Saturday, August 2, 2014

HATIMA YA COMRED WAMBURA NI KESHO MKUTANO MKUU SIMBA SC, AGENDA 13 ZAANIKWA HADHARANI!

                   

P 14
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
KLABU ya Simba sc inatarajia kufanya mkutano mkuu wa wanachama kesho Agosti 3 mwaka huu katika ukumbi wa Police Officers Mess Oysterbay, jijini Dar es salaam.
Mkutano huo wa kwanza kufanyika chini ya viongozi wapya wanaoongozwa na Rais Evans Elieza Aveva na makamu wake Geofrey Nyange ‘Kaburu’ utafanyika ukiwa na agenda 13 za kujadili.
Agenda inayotarajia kuwa moto wa kuotea mbali ni ile ya wanachama  72 waliosimamishwa na kamati ya utendaji akiwemo aliyekuwa mgombea wa Urais  Komred, Michael Richard Wambura.
‘Kidume’ Wambura alisimamishwa uanachama wake mwaka 2010 kutokana na kosa la kuipeleka klabu mahakamani.
Wanachama wengine 69 wanakabiliwa na kosa kama hilo kwani waliipeleka klabu mahakamu kuu wakitaka kusimamishwa kwa uchaguzi mkuu uliofanyika juni 29 mwaka huu kwa madai kuwa katiba ilikiukwa.
Agenda ya kwanza katika mkutano wa kesho ni kuhakiki wanachama wanaohudhuria mkutano na agenda ya pili ni kuthibitisha Agenda za mkutano huo.
Agenda ya tatu katika mkutano huo utakaotoa hatima ya Wambura ni kuthibitisha kumbukumbu za kikao kilichopita na Agenda ya nne ni Yatokanayo na kumbukumbu ya kikao kilichopita.
Agenda ya tano ni hotuba ya Rais wa Simba, Evans Aveva na agenda ya sita ni kupokea na kujadili taarifa kutoka kamati ya utendaji.
Agenda ya saba ni kuthibitisha bajeti ya mwaka ya klabu, wakati agenda ya nane  ni kuthibitisha uteuzi wa wakaguzi wa hesabu wa nje.
Agenda ya tisa ni kuthibitisha walezi na wadhamini wa klabu, wakati agenda ya kumi ni marekebisho ya katiba.
Agenda ya 11 inayotarajiwa kuwa ya vuta ni kuvute ni ile kuhusu wanachama 72 waliosimamisha na kamati ya utendaji.
Baada ya hapo, agenda ya 12 ni wanachama wa heshima na agenda ya 13 na ya mwisho ni kufunga kikao

AFCON 2015: MALAWI NA RWANDA ZAFUZU HATUA YA MAKUNDI KWA PENATI

other
 
MALAWI wamefuzu hatua ya makundi ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za mataifa ya Afrika, AFCON 2015 nchini Morocco baada ya kuifunga Benin kwa mikwaju 4-3 ya penalti.
Mechi iliyopita mjini Cotonou, Malawi walifungwa bao 1-0 na leo wakiwa nyumbani wamepata ushindi wa aina hiyo, hivyo sheria ya mikwaju ya penalti kutumika kuamua mshindi.
Bao pekee la ushindi kwa Malawi liligungwa na John Banda katika dakika ya 13.
 Malawi ambao wapo nafasi ya 16 kwa nchi za Afrika katika viwango vya FIFA walitawala mchezo kwa muda mrefu, lakini walishindwa kupata mabao mpaka penalti zikaamua.
Benin ndio walikuwa wa kwanza kulishambulia lango la Malawi, lakini nyota wake Stephane Sessegnon alikosa nafasi kadhaa na kuipa Malawi kupata faida ya ushindi kwa penalti.
Baada ya ushindi huo, Malawi watakabiliana na nchi za Mali, Ethiopia na Algeria kwenye kundi B.
Wakati huo huo, Rwanda nao wamefuzu hatua ya makundi kwa mikwaju ya penalti baada ya kufuta kipigo cha mabao 2-0 walichopata ugenini dhidi ya Congo-Brazzavile.
Mabao mawili ya Rwanda yalifungwa kipindi cha pili kupitia kwa Ndahinduka Michel katika dakika 55 na Meddy Kagere katika dakika ya 60 na kuipa nchi hiyo ushindi.

