Wednesday, April 4, 2012

SIMBA YAWASILI SALAMA NCHINI ALGERIA.

Wekundu wa Msimbazi Simba sports club wamewasili mjini Algiers hivi leo wakitokea jijini Cairo walikokuwa wameweka kituo chao cha siku moja wakiwa njiani, kuelekea kwenye mchezo wa marejeano wa michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika.
Simba, itashuka Stade 8 May 1945 mjini Setif kuwakabili wenyeji Entente Sportive Setifienne ya Algeria, kwenye mchezo wa marejeano wa michuano hiyo, ikiwa na akiba ya ushindi wa mabao mawili kwa sifuri uliopatikana kwenye uwanja wa nyumbani jijini Dar es salaam, siku nane zilizopita.
Taarifa toka mjini humo zinasema kwamba, wawakilishi hao pekee wa Tanzania katika michuano ya kimataifa, wamefika salama na kukaa uwanja wa ndege kwa masaa mawili kabla ya kupokelewa na watanzania wachache waishio mjini Algiers. 

Nae mwenyekiti wa klabu ya Simba Muheshimiwa Ismail Aden Rage ambae ameongozana na timu hiyo pia akiwa mkuu wa msafara anasema kwamba wanasikitika sana kutokana na kuwekwa uwanja wa ndege kwa muda wa masaa mawili.
Aden anasema kwamba, pia wamekuwa na malumbano na wenyeji wao juu ya usafiri wa kutoka mjini Algiers hadi mji utakaochezwa mchezo huo, kwani kutokana na umbali walilazimika wapannde ndege lakini haikuwa hivyo.
Hata hivyo, pamoja na matatizo ya hapa na pale hasa tukio la kuzuiliwa kwa kamera ya mwandishi wa Clouds FM Sports Xtra Geofrey Leah, Aden anasema kwamba jambo hilo amelisimamia kidete ili kuliweka sawa, lakini pia anashukuru kwa mapokezi ya Watanzania wachache waliopo mjini Algiers.

TFF YAIPOKA POINTI YANGA



Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imeipa Coastal Union ushindi wa pointi tatu na mabao matatu baada ya Yanga kumchezesha mchezaji Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kwenye mechi kati ya timu hizo iliyochezwa Machi 31 mwaka huu Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Uamuzi huo ulifanywa na Kamati ya Ligi iliyokutana jana (Aprili 2 mwaka huu) kupitia ripoti mbalimbali za Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza umezingatia Kanuni ya 25(f) ya Ligi Kuu ya Vodacom juu ya Udhibiti wa Wachezaji.

Kanuni hiyo inasema: “Ni lazima kwa klabu na wachezaji kutunza kumbukumbu za kadi. Klabu itakayomchezesha mchezaji mwenye kadi tatu (3) za njano au kadi nyekundu itapoteza mchezo na timu pinzani itapewa ushindi wa pointi tatu (3) na mabao matatu (3), iwapo mchezaji atacheza akiwa haruhusiwi kucheza kwa ajili ya kadi tatu (3) za njano au kadi nyekundu timu yake itapoteza mchezo. Endapo klabu haina uhakika au inataka taarifa ya idadi ya kadi zake itaomba kwa maandishi toka TFF.”

Cannavaro alioneshwa kadi nyekundu kwa kosa la kupiga kwenye mechi kati ya Yanga na Azam iliyochezwa Machi 10 mwaka huu ambapo kwa mujibu wa Kanuni ya 25(c) ya Ligi hiyo anastahili kukosa mechi tatu. Mchezaji amekosa mechi mbili tu.

Pia klabu za Coastal Union na Yanga zimepigwa faini ya sh. 500,000 kila moja kwa washabiki wake kutupa chupa za majini uwanjani wakati wa mechi hiyo. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 32(1).

Kamati ya Ligi pia imemuondoa Kamishna wa mechi hiyo Jimmy Lengwe kwenye orodha ya waamuzi kutokana na upungufu uliopo kwenye ripoti yake ambapo baadhi ya matukio makubwa hakuyaripoti. Moja ya matukio hayo ni kocha wa Coastal Union, Jamhuri Kihwelo kuzozana na mshambuliaji wa Yanga, Hamis Kiiza.

Vilevile waamuzi wa mechi namba 151 kati ya African Lyon na Simba wameandikiwa barua ya onyo kwa kupata alama za chini. Waamuzi hao ni Hashim Abdallah, Abdallah Selega, Hamis Chang’walu na Hassan Mwinchum. Naye Kamishna wa mechi namba 153 kati ya Moro United na Villa Squad, Arthur Mambeta amepewa onyo kutokana na upungufu katika ripoti yake.

