Friday, September 26, 2014

Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imekamilisha mradi wa kuboresha kituo cha kupokea na kutuma mawasiliano

Afisa Habari wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Bi. Bestina Magutu akiwaeleza waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu kukamilika kwa maboresho ya kituo cha Mawasiliano ya Radio kwa ajili ya usafiri wa anga kilichopo Mnyusi mkoani Tanga, kilichojengwa na kampuni ya JATRON ya Norway, wakati wa Mkutano Uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) leo Jijini Dar es Salaam.Kushoto ni Mhandisi Mkuu toka Mamlaka Hiyo Bi. Valentine Kayombo.

Mhandishi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Bi. Valentine Kayombo akiwaeleza waandishi wa Habari(Hawapo pichani) faida zitakazopatikana kutokana na kukamilika kwa Kituo hicho ikiwamo kuongeza ufanisi wa utoaji huduma za uongozaji ndege, wakati wa Mkutano Uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO) leo Jijini Dar es Salaam.Kulia ni Afisa Habari wa Mamlaka Hiyo Bi. Bestina Magutu.

 Inspeka Mwandamizi Idara ya Udhibiti Usalama wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Bw. Redemptus Bugumula akiwaeleza waandishi wa habari kuhusu ongezeko la marubani wanawake nchini ambao wanafikia Takribani Kumi kwa sasa wakati wa Mkutano Uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) leo Jijini Dar es Salaam.Kulia ni Mhandisi Mkuu toka Mamlaka Hiyo Bi.Valentine Kayombo.

Picha na Hassan Silayo-MAELEZO



Frank Mvungi-Maelezo

Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imekamilisha mradi wa kuboresha kituo cha kupokea na kutuma mawasiliano ya radio zinazotumika katika usafiri wa anga kilichoko Mnyuzi mkoani Tanga.

Mradi huo  uliojengwa na kampuni ya JOTRON ya NORWAY umegharimu Serikali zaidi ya shilingi milioni 200 na ulikabidhiwa rasmi kwa  TCAA mapema mwezi Agosti mwaka huu.

Hayo yamesemwa na Afisa Habari wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Bi. Bestina Magutu wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam.

Magutu alisema kuwa  kukamilika kwa kituo hicho kumeongeza ufanisi wa utoaji huduma za uongozaji ndege na kuimarisha zaidi usalama wa safari za anga hapa nchini.

Akifafanua zaidi Magutu amesema hali hiyo itachangia kuongezeka kwa mapato ya Mamlaka hiyo yanayotokana na tozo la huduma za uongozaji ndege.

Akizungumzia mikakati ya Mamlaka hiyo Magutu amesema inaendelea kuwekeza katika miundo mbinu ya kuongozea ndege hivyo kwenda sanjari na mabadiliko ya teknolojia pamoja na kumudu ukuaji wa Sekta ya usafiri wa anga hapa nchini.

Katika hatua nyingine Mamlaka hiyo imesema kuwa wanafunzi watano waliopewa ufadhili  wa kusomea urubani nchini Afrika ya Kusini wameendelea kupata ufaulu wa juu na kushika nafasi ya kwanza hadi ya tano katika darasa la watu 14 katika shule ya urubani nchini Afrika ya Kusini.
Takwimu za mwaka 2013 zinaonyesha ongezeko la miruko ya ndege ( flight movements) kutoka 222,430 mwaka 2012 hadi kufikia miruko 230,458 sawa na ongezeko la asilimia 3.6 kadhalika katika kipindi hicho idadi ya abiria imeongezeka kutoka 4,056,925 hadi kufikia 4,626,016 sawa na ongezeko la asilimia 14.Idadi ya abiria inatarajiwa kufika zaidi ya milioni 5 kufikia mwishoni mwa mwaka 2014.