Rwanda walishinda penati 4-3 na Patrick Sibomana alifunga penati ya ushindi na sasa wanaungana na mabingwa watetezi Nigeria, Afrika kusini na Sudan katika kundi A.

AZAM YAILIPA SIMBA SC MILIONI 60 USAJILI WA KAPOMBE, MNYAMA NAYE AKILIPA KITUO CHA MOROGORO MILIONI 9

                   

kapombe6
Kapombe akiwa Ufaransa kabla ya kurudi nchini
SHOMARY Kapombe alishakamilisha usajili wake wa kujiunga na mabingwa wa ligi kuu soka Tanzania bara, Azam fc na ataitumikia klabu hiyo msimu ujao wa ligi kuu na ligi ya mabingwa barani Afrika.
 Kapombe alisajiliwa na Azam kutoka klabu ya AS Cannes ya Ufaransa ambapo aliuzwa na Simba chini ya uongozi wa Ismail Aden Rage.
 Katika mauzo ya kapombe, kulikuwa na kipengele cha Simba kupata asilimia kadhaa kama mchezaji huyo atauzwa klabu yoyote duniani.
 Baada ya Kapombe kuuzwa Azam, Simba walitakiwa kulipwa milioni 60 kama mkataba unavyoelekeza.
IMG-20140802-WA0008
Makamu wa Rais wa Simba sc, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ (kushoto) akimkabidhi Hundi kiongozi wa kituo cha Morogoro Youth Academy
Kulikuwa na mvutano wa kulipwa fedha hizo, lakini Azam wameamua kumalizana na Simba ambapo jana waliipa klabu hiyo ya Msimbazi milioni 60 baada ya kumnunua Kapombe.
 Lingine kubwa zaidi, jana simba imewakabidhi ‘Morogoro youth Football academy’ milioni 9 kama share ya kituo kwa mauzo ya Mchezaji shomari Kapombe.
 Wakati simba inamsajili Kapombe kutoka kwenye kituo kulikuwa na makubaliano ya kuwapa 15% on ward sale.
 Hiki ni kitendo cha kuigwa na klabu nyingine zenye utaratibu wa kuchukua wachezaji vijana

Friday, August 1, 2014

SIMBA SC YAMTAMBULISHA RASMI ELIAS MAGURI NA SHABAN KISIGA ‘MALONE’

                    

NYANGE
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
SIMBA SC imewatambulisha wachezaji wawili iliyowasijili majira haya ya kiangazi kwa mujibu wa mahitaji ya kocha mkuu, Mcroatia Zdravko Logarusic.
Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ amesema zoezi la usajili linakwenda vizuri na amewatambulisha Shaaban Kisiga `Malone` aliyesajiliwa kutoka Mtibwa Sugar na Elias Maguri kutoka Ruvu Shooting.
“Zoezi la usajili bado linaendelea kwa kuwa muda unaruhusu. Zoezi hili linaendelea kwa taratibu na kwa umakini, wengine wanaweza kusema kuna ucheleweshaji au ugoigoi, usajili ni jambo makini linalohitaji kufanywa kwa umakini mkubwa,” alisema Kaburu.
“Zoezi hili linakwenda vizuri na kamati ya usajili inafanya kazi kwa ukaribu sana na benchi la ufundi kupitia mwalimu wetu mku,”
“Na leo hii tumekuja kuwatambulisha rasmi wachezaji wawili ambao simba imewasajili,”
“Mchezaji wa kwanza ni Shaban Kisiga, uwezo wake mnaufahamu, ni mchezaji wa kimataifa, alishachezeaSimba huko nyuma, akaenda kimataifa na akarudi Mtibwa na kusaini miaka miwili na sasa anarudi nyumbani. Mchezaji wa pili ni Elias Maguri kutoka Ruvu Shooting”.
Baada ya kutambulishwa, Shaaban Kisiga kwa apande wake alisema:
“Nashukuru kwa kurudi klabu yangu ya Simba, nawashukuru viongozi na kocha. Nina imani nitafanya vizuri na kuisaidia timu.”
Kwa upande wake Maguri alisema: “Ninashukuru kujiunga na Simba, najua ni timu kubwa yenye changamoto nyingi, kazi yangu sio kuongea bali ni vitendo uwanjani.”
Elias Maguri amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia klabu ya Simba.

