



KAMPUNI ya Bia ya Serengeti (SBL), jana ilizindua kampeni ya “Tuko Pamoja Tutashinda” ikiwa na lengo la kuwahamasisha wananchi kuiunga mkono timu ya taifa ‘Taifa Stars’.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi huo Mkurugenzi wa Mawasiliano wa SBL, Teddy Mapunda, alisema kuwa wameamua kuzindua kampeni hiyo ili kuhakikisha Watanzania wanaiunga mkono timu yao.
Stars inakabiliwa na mechi ya kuwania kutinga hatua ya makundi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2014 ambapo itacheza na Chad mechi ya kwanza itapigwa N’Djamena, Novemba 11 kabla ya kurudiana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Novemba 15.
“SBL ambao ni wadhamini wakuu wa Taifa Stars, kwa kutambua umuhimu wa kuiunga mkono timu yetu tumeamua kuzindua kampeni hii ya pamoja tutashinda, kauli mbiu yetu ikiwa In good time and in bad time, we are together and we shall win” alisema Teddy.
Mgeni rasmi katika uziduzi huo alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Dioniz Malinzi, ambaye aliishukuru SBL, kutokana na udhamini wake na kuhamasisha wananchi kuiunga mkono Taifa Stars, lakini akaiomba itupie macho pia katika kudhamini na michezo mingine.
“Hapa nchini kuna kampuni nyingi lakini ni SBL pekee inayothamini kusaidia maendeleo ya michezo, napenda kuchukua fursa hii kuwaomba wamiliki wa kampuni nyingine mbalimbali kujitokeza katika kutoa udhamini wa michezo kwani tunahitaji sapoti ya wapenda michezo ili taifa lipate mafanikio,” alisema Malinzi.
Naye Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga, ametoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi katika kuishangilia Taifa Stars, katika mechi dhidi ya Chad.
Alisema kuwa kampeni hiyo itafanyika pia katika mikoa mingine zaidi ikiwemo Mwanza, Kilimanjaro, Arusha na Mbeya ambapo magari yatakuwa yakipita barabarani huku wakifanya promosheni ya bia ya Serengeti na kutoa zawadi mbalimbali kwa watu watakojitokeza.
No comments:
Post a Comment