Thursday, September 25, 2014

WAREMBO MISS TANZANIA 2014 WATEMBELEAMAKAO MAKUU YA EAC, AICC, AUWSA LEO


 Mkuu wa Wilaya ya Arusha mjini,John Mongela akisalimiana na Warembo wanaoshiriki shindano la Redd’s Miss Tanzania 2014, walipomtembelea ofisini kwake jijini Arusha leo. Warembo hao Septemba 27 wanataraji kupandaa jukwaani kuwania taji la Miss Top Model litakalofanyika jijini Arusha.
 Warembo wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa mAMLAKA ya maji safi na maji taka Jijini Arusha(AUWSA) walipowatembelea leo
 Wakiwasili AICC
Warembo wanaoshiriki shindano la Redd’s Miss Tanzania 2014, wakimsikiliza Ofisa Habari Mwandamizi na Itifaki wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC), Catherine Kilinda aliyekuwa akiwapa maelezo mbalimbali kuhusina na kazi za kituo hicho walipokitembrelea jijini Arusha leo.Aliyevalia suti ni Rodney Thadeus Ofisa Itifaki.
 Warembo wakiwa ndani ya Bunge la Afrika Mashariki (EALA) leo


Washiriki wa shindano la Redd’s Miss Tanzania 2014, wakiwa katika picha ya pamoja huku wakiwa na benbdera ya Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) walipotembelea Makao makuu ya Jumuia hiyo jijini Arusha
Warembo wakisambaza upendo kwa Rodney Thadeus

WIZARA YA AFYA YAKABIDHI MABASI 6 KWA VYUO VYA AFYA NCHINI.

 Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Charles Pallangyo akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kabla ya kukabidhi mabasi 6 kwa wakuu wa vyuo vya Afya kutoka katika maeneo mbalimbali .Mabasi hayo yatasaidia kuaondoa upotevu wa muda na adha ya usafiri waliyokuwa wakiipata wanafunzi,watumishi na wakufunzi  wa vyuo hivyo  kufika kwenye maeneo ya mafunzo kwa vitendo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Charles Pallangyo akikata utepe kwenye basi moja kati ya sita yaliyonunuliwa kwa ufadhili wa Mradi wa Mfuko wa Dunia mzunguko wa 9 ambayo yamekabidhiwa kwa wakuu wa vyuo vya afya leo jijini Dar es salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Charles Pallangyo akikagua mabasi hayo yaliyonunuliwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Dunia mzunguko wa 9 ambayo yamekabidhiwa kwa wakuu wa vyuo  6 vya afya leo jijini Dar es salaam.

SERIKALI KUTATUA TATIZO LA MAKAZI KWA WATUMISHI


Fatma Salum-Maelezo

Serikali imejipanga kutatua tatizo la makazi kwa watumishi wa umma kwa kujenga nyumba Elfu 10 za gharama nafuu kote nchini.

Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Mtendaji Mkuu wa  Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Bw.Elius Mwakalinga wakati wa ziara ya waandishi wa habari katika miradi mbalimbali inayotekelezwa na wakala huo jijini Dar es Salaam na Pwani.

 Mwakalinga alisema kuwa  mradi huo wa nyumba elfu 10 unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 18 unahusisha nyumba za viongozi na watumishi wa kawaida wa kada zote.

“Lengo la kujenga nyumba hizi ni kuwapatia  watumishi wa umma makazi bora jirani na maeneo yao ya kazi ili kuongeza tija katika utoaji huduma kwa wananchi. Mradi huu utawawezesha kupata nyumba za kupanga na  kununua kwa gharama nafuu”.  Alisema Mwakalinga.

 

Akifafanua zaidi  Mwakalinga alisema kuwa fedha za kutekeleza mradi huo zinatokana na ruzuku ya serikali pamoja na fedha za TBA ambapo kwa mkoa wa Dar es Salaam nyumba hizo zimeanza kujengwa kwenye maeneo ya Bunju, Mbezi Beach, Ada Estate na Masaki na pia eneo la Chalinze mkoani Pwani.

 

Aidha Kaimu Mkurugenzi wa Ushauri kutoka TBA Bw. Edwin Nnunduma alisema kuwa ujenzi wa nyumba hizo unatumia teknolojia ya kisasa inayopunguza gharama na muda wa kukamilika.