Rais Kikwete awasili Washington kuhudhuria Mkutano wa Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali wa Amerika na Africa (US-Africa Leaders summit

  
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na baadhi ya maafisa waliofika kumpokea wakati akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dulles tayari kwa Mkutano wa Viongozi wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Amerika na Africa (US-Africa Leaders summit) uliondaliwa na Rais Barack Obama wa unaotaraji kuanza Agosti 4-hadi 6, 2014, ambao utatanguliwa na mikutano mingine ya maendeleo ya sekta mbalimbali na uwekezaji (2-3 Agosti, 2014) jijini Washington DC. Kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Marekani,Balozi Liberata Mulamula.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Mkewe Mama Salma Kikwete wakisalimiana na baadhi ya maafisa wa Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani wakati walipowasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dulles.PICHA NA IKULU

WAZIRI MKUU ATOA SAA 30, ATAKA KUPATA MAJIBU KUHUSU KIWANDA CHA NYAMA MBEYA

  

*Asema malumbano ya viongozi hayawasaidii wananchi
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ametoa saa 30 na kutaka kupatiwa majibu ni kwa nini maelekezo aliyotoa kuhusu kiwanda cha kusindika nyama cha Mbeya hayajafanyiwa kazi.

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Ijumaa, Agosti Mosi, 2014) wakati akizindua Kongamano la siku tatu la Uwekezaji la Mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya la mwaka 2014 ambalo limeanza leo kwenye ukumbi wa Benjamini Mkapa jijini Mbeya.

“Mbeya inaweza kuwa na fursa kubwa ya viwanda vya usindikaji nyama, unga wa mahindi ili kuongeza thamani ya mazao mnayozalisha katika mkoa wenu. Nilipokuwa hapa ziara yangu ya mwisho 2012, niliagiza kiwanda hiki kitafutiwe mwekezaji ili kianze uzalishaji. Jana nimeuliza kiwanda cha nyama kimefikia wapi, naambiwa watu bado wanaongea. Wanaongea nini?,” alihoji.

“Mtu akija kusikia habari ya kiwanda hiki atatuona ni wajinga tena ni wajinga wa kujitakia, kisa watu bado wanazungumza… hiki kiwanda cha nyama ni cha Mbeya na manuafaa yake ni kwa ajili ya wana Mbeya. Hivi wahusika ni kwani hamuioni hiyo fursa?” alisema.

“Dk. Mary Nagu watafute watu wa CHC waje hapa kujieleza ni kwa nini suala hili limechukua muda mrefu. Kabla sijaondoka hapa Mbeya kesho nataka nipate majibu kuhusu jambo hili,” aliagiza.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Waziri Mkuu alisisitiza suala la watendaji wa mikoa na wilaya kuchukulia kwa umakini suala la uwekezaji kwani wasipofanya hivyo wao ndiyo watageuka kikwazo na kukwamisha maendeleo ya wananchi wanaowaongoza.

“Ndugu zangu wa Serikali za mitaa msiwe vikwazo, kuwezi wawezeshaji. Ninyi si watawala bali ni waleta maendeleo kwa jamii. Natoa wito mshirikiane na wafanyabiashara kuharakisha maendeleo ya wananchi mliokabidhiwa kuwaongoza. Acheni kudai hongo, kwani badala ya kuwasadia jamii, mtajikuta ninyi ndo mnakuwa vikwazo vya maendeleo,” alionya.

Alisema Serikali za Mitaa zinapaswa kuwa wawezeshaji na siyo wakwamishaji wa masuala ya maendeleo na ili kufanikisha hilo aliwataka wakuu wa mikoa waanzishe one-stop centre katika ngazi ya mkoa na Halmashauri ili wawekezaji wanapofika katika mikoa yao wasizungushwe na kukatishwa tamaa kwa sababu ya mlolongo wa taasisi zilizopo.
“Uzoefu unaonyesha kuwa baada ya kufanya makongamano kama haya, wawekezaji wengi wanajitokeza lakini katika ngazi ya Mkoa na Halmashauri wanakosa mahali ambapo wanaweza kushughulikiwa na kupata huduma bora kwa pamoja “One Stop Centre”. Hali hiyo huwafanya wakate tamaa.”

