Tuesday, April 24, 2012

MISS REDD’S ARUSHA CITY CENTRE KUJULIKANA MEI 5, 2012 NDANI YA HOTELI YA NAURA SPRINGS 

 
 Washiriki wa kitongoji Kanda ya kaskazini, Miss Arusha City Center 2012, wakiwa katika picha ya pamoja, tayari kuchuana vikali Mei 5, 2012 ndani ya hoteli ya Kitalii,Naura Springs Hotel iliyopo kati kati ya jiji la Arusha.katika shindano hilo kiingilio kimepangwa kuwa ni kwa viti maalum ni sh.25,000/= na kwa viti vya kawaida ni sh 15,000/=
Washiriki wa Miss Arusha City Center 2012 wakiwa darasani kwenye mafunzo ya nadharia yatolewayo na chuo cha Udereva na Ufundi,Modern Driving School,ambao pia ni moja ya wadhamini wa shindano hilo.
---
Mashindano ya Ulimbwende ngazi ya kitongoji  Kanda ya kaskazini,Miss Arusha City Center 2012,yanatarajiwa kufanyika Mei  5 2012 ndani ya hoteli ya Kitalii,Naura Springs Hotel iliyopo kati kati ya jiji la Arusha.

Akizungumza leo jijini Arusha,Mratibu wa shindano hilo Bi Upendo Simwita kutoka  kampuni ya Tour Visual Entertainment ambao ndio waandaji wa shindano hilo, amebainisha kuwa mpaka sasa maandalizi yao yanakwenda vizuri na kila kitu kimekwisha kamililka ikiwemo sambamba na kuwapata warembo ambao mpaka sasa wametimia 20.

Bi. Upendo Simwita amesema kuwa wameishakamilisha mchakato wa kuwapata Warembo wenye mvuto na wenye vigezo stahiki,anaongeza kuwa warembo hao wenye ari kubwa ya ushindani,kama waandaji watahakikisha muwakilishi wa Miss Tanzania 2012 anatokea kwenye kitongoji hicho.

“Shindano hilo litakalokuwa la tofauti kubwa na miaka ya nyuma litawakutanisha walimbwende wapatao 20, ambao watachuana vikali jukwaani, na hatimaye kumpata Mshindi wa Miss Arusha City Center”, alisema Upendo. Amesema kuwa kiingilia katika shindano hilo kimepangwa kuwa ni kwa viti Maalum sh 25,000/= na kwa viti vya kawaida sh.15,000/=

Kwa upande wa Burudani,Upendo  amesema kuwa kutakuwepo na Msanii mahiri wa Muziki wa kizazi kipya aitwaye Sam wa Ukweli, Muziki wa Asili, Live Band ya Watoto wa Simba pamoja na burudani nyingine  mbalimbali zitakazotolewa na walimbwende wenyewe siku hiyo.

ZAIDI YA ABIRIA 40 WANUSURIKA KIFO MKOANI MBEYA, BAADA YA BASI LAO KUGONGWA NA KUPINDUKA


Basi aina ya Coaster waliokuwa wakisafiria abiria zaidi ya 40, lenye nambari za usajili T 374 AVR, likiwa limepinduka baada ya kugongwa kwa nyuma na basi jingine la kampuni ya El Saedy lenye nambari T 499 AVG. Tukio lililotokea Aprili 23 mwaka huu saa moja asubuhi eneo la Imezu na Inyala Wilaya ya Mbeya Vijijini.


Basi la kampuni ya El Saedy lenye nambari T 499 AVG lililohusika katika ajali, baada ya kuligonga kwa nyuma basi aina ya Coaster enye nambari za usajili T 374 AVR ambapo zaidi ya abiria 40 kunusurika kifo. Tukio lililotokea Aprili 23 mwaka huu saa moja asubuhi eneo la Imezu na Inyala Wilaya ya Mbeya Vijijini. 
---

Picha na Habari: Ezekiel Kamanga, Mbeya.
Abiria zaidi ya 40 wamenusurika kifo baada ya basi waliokuwa wakisafiri aina ya Coaster, lenye nambari za usajili T 374 AVR, kupinduka lilipogongwa kwa nyuma na basi jingine la kampuni ya El Saedy lenye nambari T 499 AVG.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa basi la El Saedy likiwa katika hali ya mwendokasi liliharibika mfumo wa breki kutoka eneo la Mlima Nyoka na kuligonga basi hilo dogo kwa nyuma katika mteremko wa Shule ya Sekondari Imezu, hali iliyopelekea basi hilo dogo kupinduka.

Baada ya Coaster kupinduka basi la El Saedy likiwa bado katika mwendokasi liliendelea na safari, kabla ya dereva kufanikiwa kulichepusha kabla halijavuka reli ya TAZARA katika Kijiji cha Inyala Wilaya ya Mbeya Vijijini.