 

Pia Nnunduma alisema mpaka sasa ujenzi unaendelea vizuri kwenye mikoa mbalimbali nchini ikiwemo mikoa mipya ya Katavi, Geita, Simiyu na Njombe.

 

Naye Meneja wa Kikosi cha Ujenzi cha TBA Mhandisi Wilfred Dungamu alieleza kuwa kwa sasa wakala huo unatumia kikosi cha wahandisi wa ndani kilichoanzishwa mwaka 2012 na mpango huo umesaidia kupunguza gharama kubwa zilizokuwa zikitumika kuwalipa wahandisi kutoka makampuni binafsi.

PATRICK PHIRI LAZIMA AUMIZE KICHWA KUICHAPA POLISI MORO


Kocha mkuu wa Simba sc, Mzambia Patrick Phiri (kulia)

Na Baraka Mpenja, Dar es salaam

0712461976

SIMBA SC inajiandaa kuchuana na Polisi Morogoro katika mechi ya raundi ya pili,  ligi kuu soka Tanzania bara itakayopigwa jumamosi uwanja wa Taifa, Dar es salaam.
Timu hizo mbili zitakutana zikiwa na matokeo tofauti ya mechi za ufunguzi wikiendi iliyopita. Simba walitoka sare ya 2-2 na Coastal Union uwanja wa Taifa, wakati Polisi Moro walitandikwa 3-1 na mabingwa watetezi Azam fc katika uwanja wa Azam Complex.
Kocha Patrick Phiri hakuridhishwa na kiwango cha timu yake na kuamua kwenda Visiwani Zanzibar tena kuwepa kambi ya maandalizi.
Simba kwasasa inaandamwa na majeruhi wengi. Jana kipa namba moja Ivo Mapunda alivunjika kidole mazoezini na atakaa nje ya uwanja kwa wiki nne.
Kuumia kwa Ivo ni pengo kwa kocha wa Simba ingawa ataweza kumtumia kipa bora wa msimu uliopita, Hussein Sharif ‘Casillas’.
Mbali na Ivo, Mkenya Paul Kiongera naye ataikosa mechi ya jumamosi. Bahati mbaya zaidi hata mechi ya watani wa jadi Oktoba 12 mwaka huu atakosekana kutonana na majeruhi sugu ya goti ambayo itamuweka nje ya uwanja kwa takribani wiki sita au miezi miwili.
Mshambuliaji Elius Maguli naye alikuwa anasumbuliwa na majeruhi, lakini kwasasa anaendelea vizuri na anaweza kucheza jumamosi.
Amerudi?: Gerard Jonas Mkude amesumbuliwa na majeruhi ya muda mrefu

Kiungo wa ulinzi, Jonas Mkude naye anaendelea kuimarika baada ya kukaa nje ya uwanjwa kwa muda mrefu akisumbuliwa na majeruhi, lakini hajawahi kucheza chini ya Phiri. Kwa mazingira hayo dhahiri kiungo huyu anahitaji kupata muda wa kurudisha kiwango chake.
Nyota mwingine, Haruna Chanongo atakaa nje ya uwanja kwa siku 10 baada ya kuumia wikiendi iliyopita dhidi ya Coastal Union.
Beki wa kushoto, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ naye ana majeruhi, hivyo hana uhakika wa kucheza mechi ijayo.
Kutokana na majeruhi yanayoiandama Simba, kocha Phiri analazimika kufanya mabadiliko ya kikosi chake.
Ukiangalia kwa umakini unagundua kwa haraka kuwa baadhi ya wachezaji walioumia ni wa kikosi cha kwanza, hivyo itaathiri timu kwa kiasi fulani.
Mchezaji wa kikosi cha kwanza ndiye chaguo la kwanza kwa kocha. Inapotokea tatizo, analazimika kumpanga mbadala wake.
Ivo ni kipa namba moja, Casillas ni kipa namba mbili. Phiri anapomkosa Ivo, analazimika kumtumia Casillas.
Lakini kama Ivo yuko fiti kwa asilimia 100, Mzambia huyo hawezi kumuanzisha Casillas kirahisi.
Pengo?: Kipa Ivo Mapunda (kushoto) akisalimiana na waamuzi kwenye moja ya mechi ya Simba msimu uliopita