SAMATTA KUKAA ZAIDI NJE KWA MAUMIVU YA BEGA


MSHAMBULIAJI chipukizi wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta anaweza kuwa nje ya Uwanja kwa muda zaidi kutokana na maumivu yake ya bega aliyoyapata wiki iliyopita mjini Kitwe Zambia, akiichezea klabu yake Tout Puissant Mazembe dhidi ya Power Dynamos ya huko katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Taarifa kwenye tovuti ya TPM imesema leo kwamba, Samatta akiwa Kenya alilazimika kusimama kwa muda kutokana na kuzidiwa kwa maumivu na hiyo inamaanisha hataweza kucheza mechi ya Jumapili dhidi ya Dynamos.
Samatta aliyefunga bao la Mazembe katika sare ya 1-1 ugenini kwenye mechi hiyo ya kwanza, Raundi ya Pili Ligi ya Mabingwa Afrika, sasa hataweza kucheza mechi ya marudiano Jumapili.
TP Mazemebe imepata pigo linguine, mchezaji wake kufuatia kifo cha baba wa mchezaji wao, Francis Kalala ‘Postolo’, Kasongo Ngongo aliyezaliwa mwaka 1946.

Monday, April 2, 2012

AIRTEL YAANZA SHAMRA SHAMRA ZA SIKUKUU KWA KUSHEREKEA NA WATOTO


 Watoto wa wateja wa kampuni ya Airtel Tanzania wakijumuika kwa pamoja na  watoto  wa wafanyakazi wa Airtel katika shamra shamra tamasha maalum la watoto kuelekea kusheherekea sikukuu ya pasaka kwa michezo mbali mbali kwa pamoja  ambayo imefanyika katika kituo cha michezo ya watoto kiitwacho Fun Sport  ndani ya jengo la Qualty center Jijini Dar-es-salaam kwa hisani ya Airtel.
 Watoto wa wateja wa kampuni ya Airtel Tanzania wakijumuika kwa pamoja na  watoto  wa wafanyakazi wa Airtel kukakata keki iliyoandaliwa na kampuni ya Airtel Tanzania katika shamra shamra za tamasha maalum kuelekea sikukuu ya pasaka ambapo watoto hao walipata nafasi ya kucheza  michezo mbali mbali kwa pamoja  ambayo imefanyika katika kituo cha michezo ya watoto kiitwacho Fun Sport  ndani ya jengo la Qualty center Jijini Dar-es-salaam.
 Meneja mauzo wa kampuni ya Airtel Tanzania Bi.Hilda Nakajumo akikata keki kwa  pamoja na Watoto wa wateja wa kampuni ya Airtel Tanzania na watoto  wa wafanyakazi wa Airtel katika shamra shamra za  kuelekea sikukuu ya pasaka ambapo watoto hao walipata nafasi ya  kucheza michezo mbali mbali kwa pamoja  ambayo imefanyika katika kituo cha michezo ya watoto kiitwacho Fun Sport  ndani ya jengo la Qualty center Jijini Dar-es-salaam.
 Mkurugenzi wa Biashara  wa kampuni ya Airtel Tanzania Bw.Irene  Madeje akizungumza na waandishi wa habari katika sherehe ya michezo kwa Watoto wa wateja wa kampuni ya Airtel Tanzania na  watoto wa wafanyakazi wa kampuni hiyo katika shamra shamra za  kusheherekea sikukuu ya pasaka na kuendeleza uhusiano mzuri uliopo kati ya wateja wa Airtel na wafanyakazi wa Airtel ambapo watoto hao walipata nafasi ya  kucheza  michezo mbali mbali kwa pamoja  ambayo imefanyika katika kituo cha michezo ya watoto kiitwacho Fun Sport  ndani ya jengo la Qualty center Jijini Dar-es-salaam.
Watoto wakicheza mchezo wa kuendesha magari wakati wa tamasha maalum la michezo kwa watoto lilioandaliwa na Airtel ili  kutoa nafasi kwa watoto  wafanyakazi wa Airtel pamoja na watoto wa wateja wa Airtel jijini Dar esa salaam kukutana na kucheza  michezo mbali mbali kwa pamoja, tamasha hilo  lililofanyika katika kituo cha michezo ya watoto kiitwacho Fun Sport  ndani ya jengo la Qualty center Jijini Dar-es-salaam kwa udhamini wa  Airtel .
---
Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel yaanza shamrashamra za sikukuu kwa kujumuika na watoto wa wateja wao jijini Dar es saalam ambapo watoto zaidi ya 150 walipata nafasi ya kukutana pamoja jumamosi mwishoni mwa wiki hii  katika ukumbi wa Quality Center - Fun sports na kufurahi kwa pamoja.
.
Huu ni mkakati ambao Airtel imejiwekea  kusherehekea pamoja na watoto wa wateja wao wa makapuni ( corporate customer)  wiki moja kabla ya sikukuu za pasaka huku lengo likiwa ni kuwa karibu na wateja wao na kusambaza upendo wa kampuni hiyo kwa wateja wake na familia zao.

