Vodacom Miss Tanzania 2011" kilichokuwa kikigonga vichwa vya wadau wengi wa urembo sasa kimetenguliwa baada ya Miss Ilala 2011, Salha Izrael kunyakua taji la Vodacom Miss Tanzania 2011.

Salha ambaye nyota yake ilianza kungaa tangu kuingia katika kambi hiyo na kuanza minong'ono ya hapa na pale kuwa ndiye anaestahili kuvaa taji hilo alitawazwa kuwa malkia mpya waTanzania baada ya kuwabwaga warembo wengine 29 katika shindano hilo lililofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo.

Salha mrembo aliyeanza harakati zake za Vodacom Miss Tanzania katika kitongoji cha Dar City Centre na kubahatika kunyakua nafasi ya pili kitongojini hapo na baadae kunyakua taji la Ilala. 

Pia mrembo huyu naweza kumuita Miss Chalinze 2011 baada ya vijana wengi wafanyao biashara katika njia panda ya Segera na Morogo pale Chalinze kumtabiria kuwa mshindi baada ya kumuona wakati wa safari ya kutembelea mbuga za wanyama Kanda ya Kaskazini. 

Kwa Ushindi huo wa kuamkia leo Salha amefanikiwa kuvaa taji Miss Tanzania 2011 alilokuanalo Genevieve Mpangala na kujipatia zawadi ya gari aina ya Jeep lenye thamani ya Tsh 72milioni pamoja na kitita cha Sh Milioni 8.

Nafasi ya pili ilikwenda kwa Trace Mabula ambaye pia anashikilia taji la Miss Photogenic na nafasi ya tatu ikienda kwa Miss Pesonality 2011, Alexia Willium.
Warembo waliofanikiwa kuingia hatua ya 5 bora ya Vodacom Miss Tanzania 2011 wakiwa katika picha ya pamoja. Kutoka kushoto ni Miss Sports Woman, Loveness Flavian, Miss Photogenic Tracy Mabula, Jenifa Kakolaki, Miss Personality, Alexia Willium na Salha Izrael

JK ATANGAZA SIKU TATU ZA MAOMBOLEZO, AAHIRISHA SAFARI YA KWENDA CANADA



Kufuatia msiba mkubwa uliotokana na ajali ya kuzama kwa meli ya Spice Islander katika bahari ya Hindi usiku wa kuamkia jana, Jumamosi, Septemba 10, 2011, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, ameamuru maombolezo ya kitaifa kwa muda wa siku tatu kuanzia leo tarehe 11 Septemba, 2011 ambapo bendera nchini zitapepea nusu mlingoti.

Aidha, kufuatia msiba huo, Mheshimiwa Rais, ameahirisha ziara rasmi ya kiserikali ya siku tatu nchini Canada ambako alikuwa amealikwa na Gavana Mkuu wa nchi hiyo, Mheshimiwa David Johnston.

Katika ziara hiyo iliyokuwa ifanyike kuanzia tarehe 14 – 16 Septemba, 2011, Mheshimiwa Rais angekutana pia na Waziri Mkuu wa nchi hiyo Mheshimiwa Stephen Harper. Mheshimiwa Rais ameiomba Serikali ya Canada kupanga ziara hiyo kwa tarehe za baadaye.