Tuesday, April 24, 2012

ZAIDI YA ABIRIA 40 WANUSURIKA KIFO MKOANI MBEYA, BAADA YA BASI LAO KUGONGWA NA KUPINDUKA


Basi aina ya Coaster waliokuwa wakisafiria abiria zaidi ya 40, lenye nambari za usajili T 374 AVR, likiwa limepinduka baada ya kugongwa kwa nyuma na basi jingine la kampuni ya El Saedy lenye nambari T 499 AVG. Tukio lililotokea Aprili 23 mwaka huu saa moja asubuhi eneo la Imezu na Inyala Wilaya ya Mbeya Vijijini.


















Basi la kampuni ya El Saedy lenye nambari T 499 AVG lililohusika katika ajali, baada ya kuligonga kwa nyuma basi aina ya Coaster enye nambari za usajili T 374 AVR ambapo zaidi ya abiria 40 kunusurika kifo. Tukio lililotokea Aprili 23 mwaka huu saa moja asubuhi eneo la Imezu na Inyala Wilaya ya Mbeya Vijijini. 
---

Picha na Habari: Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Abiria zaidi ya 40 wamenusurika kifo baada ya basi waliokuwa wakisafiri aina ya Coaster, lenye nambari za usajili T 374 AVR, kupinduka lilipogongwa kwa nyuma na basi jingine la kampuni ya El Saedy lenye nambari T 499 AVG.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa basi la El Saedy likiwa katika hali ya mwendokasi liliharibika mfumo wa breki kutoka eneo la Mlima Nyoka na kuligonga basi hilo dogo kwa nyuma katika mteremko wa Shule ya Sekondari Imezu, hali iliyopelekea basi hilo dogo kupinduka.

Baada ya Coaster kupinduka basi la El Saedy likiwa bado katika mwendokasi liliendelea na safari, kabla ya dereva kufanikiwa kulichepusha kabla halijavuka reli ya TAZARA katika Kijiji cha Inyala Wilaya ya Mbeya Vijijini.

Aidha baadhi ya abiria katika basi hilo dogo walikuwemo wanafunzi 28, wa kike na kiume wakielekea shuleni majira ya saa moja asubuhi, Aprili 23 mwaka huu katika Shule ya Sekondari Imezu.

Mara baada ya ajali hiyo kutokea baadhi ya abiria walikuwemo katika basi hilo dogo walikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa Jijini Mbeya, ambapo kati yao wamelazwa ili kufanyiwa uchunguzi na wengine wakiruhusiwa kurudi nyumbani.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi wa Mkoa wa Mbeya Barakiel Masaki,hakupatikana kuelezea ajali hiyo ingawa dereva wa basi la El Saedy anashikiliwa na Polisi kwa mahojiano.

Picha na Habari: MbeyaYetu Blog.

YANGA YAOMBA RADHI MKUTANO MKUU


Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga ambaye pia mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF akiwakilisha klabu za Mkoa wa Dar es Salaam, Mohamed Bhinda aliwaomba radhi wajumbe wa Mkutano Mkuu kwa kitendo cha wachezaji wake kumpiga mwamuzi Israel Nkongo kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom dhidi ya Azam iliyochezwa Machi 10 mwaka huu.

Pia alimuomba Rais wa TFF, Leodegar Tenga kutoa msamaha wa adhabu ya kulipa faini iliyotolewa na Kamati ya Ligi ya TFF kwa wachezaji wawili wa Yanga ambao mpaka sasa hawajalipa faini hiyo.

Rais Tenga alimshukuru Bhinda kwa ujasiri alioonesha wa kuomba radhi mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kwa kitendo kile.

Aliongeza kuwa kwa vile yeye ni muumini wa kanuni, na adhabu hizo zimetolewa kwa mujibu wa kanuni hawezi kutoa msamaha, hivyo wachezaji hao walipe faini hizo.

Pia Rais Tenga alisema binafsi haziingilia kamati za TFF katika uamuzi ambao zinafanya kwa vile zina watu waadilifu, na angekuwa yeye binafsi ndiye anayetoa adhabu, angetoa adhabu kali zaidi kwa vile vitendo vya kupiga waamuzi havikubaliki katika mchezo wa mpira wa miguu.