Akiongea kwa niaba ya Airtel Mkurugenzi wa Biashara wa Airtel Bi Irene Madege alisema" leo tunajisikia furaha kuwa na watoto wa wateja wetu na kujumuika nao pamoja, Tumekuwa tukifanya shughuli mbalimbali ikiwa ni katika kuwazawadia wateja wetu, lakini leo tunatumia muda huu kuwapa burudani watoto ambao ndio wateja wetu wa kesho".

Kwa muda wa takribani masaa 4 watoto zaidi ya 150 walipata burudani mbalimbali ikiwa pamoja na michezo mbalimbali ya watoto kama face painting, mashindano ya kucheza music, na pia kupata nafasi ya kukutana na wafanyakazi wa Airtel,  kumzungumza pamoja na kuwasisitiza watoto kuwa wasikivu shuleni ili  kufanya vizuri kwenye masomo yao, tunaamini watoto hawa wamekuwa na wakati mzuri pamoja nasi. Aliongeza Bi Irene.

Anguko La CCM Arumeru : Tafsiri Yangu


Ndugu zangu,
Unaweza kuwatawanya watu kwa mabomu , lakini kamwe, mabomu hayawezi kuitawanya mioyo ya watu yenye kutaka mabadiliko.

Habari kubwa usiku wa kuamkia leo ni anguko la CCM kuleArumeru Mashariki kwenye kinyang’anyiro cha kuwania kiti cha Ubunge.

Tafsiri yangu;

Kuna wakati Rais Mstaafu Benjamin Mkapa alipata kutamka; " CCM haina hati miliki ya kutawala". Mkapa aliusema ukweli wake ambao kwa bahati mbaya hupata tabu kuusimamia. Na hakika, idadi ya Watanzania wenye kutaka mabadiliko inazidikuongezeka.  Na katika siasa za nchi hiiukiona wanawake watu wazima wanashiriki mikutano ya kampeni ya wapinzani, basi,ujue ni ishara ya mabadiliko yanayokuja.

Na ukweli mwingine ni huu; vijana wengi zaidi wamekuwa mstari wa mbele katika kutakamabadiliko hayo.  Kimsingi ArumeruMashariki wamechagua mabadiliko. Na si kwamba Chadema ni chama bora na makinisana, la hasha, Watanzania wengi zaidi  vijana wanaonyesha kuichukia CCM. Miongonimwao ni Wana-CCM.  Kiukweli, mvuto wa ChamaCha Mapinduzi kwa Watanzania na hususan vijana unazidi kupungua.

Na ajabu ya matokeo ya Arumeru?

Katika hali isiyo ya kawaida, kuna Wana- CCM waliyoyapokeakwa furaha matokeo ya chama chao kushindwa Arumeru. Tafsiri yake?  Ni kushamiri, si tu kwa makundi ndani ya chamahicho, bali, hofu ya kutokea kwa mpasuko ndani ya chama hicho katika mbio zakuusaka Urais ifikapo mwaka 2015.

Kitakachotokea sasa ndani ya chama hicho ni ‘ Witch hunting’-kutafutana uchawi. Bila shaka, kuna maswali yatakayoulizwa. Moja kubwa ni hili;kimeshindwa chama  au mgombea? Na msukumowa swali hilo ni katika kumtafuta mchawi na kukitenganisha chama na mgombeakatika ‘Anguko la Arumeru’.  Huo utakuwani mwendelezo wa ‘ Vita vya Panzi’ ndani ya CCM. Lakini, katika siasa, kunawanaoamini pia, kuwa wakati mwingine kuna lazima ya kuwepo kwa ‘ Vita vya Panzi’ili kujitenganisha na kumbikumbi.

CCM ifanye nini?