Nafasi ya Kiongera ina wachezaji wengi. Bado kuna watu kama Emmanuel Okwi, Amissi Tambwe, Elius Maguli na Amri Kiemba ambao wanaweza kuziba nafasi yake.
Safu ya ushambuliaji, Simba ina wachezaji wengi wanaofanana majukumu, hivyo ni rahisi mwalimu kubadilisha kikosi chake.
Kukosekana kwa Chanongo, Ibrahim Twaha anaweza kupata nafasi ya kucheza, lakini bado utakuwa mpango B wa Phiri. Asingeweza kumchezesha Twaha wakati  Chanongo yupo.
Pengo la Mkude, bado ni gumu kuliziba, Piere Kwizera ameshindwa kukaribia uwezo wa kiungo huyo kijana.
Mechi iliyopita, Kwizera alijitahidi kupiga pasi sahihi, lakini nyingi hazikwenda maeneo sahihi. Alikuwa pole pole kuanzisha mashambulizi pale inapotakiwa na tatizo lilionekana wazi tofauti ambavyo angecheza Mkude.
Simba wanakwenda kucheza na Polisi Morogoro, kikosi kina majeruhi wengi, lakini wanaweza kupata matokeo kama watajipanga vizuri.
Majeruhi ni suala la kawaida katika soka, lakini athari yake ni kubwa na tunaona duniani kote timu zinavyohangaika pale zipoandamwa na tatizo hilo.
Kutumia wachezaji wa mpango B huwa kuna madhara kiufundi. Tumeona hata makocha wa Ulaya kama Arsene Wenger wanavyolalamika wanapokuwa na majeruhi wengi kikosini.
Mchezaji wa ‘Plan B’ huwa halingani na mchezaji wa ‘Plan A’. Siku zote ‘Plan B’ huwa inafanywa kwa kulazimisha kwasababu hakuna jinsi.
Paul Kiongera ni majeruhi

Phiri bila shaka anafanya kazi kubwa ya kuwafanya wachezaji atakaowatumia wajiamini kwasababu itakuwa mechi ya presha kwao.
Wanahitaji kushinda ili kuendelea kuwajengea imani mashabiki wao. Kinachotakiwa ni kuwapanga wachezaji kisaikolojia na waamini wataweza.
Wachezaji wa Simba bila shaka wako fiti katika utimamu wa mwili, ufundi na mbinu, lakini suala la saikolojia linatakiwa kuangaliwa zaidi.
Kikubwa vijana wanatakiwa kukalishwa chini na kuwapa mbinu zaidi ili  wajiamini.
Ugumu wa mechi unakuja kutokana na namna Polisi wanavyocheza. Walifungwa na Azam fc 3-1, lakini walionekana kuwa na hofu kubwa hususani kipindi cha kwanza.
Wachezaji wa Polisi Moro walionekana wazi kutokuwa makini, kutojiamini na wakawaruhusu Azam wacheza mpira katika eneo lao na kushambuliwa zaidi.
Kadri dakika zilivyokuwa zinasonga mbele, walionekana kubadilika na kujiamni. Kipindi cha pili walicheza vizuri, walishambulia na kupata goli moja. Haikuwa kazi rahisi kwao kwasababu walikutana na mabingwa watetezi.
Kocha Adolf Rishard ni mzoefu wa ligi kuu, lazima amewatuliza vijana wake na kuwafanya wajiamini zaidi.
Simba watakutana na upinzani kwasababu tayari Polisi Moro wamejua udhaifu wao, hivyo kocha Adolf ameendelea kuwafundisha nini cha kufanya.
Lakini uwanja wa Taifa utakuwa mgumu zaidi kwa Polisi kutokana na mazingira ya Simba kwa sasa. Timu imewavutia sana mashabiki wake, wanajitokeza kwa wingi, hivyo presha itakuwa kubwa kwa wachezaji wa Polisi.
Lakini kama Simba watawaacha wacheze mpira hususani dakika za mwanzo (20-30) na kushindwa kuwafunga, basi mechi itaweza kuwa ngumu kwao.

