Friday, September 23, 2011

WAHARIRI WAPIGWA MSASA KUHUSU HAKI ZA BINADAMU


Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. George Masaju akifungua semina ya Wahariri wa Vyombo vya habari nchini iliyolenga kuwafahamisha kuhusu kusaidia kuandika habari juu ya haki za binadamu. Semina hiyo imeandaliwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa nchini. Kulia ni Mkurugenzi wa Masuala ya mahusiano ya Katiba na Haki za Binadamu kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Mathew Mwamu.
Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Bw. Alberic Kacou hotuba ya Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. George Masaju wakati wa Ufunguzi wa Semina ya siku moja ya wahariri wakuu wa vyombo vya habari (TANZANIA EDITORS' FORUM) iliyofanyika katika hoteli ya Double Tree by Hilton jijini Dar es Salaam.
Wahariri Wakuu wa Vyombo mbalimbali vya habari nchini wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa na watoa mada katika Hoteli ya Double Tree By Hilton jijini Dar es Salaam.
Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Bw. Alberic Kacou akibadilishana mawazo na Mhariri wa Makala wa Gazeti la Serikali la kila siku (Daily News) Deogratius Mushi.

Watanzania wafanya vyema GFC Afika Kusini


Na Mwandishi Wetu TIMU ya Tanzania inayoshiriki kwa mara ya kwanza kwenye mashindano ya kujibu maswali na kupiga mipira yanayojulikana kama Guinness Mpira Chanagmoto yanayoendelea huko Johannesburg Afrika Kusini, wamefanya kufuru isiyotegemewa baada kuongoza mapaka hatua ya tano hapo juzi. 
Kinyang’anyiro hicho kinachoshirikisha jumla ya washiriki 50, 16 wakiwa ni Watanzania na waliobaki ni washiriki wa Kenya na Uganda, kinaendelea hadi hapo kesho kitakapofikia mwisho wa hatua la nane. 
Mpaka jana kabla ya hatua ya sita timu ya George Lukuba na Freddy Jordan ndio waliokuwa vinara kwa kujinyakulia kiasi kizuri cha pesa. Vijana hao walishinda katika hatua za tatu na nne za kinyang’anyiro hicho wakati Sultan Mohamed na Mansoor Seif walikuwa wapili baada ya kina Lukuba. 
Vijana hao wa Kitanzania ambao walionekana kuyumba katika hatua ya mazoezi yaliyofanyika kwa siku mbili katika studio za kisasa za Q ( Q-Studios) zilizopo huko Kew, mpakani na kitongoji cha Alexandra ambacho ni cha pili kwa kukaliwa na Wazalendo wengi wa asili ya Kiafrika baada ya Soweto kwa jiji la Johannesburg, wamewashangaza waandaazi wa changamoto hiyo ya mpira wa miguu. 
Watanzania hao wamekuwa wepesi kujibu maswali na kupiga mipira na kuwabwaga Waganda ambao walianza kwa mbwembwe nyingi wakati wa mazoezi.
Lukuba amesema wao nia yao ni lushinda kuvuta fuba (pesa) hayo yanayotolewa na watengenezaji wa kinywaji cha Guinness ambacho kinasambazwa na Kampuni ya bia ya Serengeti hapa nchini. 
Vijana hao walifanyiwa usaili wiki mbili zilizopita katika viwanja vya Leaders Club jijini Dar es Salaam, walipanda ndege kuelekea Johannesburg siku ya Jumanne wiki liyopita. Jumla ya hatua nane zinashindaniwa katika kinyang’anyiro hicho ambacho kina toa dola elfu hamsini kila hatua. 
Lukuba ambaye tuliwasiliana naye moja kwa moja jana alisema ndoto ya washiriki wa Kitanzania ni kuendela kuvuta pesa ili kuubwaga umasikini na kuwatoa nishai wenzao wa Kenya na Uganda ambao wamekuwa wakiwabeza kabla ya mashindano kuanza. 
Changamoto hiyo ya Guinness itaoneshwa na televisheni inayopendwa na watazamaji wengi nchini, ITV kwa wiki nane mfululizo. Washindi wa hatua zote nane watajiunga na wanasoka wannne waliostafu soka katika onyesho ambalo pia litashirikisha watazamaji ambao watatuma ujumbe mfupi wa maandishi kupitia simu zao za mkononi kujaribu bahati yao ya kuvuta pesa hapo baadaye. 
Wachezaji hao ni Jay Jay Okocha wa Nigeria, Rigobert Song wa Cameroon, Kalusha Bwalya wa Zambia na Mfaransa Marcel Desaily aliyekuwa beki mahiri wa timu ya Chelsea na Ufaransa iliyoshinda kombe la Dubnia mwaka 1998. Desaily kwa sass anaishi Accra, Ghana. Hii imekuwa fursa pekee kwa Watanzania kujiongezea kipato kupitia onyesho hilo. 
Labda habari za kusikitisha ni kuhusu mshiriki mmoja wa Kitanzania Juma Nassoro ambaye anaumwa jipu juu ya paja lake la kushoto ambalo limepasuka na anaendelea vizuri. 
Mshiriki mwingine wa Uganda Daniel Elagon amebanwa na malaria tokea siku ya Jumamosi wakati wa hatua ya mwanzo ambapo kulikuwa na baridi kali jijini Johannesburg. Shindano hili la Guinness limekuwa likifanyika katika nchi za Ghana na Cameroon pia Kenya na Uganda walikuwa washiriki kwa mara ya kwanza mwaka jana na hii ni mara yao ya pili. 
Washiriki hao wanatarajiwa kurejea Dar es Salaam siku ya Jumapili kwa ndege ya shirika la ndege la Afrika Kusini saa moja jioni.