Aidha baadhi ya abiria katika basi hilo dogo walikuwemo wanafunzi 28, wa kike na kiume wakielekea shuleni majira ya saa moja asubuhi, Aprili 23 mwaka huu katika Shule ya Sekondari Imezu.

Mara baada ya ajali hiyo kutokea baadhi ya abiria walikuwemo katika basi hilo dogo walikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa Jijini Mbeya, ambapo kati yao wamelazwa ili kufanyiwa uchunguzi na wengine wakiruhusiwa kurudi nyumbani.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi wa Mkoa wa Mbeya Barakiel Masaki,hakupatikana kuelezea ajali hiyo ingawa dereva wa basi la El Saedy anashikiliwa na Polisi kwa mahojiano.

Picha na Habari: MbeyaYetu Blog.

YANGA YAOMBA RADHI MKUTANO MKUU


Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga ambaye pia mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF akiwakilisha klabu za Mkoa wa Dar es Salaam, Mohamed Bhinda aliwaomba radhi wajumbe wa Mkutano Mkuu kwa kitendo cha wachezaji wake kumpiga mwamuzi Israel Nkongo kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom dhidi ya Azam iliyochezwa Machi 10 mwaka huu.

Pia alimuomba Rais wa TFF, Leodegar Tenga kutoa msamaha wa adhabu ya kulipa faini iliyotolewa na Kamati ya Ligi ya TFF kwa wachezaji wawili wa Yanga ambao mpaka sasa hawajalipa faini hiyo.

Rais Tenga alimshukuru Bhinda kwa ujasiri alioonesha wa kuomba radhi mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kwa kitendo kile.

Aliongeza kuwa kwa vile yeye ni muumini wa kanuni, na adhabu hizo zimetolewa kwa mujibu wa kanuni hawezi kutoa msamaha, hivyo wachezaji hao walipe faini hizo.

Pia Rais Tenga alisema binafsi haziingilia kamati za TFF katika uamuzi ambao zinafanya kwa vile zina watu waadilifu, na angekuwa yeye binafsi ndiye anayetoa adhabu, angetoa adhabu kali zaidi kwa vile vitendo vya kupiga waamuzi havikubaliki katika mchezo wa mpira wa miguu.

FRANCIS CHEKA NA JAPHET KASEBA KUPAMBANA TENA SIKU YA SABASABA

FRANCIS CHEKA NA JAPHET KASEBA KUPAMBANA TENA SIKU YA SABASABA

Na Mwandishi Wetu

BINGWA wa kick Boxing Japhet  Kaseba amesaini mkataba wa kucheza na Bingwa wa dunia wa ndondi mkanda unaomilikiwa na IBC, Francis Cheka wa Morogoro  katika uzani wa KG 75 utakaofanyika siku ya sabasaba jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa kusaini mkataba huo Kaseba amesema anashukulu kupata mpambano huo na atahakikisha anaonesha uwezo wake wote katika mchezo huo kwani yeye ni bingwa wa mapambano

;Najua mabondia wa hapa bongo wananikwepa sana kwa kuwa nimeshakuwa bingwa wa ngumi za mateke lakini awajui mimi ni bingwa katika mapigano yote alisema Kaseba;

Nitahakikisha naweka kambi ya kutosha na kukata ngebe za cheka ni mtoto mdogo sana katika masumbwi kwa kweli bingwa wa kweli ni Rashidi Matumla ambaye ninamuheshimu mpaka sasa cheka kanikimbia mda mrefu tu tangia tupambane 3 October 2009  ambapo alipewa ubingwa kwa kusingizia mshabiki wangu alikuja kumtupa nje ya uwanja kazi yake yeye anarudiana na Mada Maugo kila siku lakini kwa sasa kakanyaga miwaya zamu yake imefika,

Nae Promota wa mpambano huo Kaike Siraju amesema mpambano huo utakaofanyika Dar es salaam siku ya sabasaba utakuwa ni mpambano ambao aujawai kutokea kwa kuwa mabondia hao wanakubalika na mashabiki wa ndani na nje ya Nchi

Mbali na mpambano huo pia kutakua na mapambano ya utangulizi na burudani mbalimbali ambazo mtatangaziwa baadae.

BAGAMOYO KUWAKA MOTO USIKU WA MKESHA WA MUUNGANOKWANJA MAALUM KWA AJILI YA MKESHA WA SIKUKUU YA MUUNGANO LINATARAJIA KUUSHIKA MJI WA BAGAMOYO KESHO TAREHE 26.04.2012 NDANI YA CLUB LUSONA ILIYOPO KWENYE HOTELI YA MILLENIUM SEA BREEZE RESORT(OLD POST OFFICE).

KWA MUJIBU WA TAARIFA ZILIZOPATIKANA MJINI BAGAMOYO MCHANA WA LEO KUTOKA KWA MMOJA WA WARATIBU WA BURUDANI HIYO MAALUMU BW.ALBERT KAWOGO, BURUDANI HIYO YA AINA YAKE INATARAJIA KUANZA SAA 3:00 USIKU NA KIINGILIO KITAKUWA 5000/= TU.