Mabao ya mapema huwa yanawaharibia wapinzani . Kama Polisi  watafungwa mapema zaidi watashindwa kucheza mpira na itatakiwa kocha atumie maarifa kuwapanga upya, lakini wakikaza dakika 20-30 za mwanzo, wataongeza kujiamini na mechi itakuwa ngumu kwa Simba.

Tuesday, September 23, 2014

TaSUBa yaaswa kutoa mafunzo ya sanaa na utamaduni ili kukidhi mahitaji ya soko la Afrika Mashariki


 
Benjamin Sawe
Bagamoyo
 
Taasisi ya Sanaa Bagamoyo imeaswa kuendelea kutoa mafunzo ya sanaa na utamaduni  ambayo yatakidhi mahitaji ya soko  kwa nchi za Afrika Mashariki.
 
Hayo yamesemwa na Bw Makongoro Nyerere kwa niaba ya  Spika wa Bunge la Afrika Mashariki Mh. Margaret Ntantongo Zziwa katika Ufunguzi wa Tamasha la 33 la sanaa na utamaduni wa Mtanzania lililofanyika katika Taasisi hiyo mjini Bagamoyo jana

Bwana Makongoro alisema Sanaa na Utamaduni vinaweza  kutumiwa kuelezea masuala yote  yanayomuhusu binadamu na mazingira yake hususani suala zima la utaliii

Alisema ni wakati mwafaka kwa jamii kuondokana na dhana ya kuona watalii ni wale wa kutoka nje ya nchi na kusahau kuwa wale wa ndani ambao kwa idadi kubwa ni wengi wa kuwezesha Serikali kukusanya maduhuli ya kutosha.

Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa TaSUBa Bw. Michael Kadinde alisema sanaa hutumika kuelimisha jamii katika masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na  Utawala Bora, kuhifadhi mazingira, madahara ya rushwa katika jamii, namna ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya  Ukimwi na aina nyingine nyingi za utoaji elimu katika jamii.

Alitolea mfano wa sanaa ya ngoma, nyimbo, hadidhi simulizi, majigambo, uchoraji  na sanaa  nyingine nyingi za makabila mbalimbali vinaeleza  utamaduni wa Mtanzania hivyo  huwa kitambulisho cha jamii.

Bw. Kadinde alisema sanaa huonya na kutaadhalisha jamii juu ya mambo mabaya yanayoweza kuleta madahara katika jamii ikiwa ni pamoja na kuendekeza rushwa, Vijana au jamii nzima kuwa na tabia zisizokuwa  na heshima .

Aliomba Bodi ya Utalii ya Tanzania mahali palipo na vituo vya Utalii viwatumie wahitimu  wa TaSUBa kuanzisha vikundi vya sanaa ili watangaze utalii wa nchi ili na kuongeza mapato ya nchi na jamii kwa ujumla

Alisema kutoa mafunzo ya Sanaa na Utamaduni kwa nchi za Afrika Mashariki kuna changamoto zake ikiwa ni pamoja na upanuzi wa miundombinu ili kukidhi mahitaji ya ufundishaji ambapo iliyopo haiwezi kubeba mzigo mzito wa kutoa mafunzo kwa wanafunzi wa nchi za Afrika Mashariki.

Tamasha la sanaa Bagamoyo lilianzishwa mwaka 1982 ambapo mwaka huu kauli mbiu yake ni “Sanaa na Utamaduni katika kukuza utalii”.