FRANCIS CHEKA NA JAPHET KASEBA KUPAMBANA TENA SIKU YA SABASABA

FRANCIS CHEKA NA JAPHET KASEBA KUPAMBANA TENA SIKU YA SABASABA

Na Mwandishi Wetu

BINGWA wa kick Boxing Japhet  Kaseba amesaini mkataba wa kucheza na Bingwa wa dunia wa ndondi mkanda unaomilikiwa na IBC, Francis Cheka wa Morogoro  katika uzani wa KG 75 utakaofanyika siku ya sabasaba jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa kusaini mkataba huo Kaseba amesema anashukulu kupata mpambano huo na atahakikisha anaonesha uwezo wake wote katika mchezo huo kwani yeye ni bingwa wa mapambano

;Najua mabondia wa hapa bongo wananikwepa sana kwa kuwa nimeshakuwa bingwa wa ngumi za mateke lakini awajui mimi ni bingwa katika mapigano yote alisema Kaseba;

Nitahakikisha naweka kambi ya kutosha na kukata ngebe za cheka ni mtoto mdogo sana katika masumbwi kwa kweli bingwa wa kweli ni Rashidi Matumla ambaye ninamuheshimu mpaka sasa cheka kanikimbia mda mrefu tu tangia tupambane 3 October 2009  ambapo alipewa ubingwa kwa kusingizia mshabiki wangu alikuja kumtupa nje ya uwanja kazi yake yeye anarudiana na Mada Maugo kila siku lakini kwa sasa kakanyaga miwaya zamu yake imefika,

Nae Promota wa mpambano huo Kaike Siraju amesema mpambano huo utakaofanyika Dar es salaam siku ya sabasaba utakuwa ni mpambano ambao aujawai kutokea kwa kuwa mabondia hao wanakubalika na mashabiki wa ndani na nje ya Nchi

Mbali na mpambano huo pia kutakua na mapambano ya utangulizi na burudani mbalimbali ambazo mtatangaziwa baadae.

BAGAMOYO KUWAKA MOTO USIKU WA MKESHA WA MUUNGANO



KWANJA MAALUM KWA AJILI YA MKESHA WA SIKUKUU YA MUUNGANO LINATARAJIA KUUSHIKA MJI WA BAGAMOYO KESHO TAREHE 26.04.2012 NDANI YA CLUB LUSONA ILIYOPO KWENYE HOTELI YA MILLENIUM SEA BREEZE RESORT(OLD POST OFFICE).

KWA MUJIBU WA TAARIFA ZILIZOPATIKANA MJINI BAGAMOYO MCHANA WA LEO KUTOKA KWA MMOJA WA WARATIBU WA BURUDANI HIYO MAALUMU BW.ALBERT KAWOGO, BURUDANI HIYO YA AINA YAKE INATARAJIA KUANZA SAA 3:00 USIKU NA KIINGILIO KITAKUWA 5000/= TU.


TUMEJIZATITI KUTOA BURUDANI YA AINA YAKE KATIKA CLUB HII KWA KUONGEZA NGUFU YA MADJ MAARUFU KUTOKA MOJA YA KITUO CHA REDIO CHA JIJINI DAR ES SALAAM ILI WATEJA WETU WAWEZE KUPATA BURUDANI YA AINA YAKE NA NINAWAOMBA MASHABIKI WA BURUDANI YA DISKO KUJITOKEZA KWA WINGI,ALISEMA KAWOGO.


HII ITAKUWA MARA YA KWANZA KWA BURUDANI KAMA HII KUFANYIKA KATIKATI YA JUMA NDANI YA CLUB LUSONA YENYE UBORA WA AINA YAKE,AMBAYO KWA PAMOJA IMEANDALIWA NA ALBERT KAWOGO(MUKUBWA KAWOGO) WA FREE VOICE INVESTMENT NA KIMKEV ENTERTAINMENT
.

