Thursday, September 22, 2011

Vodacom Mwanza Cycle Challenge kutimua vumbi mwezi ujao

Meneja udhamini na Matukio wa Vodacom Tanzania Rukia Mtingwa akionyesha nembo itakayotumika katika mashindano ya mbio za baiskeli "Vodacom Mwanza Cycle challenge 2011"zitakazoanzia Shinyanga hadi Jijini Mwanza mnamo tarehe 22 mwezi wa kumi mwaka huu.kulia Mwenyekiti wa chama cha baiskeli cha Mkoa wa shinyanga(Kamwashi) Elisha Eliasi.
  •  Washindi kuzoa zawadi kem kem
  • Makampuni mengine yajitokeze kudhamini mbio hizo
     Shinyanga Septemba 21 2011, Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania imetangaza kuandaa na kuyadhamini mashindano ya baiskeli ya Vodacom Mwanza Cycle Challenge ambayo yamekuwa yenye mvuto wa hali ya juu katika mikoa ya kanda ya ziwa.Mashindano haya yataanzia mjini Shinyanga na kumalizikia Jijini Mwanza mwezi ujao na yatagharimu zaidi ya shilingi milioni 50.

Akizungumza naWaandishi wa Habari,leo/jana, katika uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga Meneja Udhamini na Matukio wa Vodacom Tanzania, Rukia Mtingwa alisema kwamba mashindano ya mwaka huu yameboreshwa zaidi na kuwaomba waendesha baiskeli kujitokeza kwa wingi.

“Mashindano haya yameboreshwa kwa upande wa zawadi, ubora na viwango, na tofauti na miaka ya nyuma, mashindano ya mwaka huu yatahusisha mikoa miwili muhimu kwa mchezo wa baiskeli kanda ya Ziwa, yani Shinyanga na Mwanza”Alisema.

Alisema mashindano hayo yatafanyika tarehe 22 mwezi ujao na kwamba yatakuwa mbio za kilomita 196 kwa wanaume, 80 kwa wanawake, upande wa walemavu ni Kilometa 15 kwa walemavu wanaume na Kilomita 10 kwa walemavu wanawake.

“Washindi katika kila kundi watapewa zawadi mbalimbali ambazo tutazitangaza baadae,”Alisema.

Alifafanua kuwa mashindano ya mwaka huu ya Vodacom Mwanza Cycle Challenge yameandaliwa na kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania kwa takribani miaka mitano na pia Vodacom ina nia ya kuendelea kuandaa na kukuza mchezo huu ili Tanzania iweze kujulikana zaidi kimataifa katika mchezo huu wa baiskeli.


“Shindano hili la Vodacom Mwanza Cycle Challenge ni mahususi kwa kukuza mchezo huu hapa nchini kwa lengo la kupata wawakilishi bora katika mashindano mbalimbali ya kimataifa,”alifafanua.

Katika kuzingatia kuwa mwaka huu Tanganyika inasherehekea miaka 50 ya uhuru, Vodacom Tanzania itatoa zawadi ya mshiriki mwenye umri wa kuanzia miaka 50 atakaemaliza wa kwanza katika kundi la washiriki 50 wa kwanza. Hivyo amewataka Watanzania wenye uwezo kujiandikisha kwa wingi ili kuweza kushiriki na hatimae kujishindia zawadi kem kem.

Nae Mwenyekiti wa Baiskeli Kanda ya Ziwa bwana Elisha Eliya, amesema mwaka huu ili kuleta mabadiliko na kuboresha zaidi mashindano haya, mbio zitaanzia Mkoa wa Shinyanga na kumalizikia Mwanza kwa sababu hii ni mikoa miwili inayoongoza katika uendeshaji wa baiskeli katika kanda hii.

Amewataka wanamichezo wote nchini wanaoshiriki katika mashindano haya kuanza kujiandaa wao pamoja na vifaa vyao vya michezo ili waweze kuwa katika hali nzuri ya kiushindani zaidi.
Ametoa wito kwa washiriki kutoka mikoa yote nchini kujiandikisha kwa wingi na kufika Shinyanga mapema ili kuhudhuria semina ya washiriki wote siku moja kabla ya mashindano.

Bwana Eliya amesema kuwa mashindano ya mwaka huu yatakuwa na ushindani wa hali ya juu kwani njia itakuwa ya moja kwa moja na watahakikisha hakuna mtu atakaeingia kwenye mashindano kati kati ya njia hivyo kupata washindi halali,Na alichukua frusa hiyo kwa kutoa wito kwa makambuni mbalimbali hapa nchini kujitokeza kudhamini mbio hizo.