Jibu; ifuate njia ya Dr Harrison Mwakyembe

Akizungumza na mamia ya wananchi wa Kata ya Ipinda  hivi majuzi Dr Mwakyembe alitoa kwa watu wake kauli ya ‘ Kichifu’ na iliyojaa hekimana busara. Alisema; “ Mimi sikubaliani na mtu yeyote anayesema kitu cha kwanzani chama  chako…. Hapana, mimi kitu chakwanza  kwangu siyo CCM , cha kwanza mimini Mtanzania, cha pili ndio tunaingia kwenye vyama. Mtu anayekimbilia chamakuwa cha kwanza hivi hicho chama kingetokea wapi kama siyo taifa?”. ( Dr HarrisonMwakyembe, Nipashe, Machi 31, 2012)

Na nilimwona na kumsikia Dr. Mwakyembe akiyasema hayo kwenyeruninga.  Umati ule uliomshangilia DrMwakyembe ulikuwa wa wananchi bila kujali itikadi zao. Kulikuwa na Wana -Chademapia, na kiongozi wa Chadema alipewa kipaza sauti kuongea kumkaribisha ‘ ChifuMwakyembe’ aliyerudi nyumbani na mtazamo mpya wa kizalendo.

Kuifuata njia ya Mwakyembe itawasaidia CCM kurudishaumaarufu wao. Maana,  moja ya sababu za wananchiwalio wengi kuichukia CCM ni hulka yake ya kuwabagua wapinzani na kuwaona niwatu wasiofaa kushiriki uongozi wa nchi.

WaTanzania wengi sasa wanatambua, kuwasi kweli wapinzani ni watu wabaya. Ni maadui. Kwamba watasababisha vita navurugu. Wananchi wameona pia kazi njema inayofanywa na upinzani. Ghiliba hii yaCCM kuwachonganisha wapinzani kwa wananchi imepitwa na wakati. Badala yake,inachangia kupunguza kura za CCM.

Na CCM isipobadilika sasa, na Chadema ikabaki kama ilivyosasa bila kusambaratika, basi, CCM  itakuwa na wakati mgumu sana ifikapo 2015,maana, kuna ‘Jeshi kubwa’ la vijana linalojiandaa na kushiriki uchaguzi wa2015.  Jeshi hili linaundwa na vijanawengi wasio na ajira wala hakika ya maisha yao ya kesho. Wanaiona CCM kamasehemu ya matatizo yao. Wana kiu ya kumpata mkombozi.



Na wanafunzi hawa wa Shule za Kata wamegeuka kuwa ‘agitators’ wazuri wa mabadiliko. Ikumbukwe, shule za kata ziko vijijini. Sikuhizi hata  waliokuwa wakiitwa ‘ wajinga’wa vijijini wamepata walimu wa kuwafungua macho. Watoto wao wenyewe wanaosomaau waliomaliza shule za kata na kubaki vijijini kwa vile hata uwezo wakujisomesha elimu ya juu hawana. Hawa hawana mapenzi na CCM.

Na katika vijana mia moja hii leo, utapata kazi kubwakuwapata 20 wanaoipenda CCM. Huundio ukweli wa hali halisi. CCM ibadilike na kuwa chama cha kisasa kilichotayari hata kuongoza nchi pamoja na wenzao wa upinzani. Yumkini jitihada za CCMkuangamiza upinzani zaweza kuwa na madhara makubwa endapo CCM itapata bahatimbaya ya kuondolewa madarakani 2015. Maana, anguko hilo laweza pia kumaanisha kifo cha chama hicho.
 
CCM haipaswi sasakufikiria mikakati ya kuangamiza upinzani ili watawale daima. Dhana ya ’ CCMDaima’ ni ndoto iliyopitwa na wakati. Katika Tanzania ya sasa kuna wengi wenyekuombea  kubaki hai na kushiriki kuzifutandoto kama hizo.

CCM ya sasa inapaswa kupanga mikakati yakuendelea kuongoza dola huku ikishirikiana hata na wapinzani. Ingawa hata huoni mtihani mgumu wenye kukihitaji chama hicho kuwa na watu makini zaidi badalaya waendekeza fitina na majungu.

Na hii ni tafsiriyangu.