MAFUGULI ASHIRIKI KUUAGA MWILI WA MUASISI WA CHAMA CHA MAPINDIZI WA WILAYA YA CHATO

                                   Waziri Magufuli akitoa salamu za mwisho

 
Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Chato leo ameshiriki kuuaga mwili wa Marehemu Constantine Jaha Misungwi ambaye ni muasisi wa Chama cha Mapinduzi wilayani Chato.
 
Marehemu Misungwi alizaliwa tarehe 01 Julai mwaka 1925 ambapo katika muda mwingi wa uhai wake alikuwa akijihusisha sana na shughuli za kisiasa. Marehemu Misungwi ndiye mwanzilishi wa mji wa Chato na katika nyakati tofauti aliwahi kushika nafasi mbali mbali ikiwamo ya Uenyekiti wa Chama cha Mapinduzi katika mji wa Chato, Udiwani na pia Uenyekiti wa Chamba Cha Mapinduzi katika Jimbo la Biharamulo Mashariki.
Marehemu mzee Misungwu ndiye aliyemshawishi Mheshimiwa Magufuli kujiunga na siasa mnamo mwaka 1990 na baadaye kumchukulia tena fomu za kugombea Ubunge wa Jimbo la Biharamulo Mashariki mwaka 1995 na kushinda kwa mara ya kwanza.
Mmoja ya watoto wa marehemu, Bwana Kaloli ameelezea kuwa baba yake alilazimika kuletwa Dar es Salaam kutokea Chato kwa ajili ya matibabu ya kansa na alilazwa kwa wiki mbili katika Hospitali ya Tumaini kabla ya kuruhusiwa kutoka mnamo tarehe 20 Aprili 2012 lakini hata hivyo mauti yakamfika siku mbili baadaye akiwa nyumbani kwa mwanaye huyo.Mwili wa Marehemu Mzee Misungwi umesafirishwa leo kuelekea Chato kwa mazishi

KANUSHO LA HABARI POTOFU KATIKA TANZANIA DAIMA



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Gazeti la Tanzania Daima la leo Jumapili Aprili 22, 2012 lina  habari katika ukurasa wake wa mbele yenye kichwa cha habari ‘JK alinda Mawaziri’,   inayodai  kumekuwa na mazungumzo baina ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Waziri Mkuu Mhe Mizengo Pinda kuhusu hatua inayopaswa kuchukuliwa dhidi ya mawaziri waliotakiwa kujiuzulu.

Habari hiyo imedai kuwa  Mhe. Pinda anataka mawaziri wanaokabiliwa na tuhuma waondoke ili kuleta uwajibikaji serikalini, lakini, imeendelea  kudai habari hiyo, “Rais Kikwete amesema mawaziri hao waachwe waendelee na kazi zao, kwa kuwa suala hili ni la upepo tu, liachwe litapita”.

Tunachukua nafasi hii kuweka bayana kwamba habari katika hilo hazeti la Tanzania Daima Jumapili si za kweli, bali ni za uzushi na upotoshaji mkubwa.
Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye alikuwa katika ziara ya kikazi nchini Brazil, amerejea jana Aprili 21, 2012 jioni. Hajaonana wala kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu, Mhe. Pinda.

Hivi sasa Mhe. Rais anasubiri kupata taarifa rasmi  kutoka Bungeni Dodoma.

Mhe Rais anawasihi wananchi wasiamini habari hizo za upotoshaji zilizomo kwenye gazeti hilo la Tanzania Daima Jumapili.

Pia ametoa rai kwa wanahabari wasitoke nje ya mstari wa weledi katika kutekeleza kazi zao ili kuendelea kulinda heshima zao binafsi, vyombo wanavyofanyia kazi pamoja na taaluma yenyewe.

Mwisho

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
22 Aprili, 2012

Friday, April 20, 2012

NIMEZAA NA MAREHEMU STEVE KANUMBA-SALMA HAMIDU

 Habari: Mashaka Baltazr wa Global Publisher, Mwanza

SALMA Hamidu, mkazi wa Igogo, jijini Mwanza ameibuka na kudai amezaa na marehemu Steven Kanumba mtoto wa kike aitwaye Treasure Steven Charles Kanumba (2), Ijumaa linashuka na maneno ya kinywa chake.