MANISPAA YA ILALA YAJIPANGA KUWA NA BARABARA ZENYE HALI BORA

    Afisa Uhusiano wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala Bi Tabu Shaibu akiwaeleza waandishi wa Habari (Hawapo pichani) waandishi wa Habari kuhusu Miradi iliyotekelezwa kwa ajili ya kupunguza msongamano katika halmashauri hiyo, wakati wa mkutano uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.Kushoto ni Afisa Habari wa Idara ya Habari Bw. Frank Mvungi.
 

     Mhandisi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala Bw. Batimagwa James akiwaeleza waandishi wa habari kuhusu hatua zinazochukuliwa na Manispaa hiyo katika kuhakikisha barabara zinakuwa kwenye hali nzuri katika kipindi chote cha mwaka.kulia ni Afisa Uhusiano wa Halmashauri hiyo Bi Tabu Shaibu
 
HASSAN SILAYO-MAELEZO

 
 
 
 
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kupitia Idara ya Ujenzi inahudumia barabara zenye urefu wa kilomita 536.9 ambazo kati ya hizo kilomita 144.2 ni za lami, kilomita 64.7 ni za Changarawe na kilomita 328 ni za udongo.  Huduma hizi ni pamoja na kujenga, kukarabati na kusimamia sheria za matumizi ya barabara katika eneo la Manispaa ya Ilala.
MIRADI ILIYOTEKELEZWA HADI SASA KWA AJILI YA KUPUNGUZA NSONGAMANO
Ujenzi wa Barabara ya Mazengo hadi Kibasila kwa kiwango cha Lami Km.1.2
Ujenzi wa Barabara ya Lindi kwa kiwango cha Lami Km. 0.7
Ujenzi wa barabara ya Vingunguti  Baracuda- urefu wa 1.3 km unaendelea na tayari mita 880 ziko hatua kuanza kuweka lami nyepesi na lami ngumu. 
UCHONGAJI WA BARABARA ZA UDONGO
Halmashauri imeweza kutekeleza kazi za uchongaji wa barabara za udongo na changarawe kwa kutumia greda lake moja.  Barabara zilizochongwa ni za maeneo ya kata za Ukonga, Pugu, Majohe, Kivule, Msongola, Chanika, Kitunda, Kinyerezi, Tabata, Kimanga, Gongolamboto, Kipawa, Kiwalani, Vingunguti, Upanga Mashariki, upanga Magharibi, Gerezani Ilala, Jangwani, Mchikichini na Buguruni. Barabara hizi zimekuwa zikiharibika wakati wa kipindi cha mvua zinapokuwa nyingi mathalani mvua zilizonyesha katika Mkoa wa Dares Salaam na kuleta maafa. Barabara nyingi ziliharibika kiasi cha kutopitika kabisa hali iliyoathiri huduma mbalimbali.
Kwa kuliona hilo na kuhakikisha kuwa Barabara hizi zinapitika wakati wote Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imenunua Magreda mawili (2) kwa gharama ya Tshs 1.2 billioni. Pamoja na jitihada hizo yapo maeneo mawili ambayo kwa sasa ni kero
ENEO LA HYDARI PLAZA
Eneo hili hujaa maji wakati wa Mvua kutokana na kuwepo kwa Chemba za Maji taka zinazotiririsha maji barabarani na kusababisha mashimo ambayo yamekuwa adha kwa watumiaji wa barabara hiyo. Halmashauri imekuwa ikiziba viraka vya lami bila mafaikio. DAWASCO ambao ndiyo wamiliki wa chemba hizo wametakiwa kuzikarabati chemba zao.  Halmashauri inaendelea na maandalizi ya kuweka zege badala ya lami ili eneo hilo liweze kupitika kwa urahisi.  Kazi hii itafanyika mapema katika mwaka huu wa fedha 2014/2015.
ENEO LA SHULE YA UHURU WASICHANA HADI UHURU MCHANGANYIKO – BARABARA YA LINDI
Eneo hili lilifanyiwa ukarabati wa mfereji wa maji ya mvua ili kuyaingiza katika kalavati kuu lilopo katikati ya barabara ya Mismbazi, kisha lami iliwekwa.  Lakini kufuatia eneo hilo kutumiwa na Daladala za Temeke/Tandika – Kariakoo bila udhibiti wa kutosha wameharibu mferefi huo na kusababisha maji kutuama na kuharibu tabaka lote la lami,  Halmashauri ina kusudia kuujenga upya mfumo wa maji ya mvua na kuweka lami kipande hicho katika mwaka wa fedha 2014/2015.
 
