Friday, December 7, 2012

BARABARA YA DAR LINDI KUKAMILIKA JUNI MWAKANI


THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

 

 
 
 
 
 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Barabara ya Dar-Lindi kukamilika Juni mwakani

                   Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameambiwa juzi, Jumatano, Desemba 5, 2012, kuwa ujenzi wa Barabara ya Dar es Salaam-Lindi utakamilika katika miezi sita ijayo kuanzia sasa.

                   Rais Kikwete alipewa maelezo hayo na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Mhandisi Gerson Hosea Malangalila Lwenge wakati aliposimama kukagua maendeleo ya ujenzi kwa akiwango cha lami wa kilomita 56 kati ya  Nyamwage, Mkoa wa Pwani na Somanga, Mkoa wa Lindi.

                   Rais Kikwete alisimama kukagua ujenzi wa Barabara hiyo wakati akirejea Dar es Salaam kutoka Lindi ambako alifanya ziara yenye mafanikio makubwa ya siku tatu kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo na kusikiliza changamoto za wananchi.

                   Akipewa maelezo ya ujenzi wa Barabara hiyo kwenye eneo la Somanga, Rais Kikwete aliambiwa kuwa kati ya kilomita hizo 56 tayari kilomita 30 zimeshatiwa lami. Barabara hiyo inajengwa na Kampuni ya MS Karafi.

                   Naibu Waziri huyo alimwambia Rais Kikwete: “Mjenzi anajenga kiasi cha mita 250 kila siku na kama hapakuwepo na kuharibika kwa lolote ama mvua isipokuwa nyingi kupita kiasi, basi ujenzi wa Barabara hii utakuwa umekamilika katika miezi sita ijayo kuanzia sasa.”

                   Naibu Waziri alimwambia Rais Kikwete kuwa ni kweli ulikuwepo ucheleweshaji kwa upande wa mjenzi, lakini sasa maendeleo ni mazuri. Barabara hiyo ilipangwa kukamilika Juni, mwaka jana, 2011.

                   “Kwa jumla ujenzi wa Barabara nzima umekamilika kwa asilimia 78, njia ya awali ambako lami itawekwa imekamilika kwa asilimia 98, madaraja madogo kiasi cha 55 tayari yamejengwa na vifaa vyote ikiwa ni pamoja na kokoto viko kwenye eneo la ujenzi.”

                   Barabara ya Dar es Salaam-Lindi ina urefu wa jumla ya kilomita 452 na kukamilika kwa kipande cha Nyamwage-Somanga una maana kuwa mtu yoyote anaweza kusafiri kwa lami tupu kutoka Mtwara hadi Kagera ama Mwanza ama Arusha ama Tunduma.

 

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu.

Dar es Salaam.

07 Desemba, 2012

 

No comments:

Post a Comment