Akizungumza na mwandishi wetu, Salma anayefanya kazi kwenye Ofisi ya Uwakili ya Law Consultancy jijini Mwanza, alidai alianza kufahamiana na marehemu mwaka 2006 wakati yeye akiwa kwenye Kundi la Nyakato Arts chini ya Mwalimu Joseph.

CHANZO CHA UHUSIANO
Salma akasema kuwa, uhusiano wao uliunganishwa na Mwalimu Joseph ambaye alimpa marehemu namba zake za simu wakati alipopeleka filamu za Machozi Yangu na Siri Yangu kuifanyia uhariri (editing) jijini Dar es Salaam katika studio alizokuwa akifanyia kazi marehemu.

“Marehemu alipoona picha zangu kwenye filamu hizo alivutiwa na mimi katika kuigiza, akaomba namba zangu za simu kwa Mwalimu Joseph,” alisema Salma.

Mrembo huyo aliendelea kuweka wazi kuwa, baadaye Mwalimu Joseph alirejea Mwanza na kumtaka radhi kwa kumwambia alimpa Kanumba namba zake za simu.

SIMU YA KWANZA YA KANUMBA KWA SALMA
“Baada ya wiki mbili nilipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha ni Kanumba. Aliuliza kama huwa nasafirisafiri.

“Nilimjibu si sana kwa sababu nasoma. Wakati huo nilikuwa nasomea kompyuta kwenye Chuo cha English Kingdom Nyakato,” alisema Salma.
Akaongeza: Marehemu alinielewa, lakini akaniomba niwe mwenyeji wake punde atakapokuja Mwanza, nikaridhia ombi lake, alikata simu, lakini tukaendelea kuwasiliana kwa simu kila mara.

Salma alisema mawasiliano yake na Kanumba yalidumu kwa mwaka mmoja bila kuonana ‘laivu’.

Aidha, alidai kuwa siku moja marehemu alimpigia simu akimtaka kujiunga na kundi lake lililopo Dar, akamkubalia lakini tatizo likawa umbali. “Lakini marehemu akaniambia nisiwe na wasiwasi kuhusu hilo,” alisema Salma.

Akizidi kumwaga data za uhusiano wao ulivyoanza, Salma alisema:
 (Salma Hamidu aliyezaa na marehemu Steve Kanumba.)

LAIVU KWA MARA YA KWANZA
“Mwaka 2007, Kanumba aliniita Dar, alinitumia tiketi ya ndege ya Precision Air, kwetu niliaga nakwenda kumsalimia mama mkubwa anayeishi Tabata.

“Nilipofika Dar, nilimpigia simu Kanumba kumtaarifu nimefika, akanitaka tukutane Ubungo Plaza Hotel (Blue Pearl),” alisema Salma.

Pale Ubungo Plaza, marehemu kwa mara ya kwanza alimtamkia lililo moyoni mwake kwamba ametokea kumpenda na akamuomba wawe wapenzi.
“Sikuwa na uamuzi wa haraka, lakini kutokana na ushawishi wake nilikubali, baadaye nilirudi Tabata kwa mama mkubwa.

“Usiku alinipigia simu, akaniomba kesho yake tusafiri kwenda Zanzibar, nilikubali, asubuhi niliaga kwa shangaza tukaenda Zanzibar.

“Tulifikia Bwawani Hoteli. Tulikaa kwa siku tatu na kwa mara ya kwanza nilikutana na marehemu kimwili. Tuliporudi Dar mimi nikarejea Mwanza,” alisema Salma.

KANUMBA PENZI LAKOLEA, ATUA MWANZA
“Baada ya kama miezi minne na siku kadhaa hivi, marehemu alinipigia simu akasema yuko Mwanza, anataka kuja chuoni kuniona. Alikuja akiwa ameongozana na marafiki zake wawili, Credo na Theonist Rutashoborwa.

“Walikuja hadi chuoni, mimi nilitoka tukaenda kukaa kwenye baa ya Shentemba. Ilipofika saa 2 usiku, tukahamia Isamo Hotel,” alisema Salma.