Malinzi Mwenyekiti Mpya BMT


Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Dkt. Emmanuel John Nchimbi (Mb) amemteua Bw. Dionis Malinzi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
Aidha pia amewateua wafuatao kuwa Wajumbe wa Baraza la Michezo la Taifa.
    1. Mhe. Jenister Mhagama (Mb)
    2. Mhe. Mkiwa A. Kimwanga (Mb)
    3. Bw. Jamal Rwambow
    4. Bw. Venance Mwamoto
    5. Bw. Juma Pinto
    6. Dkt. Cyprian Maro
    7. Bw. Kanali Eliot Makafu
    8. Bibi Jeniffer Mmasi
    9. Bw. Ramadhani Dau
    10. Bw. Alex Mgongolwa
    11. Bw. Maulid Kitenge
Wengine ni Wajumbe wa kuteuliwa kutokana na nafasi zao:
Mkurugenzi Mkuu - Bodi ya Michezo ya Kubahatisha
Kamishna wa Elimu - Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
Mwakilishi - TAMISEMI
Mkurugenzi wa Michezo – Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.
Mwakilishi - Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Wajumbe kutoka Wawakilishi wa Vyama vya Michezo (Makatibu) ni:
CHANETA - Chama cha Netiboli Tanzania
TPC - Tanzania Paralympic Committee
AAT - Automobile Association of Tanzania
TSA - Tanzania Swimming Association
BFT - Boxing Federation of Tanzania
RT - Riadha Tanzania
TFF - Tanzania Football Federation
TBF - Tanzania Basketball Federation
TOC - Tanzania Olympic Committee
TTTA - Tanzania Table Tennis Association
 
Uteuzi huu umefanywa kwa kuzingatia Mamlaka ya Waziri chini ya kifungu cha 3(2) cha nyongeza ya Katiba ya Sheria ya BMT Na. 12 ya mwaka 1967 na marekebisho yake katika Sheria Na. 6 ya mwaka 1971.
Wajumbe hao watalitumikia Baraza kwa kipindi cha miaka mitatu.
Imetolewa na Wizara ya Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo
22.09.2011

Thursday, September 22, 2011

PINDA AFUNGA KLINIKI YA KANISA TARIME


Waziri Mkuu Mizengo Pinda akifungua kliniki ya mama na mtoto katika kituo cha afya cha kanisa Katoliki jimbo la Musoma cha Masanga wilayani Tarime. Alikuwa katika ziara ya mkoa huo Septemba 21,2011.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akisalimiana na Sister Maria wakati alipowasili kwenye misheni ya Kanisa katoliki ya Masanga wilayni Tarime  akiwa katika ziara ya mkoa wa Pwani Septemba 21,2011.
Wasanii wa Tarime wakicheza ngoma maarufu ya Eritungu wakati Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipohutubia mkutano wa hadhara katika Misheni ya kanisa Katoliki ya Masanga  akiwa katika zaira ya mkoa wa Mara, Septemba 21,2011.