Maggid Mjengwa,
Iringa
0788 111 765
http://mjengwablog.com

Watanzania waanza vema katika South Africa Fashion Week


Mwanamitindo mahiri Millen Magese akiwapungia mkono washabiki wake waliokuwa wakimshangilia wakati akiingiaa katika onesho hilo la mavazi ya Afrika Kusini. 
 Mwanamitindo ambae matunda yake yameanza kuonekana mapema Anastazia Gura akitengenezwa nywele kabla ya kupanda jukwaani.
Mwanamitindo Anastazia Gura akipita mbele ya watazamaji walioshiriki katika onesho la wiki ya mavazi ya Afrika Kusini jana usiku wakati alipokuwa akionesha  mavazi yaliyobuniwa na mbunifu mkubwa wa mvazi ndani na nje ya Afrika Kusini, Olive Clandle.

Wabunifu wa mavazi wa Tanzania wakiwa wamepozi katika picha pamoja na Olive Clandle muda mfupi baada ya kumalizika kwa onesho la mbunifu huyo.
********
MWANAMITINDO Anastazia Gura aliyechaguliwa na mbunifu  mkubwa wa mavazi wa Afrika Kusini Olive Clandle kuonesha mavazi yake ameeleza kufurahishwa na hatua hiyo.  Anastazia akihojiwa na waandishi wa habari wa hapa Afrika Kusini alisema kuwa akiwa kama mwanamitindo chipukizi kuchaguliwa kuonesha mavazi ya mbunifu huyo ni hatua kubwa kwake.
 Alisema kuwa kwa kitendo cha kuchaguliwa bila hata ya kuonekana katika jukwaa ni dhahiri kuwa anavya vigezo vya kutosha na hivyo amepania kufika mbali zaidi.  Anastazia alichaguliwa mara tu baada ya kuonekana akijaribisha nguo za wabunifu wa kitanzania wanaoshiriki katika onesho hilo la wiki ya mavazi.
 Alifika nchini Afrika Kusini kwa lengo la kuonesha mavazi ya wabunifu watatu wa kitanzania waliochaguliwa na mwanamitindo wa kimataifa Millen Magese.  Lakini hata hivyo alijikuta akichaguliwa kuonesha na mavazi ya mbunifu Olive Clande huku akiwa ndio kwanza anaingia katika tasnia ya uanamitindo huku akiwa hajawahi hata kutembea jukwaani.
 Hatua hiyo imeonekana kuwashangaza waandishi wa habari wa mitindo na hata wanamitindo wengine waliopo hapa Afrika Kusini kwa kuwa mara zote mbunifu huyu hupendelea kuwatumia wanamitindo wenye majina makubwa.
 Akizungumzia hatua hiyo Millen alisema kuwa Anastazia na vigezo vyote vinavyotakiwa kuwa mwanamitindo na ndio maana ameweza kupatiwa nafasi hiyo kirahisi.  “Ni kwamba ili uweze kuchaguliwa inatakiwa angalau uwe na vigezo vya kimataifa ili kumwezesha mbunifu kuchagua mtu wa kumuoneshea nguo zake” alisema Millen.

Mbunge Arumeru Mashariki ni Joshua Nassari wa CHADEMA




MGOMBEA Ubenge Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) amewashinda wagombea wenzake saba kutoka vyama vya CCM, AFP, DP, NRA, SAU, UPDP na TLP katika uchaguzi mdogo wa Ubunge uliofanyika Aprili 1, 2012.

Kwa Mujibu wa Matokeo ya liyotangazwa asubuhi hii yanaonesha kuwa Mgombea Ubunge wa Joshua Nassari CHADEMA amepata kura  32,972, na kumshinda Mgombea mpinzani wake mkuu katika uchaguzi huo, Sioi Sumari wa Chama cha Mapinduzi (CCM) aliyepata kura 26,757.

Kwamatokeo hayo inafanya kuwa idadi ya Kura zilizompa ushindi  Nassari wa Chadema kuwa kura 6,215 dhidi ya Sioi Sumari CCM.

Msimamizi wa huo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Wilaya ya Arumeru Bw Gracias Kagenzi amemtangaza mgombea wa CHADEMA Bw Joshua Nassari kuwa mshindi.

Gagenzi pia ametangaza matokeo ya wagombea wengine ambao walitoka vyama vya Siasa nchini kuwa kama yafuatavyo:-
AFP – 139, DP -77, NRA – 35, SAU – 22, UPDB – 18 na TLP – 18.

Kwa mujibu wa Bw Kagenzi zaidi ya watu 120,000 walijiandikisha na aliojitokeza na kupiga kura walikuwa 60,696 ambapo kura halali zilikuwa 60,038 na zilizoharibika ni kura 661.

Aidha CHADEMA pia jana katika Uchaguzi wa Udiwani imepata Ushindi katika Kata za Kirumba mkoani Mwanza na Kiwira mkoani Mbeya.