Vodacom Tanzania imekuwa ikidhamini michezo mbalimbali kama vile Soka, Riadha, kuogelea, mashindano ya boti, mashindano ya Mbuzi, Vodacom Miss Tanzania, Tenisi na mingine mingi ili kuhakikisha kwamba taifa linafanya vizuri katika tasnia nzima ya michezo.

Wednesday, September 21, 2011

MAONYESHO YA PICHA YA "AMRIK" YAFANA JIJINI DAR ES SALAAM.


Balozi wa Umoja wa Falme za nchi za Kiarabu nchini Bw. Mallalla Mubarak Al-Ameri na kiongozi wa Mabalozi wa Kundi la nchi za Kiarabu akisoma hotuba kwa wageni waalikwa katika maonyesho ya Picha yaliyofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee VIP jijini Dar es Salaam.
Balozi wa Brazil nchini Mh. Francisco Luz akizungumza wakati wa kufunga maonyesho ya "AMRIK" yaliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Ubalozi wa Brazil, Taasisi za nchi za Kiarabu  na Aga Khan. Ambapo Balozi huyo amewapongeza walioshiriki maonyesho hayo. Maonyesho hayo yenye lengo la kuhamasisha ushirikiano kati ya Wabrazil na Waarabu yalitarajiwa kufanyika wiki iliyopita lakini yakaahirishwa kufuatia ajali ya kuzama kwa Meli ya MV SPICE ISLANDER iliyotokea huko Zanzibar.Katikati ni Balozi wa Umoja wa Falme za nchi za Kiarabu nchini Bw. Mallalla Mubarak Al-Ameri na kiongozi wa Mabalozi wa Kundi la nchi za Kiarabu na Kushoto ni Mwakilishi wa Mtandao wa Maendeleo kutoka Taasisi ya Aga Khan Bw. Navroz Lakhani.
Mwakilishi wa Mtandao wa Maendeleo kutoka Taasisi ya Aga Khan Bw. Navroz Lakhani ambao ni miongoni mwa wadhamini wa maonyesho hayo akizungumza machache katika hafla ya ufungaji wa maonyesho hayo.
Kutoka kushoto pichani ni Balozi wa Umoja wa Falme za nchi za Kiarabu nchini Bw. Mallalla Mubarak Al-Ameri na kiongozi wa Mabalozi wa Kundi la nchi za Kiarabu, Balozi wa Brazil nchini Mh. Francisco Luz na Makamu wa Balozi Bw. Ronaldo Vieira wakisikiliza hotuba kutoka kwa Mwakilishi wa Mtandao wa Maendeleo kutoka Taasisi ya Aga Khan (hayupo pichani).
Afisa Ubalozi Lucy Mwambungu akiwa katika picha ya pamoja na msanii wa siku nyingi wa michezo ya Kuigiza Christina Manongi maarufu kama Sinta pamoja na Makamu wa Balozi wa Brazil nchini Ronaldo Vieira.
Pichani juu na chini ni wageni waalikwa kutoka Balozi mbalimbali nchini, Taasisi za Kiserikali na zisizo za kiserikali wakifuatilia picha zilizokuwa zikionyeshwa katika maonyesho hayo jijini Dar es Salaam.
Mke wa Balozi wa Brazil nchini Mama Luz akibailishana mawazo na mmoja wa wageni waalikwa.
Balozi wa Marekani nchini Alfonso E. Lenhardt akiangalia picha zilizokuwa zimetandazwa katika maonyesho hayo.
Pichani Juu na Chini ni miongoni mwa wadau mbalimbali kutoka sehemu na Idara Tofauti za ndani na nje ya nchi wakifuatilia matukio yaliyokuwa yakiendelea katika hafla hiyo ya maonyesho ya picha yanayoelezea ushirikiano wa nchi  ya Brazil na zile za kiarabu katika nyanja mbalimbali.