Salma aliendelea kusema kuwa, pale Isamo walipata chakula kabla ya kujitupa kitandani lakini siku hiyo muda mwingi alikuwa akijisikia vibaya, marehemu akamtaka asubuhi akapime.

“Asubuhi nilikwenda kwenye Kliniki ya Dokta Ng’walida, daktari bingwa wa magonjwa ya akina mama na watoto. Vipimo vilionesha nilikuwa na ujauzito wa miezi minne.

“Nilimwonesha marehemu majibu yale, hakuonekana kukubali wala kukataa, lakini baadaye akasema kazi yake haimruhusu kuwa na mtoto wala familia hadi atakaponiambia. 

“Baada ya siku mbili, aliaga kurejea Dar pamoja na marafiki zake. Siku chache baadaye huku nyuma kwa bahati mbaya ujauzito ulitoka, nilikwenda kwa daktari mmoja Nyakato National ambaye alithibitisha hilo. Huo ulikuwa mwaka 2008.

UJAUZITO WA PILI
Salma alisema kuwa mawasiliano na marehemu yaliendelea. Kuna siku alimpigia simu akimtaka wakutane jijini Arusha.

Alipofika alipokelewa na Kanumba mwenyewe kabla ya kwenda kupiga kambi kwa rafiki yake mmoja aliyekuwa akiishi peke yake.

Akasema kukutana kwao kimwili kwa safari hii, ndiko kulimpa ujauzito na hatimaye kujifungua binti anayeitwa Treasure au Tunu.
Arusha waliondoka na ndege hadi Mwanza ambapo walifikia Ladson Hotel, ipo Bwiru na kukaa kwa siku mbili kabla ya kumruhusu kurejea nyumbani kwao Igoma.

Akiwa na ujauzito huo, Kanumba alimtumia nauli akimtaka wakutane mjini Morogoro.

“Nikiwa na tumbo langu, aliniita Morogoro, nilisafiri kwa basi hadi kule, nilifikia kwa shangazi yangu yeye alipanga kwenye hoteli ipo jirani na Kituo cha Mabasi cha Msamvu.

KANUMBA ATOA ONYO
“Kulitokea kutokuelewana kidogo na marehemu kwa sababu ya ujauzito ule, akirejea mazungumzo yake ya awali kuwa, kazi yake haimruhusu kuwa na mtoto wala familia, lakini nilimwambia sina namna ya kufanya kuhusu ujauzito ule.

“Hata hivyo, marehemu alinionya nisimwambie mtu kuhusu ujauzito kuwa ni wa kwake, iwe siri yangu na yake kwa sababu hakutaka habari hiyo ifike kwenye magazeti,”alisema Salma.

Akaongeza: Baada ya hapo, alinipa shilingi 150,000 nikarudi nyumbani Mwanza.

“Nikiwa Mwanza alikuwa akinipigia simu akitaka kujua naendeleaje na tumbo langu na kunitaka nijiandae kwa safari ya Dar, atanitumia tiketi ya ndege.

“Nilisafiri, nilipofika Dar nilimjulisha, akasema tusikae Dar, twende Zanzibar. Kule tulifikia tena Bwawani Hotel. Tulikaa kwa siku nne, kisha tukarejea Dar.
Lakini tukiwa Zanzibar kuna mtu alinipigia simu na yeye akiwepo, alikasirika sana na kuninyang’anya simu, akachukua namba kisha akampigia mtu huyo, waligombana kwenye simu. Aliipasua simu yangu, akaenda kuninunulia nyingine.

“Alikuwa mtu mwenye hasira, hakutaka kusikia unazungumza na simu hasa ikiwa ni sauti ya kiume. Ugomvi huo ulisababisha aikane mimba, akasema namsingizia ni ya mwanaume aliyenipigia simu. Ilifika mahali akasema kila mtu aishi kivyake.

“Hata hivyo, alikuja kuniomba msamaha huku akizidi kunionya kuwa ole wangu nitangaze nina mimba yake.”

Alisema ugomvi wake na Kanumba ulitokana na ujauzito na ilifika mahali Salma alimweleza mama yake ambaye alimlaumu kwa kujiingiza kwenye uhusiano na mwanaume huyo.