MASHIMO YA BARABARANI
Uchakavu wa barabara za lami hasa maeneo ya katikati ya Jiji (Kata na Gerezani, Kivukoni, Kisutu, Mchafukoge, Jangwani, Kariakoo, Upanga mashariki na magharibi). Hali hii inatokana na barabara nyingi katika maeneo haya kuchoka (kuzeeka) kwani nyingi zilijengwa katika miaka ya 1990. Uchakavu huu unachangia kuwepo kwa mashimo mengi kwakuwa zinaharibika kwa wakati mmoja.
Jambo lingine linalochangia uharibifu wa barabara na kuwa na mashimo ni ukataji ovyo wa barabara kwa lengo la kuweka na kukarabati miundombinu ya maji safi na taka na mikonga ya mawasiliano ya simu. Wakandarasi ambao hurusiwa kufanya kazi hiyo huchukua muda mrefu kurejesha barabara katika hali ya awali. Hali inasababisha maji ya mvua kutuama na kuharibu tabaka la barabara. Halmashauri imekuwa ikiyaziba mashimo hayo kulingana na hali ya upatijanaji wa fedha, Hata hivyo bado hali haijawa bora kwani Barabara hizi zinahitaji matengenezo makubwa ya kuwekwa Lami upya.
 
CHANGAMOTO
·         Uhaba wa fedha za kukidhi mahitaji ya matengenezo mapya na ukarabati wa barabara, madaraja makalavati na mifereji ya maji ya mvua ukilinganisha na ukubwa wa mtandao wa barabara.
·         Ukataji holela wa barabara kwa malengo ya kuweka mifumo ya maji safi, maji taka, mawasiliano (fibre cables), n.k kinyume cha utaratibu ambapo Halmashauri hutoa vibali na kusimamia urejeshaji wa miundombinu iliyoharibiwa.
·         Wizi wa mifuniko ya chemba za maji ya mvua kwa ajili ya biashara ya chuma chakavu. 
·         Utupaji ovyo wa taka na michanga barabarani, hali hii inasababisha kuziba kwa mifereji ya maji ya mvua na kusababisha uharibu wa barabara kutokana na mafuriko, madibwi makubwa ya maji.  Hii ni kero kwa watumiaji wa barabara.
·         Wananchi kuunganisha mfumo wa maji taka ya majumbani kwenda mifereji ya maji ya Mvua.  Hususan katika Kata za Gerezani, Kariakoo, Jangwani, Kisutu na Mchafukoge ambapo baadhi yao wamekamatwa na kutozwa faini na kisha kuziba mifumo hiyo.  Kitendo hiki kinasababisha kuwepo kwa harufu mbaya katika maeneo mbalimbali kwa watumiaji wa Barabara. 
 
Mikakakati
·         Halmashauri inaendele a kuweka mifuniko ya mifereji ya maji ya mvua. Hadi sasa jumla ya mifuniko 410, ambapo 250 imewekwa kwenye chemba zilizo kuwa wazi na 160 ipo kwa ajii ya dharura
·         Kujenga mifereji mipya ya maji ya mvua katika sehemu korofi.
·         Kuunda kitengo kitakachodhibiti uzito wa magari kwa kuweka mizani zinazohamishika katika maingilio yote ya barabara kuu za kuingia katikati ya Halmashauri kwa masaa 24.
 
Imeandaliwa na;
Tabu F.Shaibu- Afisa Uhusiano