TANZANIA YAPATA TUZO YA DUNIA YA AFYA,TEKNOLOJIA NA MAENDELEO

Rais Jakaya Kikwete akizungumza na Mwenyekiti wa Grameen Bank Bhaban ya nchini Bangladesh Professor Muhammad Yunus mara baada ya kikao cha majadiliano kuhusu wanawake na maendeleo ya kilimo yaliyofanyika huko Nwe York wakati wa kikao cha 66 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 19.9.2011.
Rais Jakaya Kikwete akifurahia tuzo ya Global Health,Technology and Development mara baada ya kukabidhiwa na Mwenyekiti wa South-South Awards 2011 Mheshimiwa Winston Baldwin Spencer, Waziri Mkuu wa Antigua and Barbuda (kulia) katika sherehe iliyofanyika katika hoteli ya Waldorf Astoria jijini New York tarehe 19.9.2011
Rais Jakaya Kikwete akishiriki katika majadiliano na baadhi ya viongozi mashuhuri duniani kuhusu wanawake na maendeleo ya kilimo duniani (Women and Agriculture. A conversation on improving Global food security.) Mkutano ulioandaliwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton katika hoteli ya Intercontinental Barclay jijini New York katika siku ya kwanza ya kikao cha 66 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (United Nations General Assembly) tarehe 19.9.2011.
Rais Jakaya Kikwete akiwahutubia marais na Wakuu wa nchi mbalimbali duniani walioshiriki katika sherehe ya utoaji tuzo hizo wakati wa kikao cha 66 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York nchini Marekani tarehe 19.9.2011.

Matembezi ya Hisani ya Shear Charity Ball Octoba Mosi Dar es Salaam

 

Mkurugenzi wa Kampuni ya Shear Illusions na Mwenyekiti Kamati ya Maandalizi Shear Charity Ball,Shekha Nasser akiongea na waandishi (hawapo pichani) jana jijini Dar es Salaam wakati akitangaza kundi Kundi la wacheza Dansi wa muziki wa Salsa la ‘Mutati Dancers’ toka nchini Kenya litakalo tumbuiza siku ya tafrija ya hisani ya kila mwaka ya Shear (Shear Charity Ball 2011) yenye lengo ya kutunisha mfuko na kusaidia akina mama wenye matatizo ya fistula katika hospitali ya CCBRT na pia kuwezesha ukarabati wa mfumo mzima wa maji safi na maji taka katika hospitali ya Amana.Tafrija hii ya hisani itafanyika tarehe 01 Oktoba kuanzia saa moja kamili jioni katika ukumbi wa Kivukoni, uliopo katika hoteli ya Movenpick,jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Bilicanas Group,Dk. Lilian Mbowe akionyesha moja ya kipeperushi kinachoonyesha shughuli mbali mbali zinazofanywa na kampuni hiyo ambao ni moja ya wadhamini wa tafrija ya hisani ya kila mwaka ya Shear (Shear Charity Ball 2011) yenye lengo ya kutunisha mfuko na kusaidia akina mama wenye matatizo ya fistula katika hospitali ya CCBRT na pia kuwezesha ukarabati wa mfumo mzima wa maji safi na maji taka katika hospitali ya Amana.Kulia ni Meneja Uhusiano wa Precision Air,Annette Nkini.
Mkurugeni wa Kampuni ya Ulinzi ya G4s,Jacqui Bothma (kushoto) akizungumza katika mkutano huo wa maandalizi ya tafrija ya hisani ya kila mwaka ya Shear (Shear Charity Ball 2011) yenye lengo ya kutunisha mfuko na kusaidia akina mama wenye matatizo ya fistula katika hospitali ya CCBRT na pia kuwezesha ukarabati wa mfumo mzima wa maji safi na maji taka katika hospitali ya Amana.Katikati ni Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano na Huduma kwa Wateja wa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF),Theopista Muheta na kulia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Shear Illusions na Mwenyekiti Kamati ya Maandalizi Shear Charity Ball,Shekha Nasser
Meneja Uhusiano wa Precision Air,Annette Nkini akizungumza na waandishi wa habari wakati katika mkutano uliofanyika leo kwenye hoteli ya Peacock iliyopo katikati ya jiji la Dar.Precision Air ni mmoja ya wadhamini wa tafrija ya hisani ya kila mwaka ya Shear (Shear Charity Ball 2011) yenye lengo ya kutunisha mfuko na kusaidia akina mama wenye matatizo ya fistula katika hospitali ya CCBRT na pia kuwezesha ukarabati wa mfumo mzima wa maji safi na maji taka katika hospitali ya Amana.
Baadhi ya waanahabari ambao ni wadau wa Shear Charity Ball wakifuatilia kwa makini mkutano.

Tuesday, September 20, 2011

TBL yachangia waathirika wa ajali ya Meli Zanzibar


Meneja Miradi Maalumu wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Emma Oriyo akikabidhi kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi hundi ya Sh.milioni 10 zilizotolewa na kampuni hiyo kwa ajili ya kusaidia waathirika wa ajali ya Mv.Spice Islander. Hafla hiyo ilifanyika mwishoni mwa wiki mjini Unguja.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi akimshukuru Ofisa Uhusiano wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Dorris Malulu baada ya kupokea mchango wa TBL, wa sh. mil. 10 za kusaidia waathirika wa ajali ya Mv.Spice Islander. Hafla hiyo ilifanyika mwishoni mwa wiki mjini Unguja.Katikati ni Meneja Miradi Maalum wa TBL, Emma Oriyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Mwakilishi wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Zanzibar, Mweidady Mbaga baada ya kupokea mchango wa TBL, wa sh. mil. 10 za kusaidia waathirika wa ajali ya Mv.Spice Islander. Hafla hiyo ilifanyika mwishoni mwa wiki mjini Unguja.Kulia ni Meneja Miradi Maalum wa kampuni hiyo, Emma Oriyo na Ofisa Uhusiano wa kampuni hiyo, Dorris Malulu.