“Ninashauri kila Mkoa na kila Halmashauri iweke mfumo mzuri wa kuwapokea wawekezaji hususan kuwa na Mratibu (Focal Point) wa masuala ya uwekezaji ambaye ndiye atakuwa “One Stop Centre” wa kushughulikia wawekezaji wanaojitokeza na kuwahudumia kwa ufanisi bila urasimu. Ni imani yangu kuwa tukifanya hivyo, tutawezesha Kanda hii kuwa kitovu kikubwa cha uwekezaji katika nchi yetu,” aliongeza.
Alisema kila mmoja hana budi kuendelea amani na utulivu wa nchi ili uwekezaji uweze kufanikiwa na kushamiri. “Hakuna uwekezaji endelevu na wenye tija katikati ya fujo na migogoro, na uwekezaji utashamiri pale tu penye amani na utulivu,” alisisitiza.
Mapema, Waziri wa Nchi (OWM-Uwezeshaji na Uwekezaji), Dk. Mary Nagu alisema ili uwekezaji uweze kuwanufaisha wananchi, ni lazima rasilmali za nchi zigeuzwe kuwa bidhaa. “Ukiangalia chuma cha Liganga kipo pale miaka mingi, bila kukigeuza kuwa bidhaa, bado hakiwezi kuwanufaisha wananchi wetu,” alisema. Alisema bila uwekezaji hakuna uchumi, na bila uchumi hakuna maendeleo na bila maendeleo hakuna maisha bora kwa kila Mtanzania.

Katika hatua nyingine, Wakuu wa mikoa ya Mbeya, Iringa na Njombe walipewa nafasi ya kuzungumza na washiriki wa kongamano hilo ikiwa ni pamoja na kuelezea fursa mahsusi zilizomo kwenye mikoa yao.

Mada zitakazowasilisha katika kongamano hilo ambalo kaulimbiu yake ni “Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii katika Nyanda za Juu Kusini” zinahusu fursa za uwekezaji katika sekta za uchumi na miundombinu katika kanda hiyo, fursa za uwekezaji katika sekta za huduma za jamii katika kanda hiyo, fursa za uwekezaji katika kilimo cha mazao ya bustani (matunda, mboga, maua na viungo) na mchango wa taasisi za fedha katika uwekezaji.

Nyingine ni mchango wa sekta binafsi katika uwekezaji, na nafasi ya MKURABITA katika kukuza mitaji ya uwekezaji.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, AGOSTI MOSI, 2014

CHUO CHA CBE CHAZINDUA MAADHIMISHO YA MIAKA 50 JIJINI DAR, WADAU MBALIMBALI WAPONGEZA UBORA WA ELIMU INAYOTOLEWA

  
Mbunge wa Ilala Mh. Mussa Zungu ambaye alikuwa mgeni rasmi wakati wa Uzinduzi wa Maadhimisho ya miaka 50 ya Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam (CBE) akikata utepe kuashiria uzindunzi wa maadhimisho ya chuo hicho kutimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake katika hafla iliyofanyika leo jijini Dar es salaam.
Viongozi mbalimbali waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 50 ya Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam (CBE) wakiangalia moja ya picha ya kumbukumbu ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere iliyopigwa wakati akifungua Chuo hicho Januari, 1965. Kutoka kushoto ni Mkuu wa chuo hicho Prof. Emanuel Mjema, Mh. Musa Zungu (Mb) jimbo la Ilala,Mke wa Waziri Mkuu Mama Tunu Pinda,Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo hicho Prof. Mathew Luhanga na Prof.Eliuta Mwageni Makamu Mkuu wa Chuo Utawala na Fedha.
Viongozi mbalimbali waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 50 ya Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam (CBE) wakiwa katika picha ya pamoja wakiongozwa na Mbunge wa Ilala Mh. Mussa Zungu na Mke wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda (katikati). Nyuma ni bango lenye picha ya kumbukumbu ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere iliyopigwa wakati akifungua Chuo hicho mwaka 1965.
Mke wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Tunu Pinda kwa niaba ya wanafunzi waliosoma katika chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam akizungumza na wadau na wanajumuiya wa Chuo hicho wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 50 ya Chuo hicho jijini Dar es salaam.