YANGA ,AZAM SAFI SIMBA YAVUTWA MKIA

Mshambuliaji wa Yanga, Kenneth Asamoah (kushoto) akijaribu kuwatoka mabeki wa Villa Squad wakati wa mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa jana kwenye Uwanja Azam Chamanzi jijini Dar es Salaam.Yanga ilishinda 3-2. Picha na Jackson Odoyo.
Mwandishi Wetu
MABINGWA watetezi Yanga wamewanyuka Villa Squad pungufu kwa mabao 3-2 kwenye Uwanja wa Chamazi huku vinara wa ligi Simba wakilazimisha sare ya 3-3 na Toto African jijini Mwanza.Wakati Yanga wakipata ushindi wao wa pili na kufikisha pointi tisa, matajiri wa Chamazi, Azam wenyewe wamesogea hadi nafasi ya pili kwenye msimamo kwa kufikisha pointi 14 na kuisogelea Simba inayoongoza kwa pointi 15 baada ya kupata sare ya tatu katika mechi saba.

Macho ya wengi yalikuwa Uwanja wa Chamazi, ambapo Yanga ilipokuwa na kibarua kizito mbele Villa Squad waliokuwa wa kwanza kupata bao kupitia Nsa Job, lakini mabingwa hao walisawazisha kupitia Haruna Niyonzima na Kenneth Asamoah na Hamis Kiiza waliongeza mabao mengine kabla ya Kigi Luseke kuifungia Villa bao la pili na kufanya matokeo kuwa 3-2.

Azam wenyewe wakiwa ugenini itabidi wamshukuru John Boko kwa kuwafungia bao pekee katika mechi dhidi ya Coastal Union akimalizia penalti yake iliyotemwa na kipa.

Katika mechi ya Yanga dhidi ya Villa, nyota wa kimataifa wa Yanga walilipa fadhila kwa kufunga mabao na kumpunguzia presha kocha wao Sam Timbe aliyepewa mechi tatu za kuhakikisha anapata ushindi.

Mshambuliaji Mwape alikosa bao katika dakika ya tano kwa kushindwa kuunganisha krosi ya Ally Shamte iliyotoka sentimita chache kutoka goli la Villa Squad.

Kenneth Asamoah naye alikosa bao baada ya kuunganisha kwa kichwa krosi ya Oscar Joshua na kutoka nje, wakati nyota hao wa Yanga wakikosa Nsa Job alitumia vizuri mwanya wa kipa Yaw Berko kutoka kwenye mstali na kuinua mpira juu na kujaa wavuni katika dakika ya 11.

Dakika nne baadaye Niyonzima aliisawazishia Yanga bao kwa mpira wa adhabu ambao aliupiga na kwenda moja kwa moja wavuni na kufanya matokeo kuwa 1-1.Kocha wa Villa Squad, Said Chamosi alimtoa Haruna Shamte katika dakika ya 24 na kumwingiza Evalist Maganga.

US kusaidia wasanii wa Tamasha la Mtemi Milambo wa Tabora

Wasanii wa muziki wa asili walioshiriki Tamasha la tatu ta Mtemi Milambo mwaka huu lililofanyika Julai 8-10,201 katika viwanja vya Uyui sekondari Tabora na kufunguliwa na aliyekuwa mkuu wa mkoa huo Mhe.Abeid Mwinyimussa wamepata udhamini wa kurekodi nyimbo za muziki wa asili za makabila ya Kisukuma na Kinyamwezi.
Wasanii waliofanya vizuri mwaka huu Ali Mango, Asha Kaombwe,Hamis Mpiga, Paulina Muhala, Paul Magadala wataungana na wasanii wengine wa miaka iliyopita na kuunda bendi ya muziki wa asili iitwayo Mwana Milambo ambayo itakuwa inapiga muziki huo katika mahoteli,maharusi na kumbi mbalimbali za burudani.
 