SERENA ATOZWA FAINI KWA KUTUKANA



Serena Williams ametozwa faini ya dola 2,000 na ameepuka kufungiwa mashindano makubwa baada ya kumtolea maneno makali mwamuzi Eva Asderaki katika fainali ya US Open.

Sam Stosur alishinda mchezo huo kwa 6-2 6-3 baada ya Williams kuambiwa amekiuka taratibu kwa kutoa kauli za utovu wa nidhamu.

Williams alikuwa anatumikia muda wa miaka miwili wa kuchunguzwa tabia yake kutokana na kitendo kama hicho alichofanya mwaka 2009.

Tukio hilo lilitokea wakati Williams alipoonekana amefanikiwa kupata ponti lakini neno alilotumia kwa kupaza sauti la "Come on!" akionesha hasira fulani, lilitafsiriwa kwamba alilitoa kabla ya Stosur hajapata nafasi ya kuurejesha mpira kwake.

Pointi na mchezo katika seti ya pili alipewa Stosur na akiwa amekasirika Williams akamtolea maneno makali mwamuzi kutoka Ugiriki Asderaki.

Williams, mwenye umri wa miaka 29, alipewa hundi ya dola milioni 1.4 baada ya kuwa mshindi wa pili.

MAUAJI MAKUBWA YAFANYIKA BURUNDI


                                                                       Rais Nkurinziza
Takriban watu 36 wameuawa baada ya watu wenye silaha wasiojulikana kufyatua risasi kwenye baa iliyojaa watu karibu na mji mkuu wa Burundi, Bujumbura, maafisa wamesema.

Wamesema idadi ya waliofariki dunia inaweza kuongezeka kwani watu wengi wamejeruhiwa vibaya kwenye uvamizi huo eneo la Gatumba.

Kundi la mwisho la waasi la Burundi lilisalimisha silaha zao rasmi mwaka 2009 lakini mashambulio ya hapa na pale yamekuwa yakiendelea.

Mwandishi wa BBC Prime Ndikumagenge mjini Bujumbura amesema ni shambulio baya kabisa kutokea tangu uchaguzi kufanyika mwaka jana.

Aliyekuwa mkuu wa waasi Agathon Rwasa alijitoa kugombea urais na kukimbia baada ya chama chake cha National Liberation Forces (FNL) kuishutumu serikali kwa udanganyifu.

Serikali imelaumu mashambulio ya hivi karibuni kufanywa na magenge lakini mwandishi wetu alisema baadhi wanahofia huenda kundi jipya la waasi limeibuka.

Miili kwenye maegesho ya magari
" Idadi kubwa ya watu, baadhi wakiwa wamevaa sare za kijeshi na bunduki aina ya Kalashnikov na maguruneti yaliingia kwenye baa ya 'Chez les Amis'.

Mmoja aliyenusurika lakini akapoteza ndugu zake wawili na rafiki mmoja aliliambia shirika la habari la AFP, "Walimwambia kila mmoja alale chini na kuanza kupiga risasi."

Daktari aliyetoa jina lake moja la Leonard alisema hospitali anapofanyia kazi "ilizidiwa" na idadi ya majeruhi.

AFP inaripoti kwamba miili ya watu iliachwa kwenye maegesho ya magari katika hospitali moja.

Rais Pierre Nkurunziza alitembelea eneo lilipofanyika shambulio hilo huko Gatumba na kuahidi kuwachukulia hatua kwa wale waliohusika.

Alisema ameahirisha safari yake ya wiki hii ya mjini New York, ambapo kutakuwepo mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Takriban watu 300,000 wanadhaniwa kuuawa nchini Burundi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 12 baina ya Watutsi walio wachache lakini ndio waliokhodhi jeshi na waasi wa Kihutu.

Mapigano hayo yaliisha rasmi mwaka 2005 kwa makubaliano ya amani yaliyomshuhudia kiongozi wa waasi Pierre Nkurunziza kuchaguliwa kuwa Rais lakini waasi wa FNL wameendelea kupigana