MISAADA KUTOKA KWA KANUMBA
Kwa upande wa misaada, Salma alisema akiwa mjamzito, marehemu alimtumia shilingi Milioni mbili na laki mbili kwa ajili ya kununua kiwanja.

Baadaye alimtumia shilingi Milioni moja za kupanga nyumba. Fedha hizo alizituma kupitia Benki ya Standard Chartered Tawi la Mwanza.
Baada ya kutuma fedha hizo, marehemu aliwahi kwenda Mwanza na kufikia kwenye Hoteli ya Ryans Bay. Wakati huo mimba ilikuwa na umri wa miezi saba.

HAKUTAKA KUPIGA NAYE PICHA
Salma anasema: Nilimtaka tupige picha ya ukumbusho akakataa, lakini nilipojifungua alikuja na kumpiga picha mtoto kwa kutumia simu yake akisema, ‘mtoto mama yangu mtupu kwani amefanana naye sana.’

Aliongeza kuwa alipojifungua Kanumba alimtumia shilingi 500,000 za matumizi ya mtoto kupitia simu ya mama yake mzazi na Salma (hakumtaja jina).

Aliendelea kusema kulijitokeza sakata wakati wa kumpa jina mtoto, Kanumba akitaka amwite jina la mama yake, huku Salma naye akitaka kumwita la mama yake, ndipo wakakubaliana mtoto aitwe Treasure au Tunu ili kumaliza mzozo wa kugombea kumwita mtoto jina la upande mmoja.

“Treasure alipofikisha miezi saba alisema nimpige picha nimtumie ili amwone alivyofikia, nilifanya hivyo. Siku moja akaniambia angetunga filamu kuhusu maisha yetu ambayo alipendekeza iitwe My Gift.

“Siku chache kabla ya kifo chake alinipigia simu pamoja na mtoto akisema alitaka kusafiri na asingekuwepo kwa mwezi wote wa Machi mwaka huu, alimsamilia mwanaye. Lakini cha kushangaza siku chache nikapewa taarifa za kifo chake,” alisema Salma.

KWA NINI USIRI?
Salma alisema mpaka sasa anashindwa kuelewa ni kwa nini marehemu alitaka uhusiano wao uwe wa siri. Lakini baadhi ya marafiki zake walikuwa wakifahamu uhusiano huo.

NENO LA MWISHO LA SALMA
“Kanumba kaniacha njia panda, sijui la kufanya, lakini ni vyema kama angemtambulisha mwanaye kwa ndugu zake kuliko hivi sasa ambapo mengi yatazuka kuwa pengine natafuta fedha za marehemu.

“Sijaweka wazi ili nipate chochote, bali nahisi dhambi kuficha kwa sababu huyu mtoto si damu yangu peke yangu.

“Nitakuwa mbaya kwa Mungu kama nisiposema ukweli. Angekuwepo mwenyewe nisingesema kwa sababu yeye ndiye alikuwa kiongozi wa maisha ya mtoto.

“Narudia tena, nina uwezo wa kumlea na wala sihitaji mtoto achukuliwe na kwenda kuishi kwa baba, ila familia ijue kuna damu yao kwangu.

“Kama hawataamini, niko tayari kufika Dar na kupima DNA ili familia ya marehemu ijiridhishe,” alisema Salma.

Hata hivyo, Salma alikiri kufanya kosa la kutowahusisha marafiki wa Kanumba kumtegulia kitendawili hicho na kudai pengine umri mdogo ulichangia. Salma alizaliwa mwaka 1987.

Alisema mtu pekee ambaye watu wanamfahamu na ndiye shahidi wa uhusiano wake na marehemu ni msanii wa maigizo, Ramadhan Malele ‘Swebe’ ambaye alikuwa akiwasiliana naye mara kwa mara.

Salma alisema kabla Kanumba hajafikwa na mauti, yeye aliwahi kukutana na Swebe jijini Mwanza ambapo alimsimulia hali ilivyo na akamshauri kusikiliza matakwa ya marehemu ya kutotoa siri ya kuwepo kwa mtoto huyo.