Nyimbo zitakazorekodiwa ni Kamnyagara kane, Usoga wi kuwa, Kushoke kukaya, kana nabuta, Sensema malunde, Ng,ombe yalala, Wela wa kulya, Nzagamba ya Sukuma na Miaka hamsini ya Uhuru.
 
Lengo kuu ni kuzihifadhi nyimbo mbalimbali zilizotumiwa na wazee wetu wa kale katika vita, kilimo, harusi,na mazishi.
 
Nyimbo hizi nyingi huimbwa sehemu mbalimbali lakini ni muhimu kuzirekodi kwa ajiri ya faida ya vizazi vya baadae.
 
Nyimbo hizo zote zitarekodiwa katika studio ya Aegies chini ya muandaaji maarufu Peter John a.k.a Nice P.

MAKAMU WA RAIS DK. BILAL ASHUHUDIA UTIAJI SAINI MKATABA WA MIRADI YA MAKAA YA MAWE YA MCHUCHUMA NA CHUMA CHA LIGANGA BAINA YA NDC NA KAMPUNI YA CHINA

 

Makamu wa Rais , Dkt. Mohammed Gharib Bilal, (katikati) akishuhudia zoezi la utiaji saini na kubadilishana  mkataba wa miradi ya Makaa ya mawe ya Mchuchuma na Chuma cha Liganga, baina ya Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) na Kampuni ya Sichuan Hongda Corporation Ltd ya China, wakati Mwenyekiti wa Bodi ya NDC, Christant Mzindakaya na Mwenyekiti wa Bodi ya kampuni hiyo, Liu Canglong, wakisainiana mkataba huo katika ukumbi wa mlimani City jijini Dar es Salaam, leo Septemba 21, 2011.
Makamu wa Rais , Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiteta jambo na Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) Christant Mzindakaya, nje ya ukumbi wa Mlimani City Dar es Salaam leo Septemba 21, baada ya kumalizika kwa zoezi la kutiliana saini mkataba wa ya Makaa ya mawe ya Mchuchuma na Chuma cha Liganga, baina ya Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) na Kampuni ya Sichuan Hongda Corporation Ltd ya China.
Makamu wa Rais  Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akipokea zawadi kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya kampuni ya Sichuan Hngda Corporation Ltd, Liu Canglong, baada ya kuhudhulia zoezi la utiaji saini mkataba wa miradi ya Makaa ya Mawe ya Mchuchuma na Chuma cha Liganga, uliofanyika leo septemba 21 kwenye Ukumbi wa Mlimani City Dar es Salaam, baina ya Shirika la maendeleo ya Taifa (NDC) na kamuni hiyo kutoka nchini China.
Makamu wa Rais , Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akitia saini katika Bendera maalum ya kumbukumbu ya watu wa China,  wakati Mwenyekiti wa Bodi ya NDC, Christant Mzindakaya (kulia) na  Mwenyekiti wa Bodi ya kampuni ya Sichuan Hongda Corporation Ltd ya China, Liu Canglong, (kushoto) waliposainiana mkataba wa miradi ya Makaa ya Mawe ya Mchuchuma na Chuma cha Liganga katika  ukumbi wa mlimani City jijini Dar es Salaam, jana Septemba 21, 2011.
Makamu wa Rais , Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisoma hotuba yake wakati alipokuwa mgeni rasmi kwenye utiaji saini mkataba wa miradi ya Makaa ya Mawe ya Mchuchuma na Chuma cha Liganga, baina ya Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) na kampuni ya Sichuan Hongda Corporation Ltd ya nchini China, uliofanyika kwenye ukumbu wa Mlimani City Dar es Salaam.
Makamu wa Rais , Dkt. Mohammed Gharib Bilal, (katikati) akishuhudia zoezi la utiaji saini mkataba wa miradi ya Makaa ya mawe ya Mchuchuma na Chuma cha Liganga, baina ya Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) na Kampuni ya Sichuan Hongda Corporation Ltd ya China, wakati Mwenyekiti wa Bodi ya NDC, Christant Mzindakaya na Mwenyekiti wa Bodi ya kampuni hiyo, Liu Canglong, wakisainiana mkataba huo katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.