TUMEJIZATITI KUTOA BURUDANI YA AINA YAKE KATIKA CLUB HII KWA KUONGEZA NGUFU YA MADJ MAARUFU KUTOKA MOJA YA KITUO CHA REDIO CHA JIJINI DAR ES SALAAM ILI WATEJA WETU WAWEZE KUPATA BURUDANI YA AINA YAKE NA NINAWAOMBA MASHABIKI WA BURUDANI YA DISKO KUJITOKEZA KWA WINGI,ALISEMA KAWOGO.


HII ITAKUWA MARA YA KWANZA KWA BURUDANI KAMA HII KUFANYIKA KATIKATI YA JUMA NDANI YA CLUB LUSONA YENYE UBORA WA AINA YAKE,AMBAYO KWA PAMOJA IMEANDALIWA NA ALBERT KAWOGO(MUKUBWA KAWOGO) WA FREE VOICE INVESTMENT NA KIMKEV ENTERTAINMENT
.

MAFUGULI ASHIRIKI KUUAGA MWILI WA MUASISI WA CHAMA CHA MAPINDIZI WA WILAYA YA CHATO

                                   Waziri Magufuli akitoa salamu za mwisho

 
Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Chato leo ameshiriki kuuaga mwili wa Marehemu Constantine Jaha Misungwi ambaye ni muasisi wa Chama cha Mapinduzi wilayani Chato.
 
Marehemu Misungwi alizaliwa tarehe 01 Julai mwaka 1925 ambapo katika muda mwingi wa uhai wake alikuwa akijihusisha sana na shughuli za kisiasa. Marehemu Misungwi ndiye mwanzilishi wa mji wa Chato na katika nyakati tofauti aliwahi kushika nafasi mbali mbali ikiwamo ya Uenyekiti wa Chama cha Mapinduzi katika mji wa Chato, Udiwani na pia Uenyekiti wa Chamba Cha Mapinduzi katika Jimbo la Biharamulo Mashariki.
Marehemu mzee Misungwu ndiye aliyemshawishi Mheshimiwa Magufuli kujiunga na siasa mnamo mwaka 1990 na baadaye kumchukulia tena fomu za kugombea Ubunge wa Jimbo la Biharamulo Mashariki mwaka 1995 na kushinda kwa mara ya kwanza.
Mmoja ya watoto wa marehemu, Bwana Kaloli ameelezea kuwa baba yake alilazimika kuletwa Dar es Salaam kutokea Chato kwa ajili ya matibabu ya kansa na alilazwa kwa wiki mbili katika Hospitali ya Tumaini kabla ya kuruhusiwa kutoka mnamo tarehe 20 Aprili 2012 lakini hata hivyo mauti yakamfika siku mbili baadaye akiwa nyumbani kwa mwanaye huyo.Mwili wa Marehemu Mzee Misungwi umesafirishwa leo kuelekea Chato kwa mazishi

KANUSHO LA HABARI POTOFU KATIKA TANZANIA DAIMATAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Gazeti la Tanzania Daima la leo Jumapili Aprili 22, 2012 lina  habari katika ukurasa wake wa mbele yenye kichwa cha habari ‘JK alinda Mawaziri’,   inayodai  kumekuwa na mazungumzo baina ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Waziri Mkuu Mhe Mizengo Pinda kuhusu hatua inayopaswa kuchukuliwa dhidi ya mawaziri waliotakiwa kujiuzulu.

Habari hiyo imedai kuwa  Mhe. Pinda anataka mawaziri wanaokabiliwa na tuhuma waondoke ili kuleta uwajibikaji serikalini, lakini, imeendelea  kudai habari hiyo, “Rais Kikwete amesema mawaziri hao waachwe waendelee na kazi zao, kwa kuwa suala hili ni la upepo tu, liachwe litapita”.

Tunachukua nafasi hii kuweka bayana kwamba habari katika hilo hazeti la Tanzania Daima Jumapili si za kweli, bali ni za uzushi na upotoshaji mkubwa.
Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye alikuwa katika ziara ya kikazi nchini Brazil, amerejea jana Aprili 21, 2012 jioni. Hajaonana wala kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu, Mhe. Pinda.

Hivi sasa Mhe. Rais anasubiri kupata taarifa rasmi  kutoka Bungeni Dodoma.

Mhe Rais anawasihi wananchi wasiamini habari hizo za upotoshaji zilizomo kwenye gazeti hilo la Tanzania Daima Jumapili.

Pia ametoa rai kwa wanahabari wasitoke nje ya mstari wa weledi katika kutekeleza kazi zao ili kuendelea kulinda heshima zao binafsi, vyombo wanavyofanyia kazi pamoja na taaluma yenyewe.

Mwisho

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
22 Aprili, 2012

Friday, April 20, 2012

NIMEZAA NA MAREHEMU STEVE KANUMBA-SALMA HAMIDU

 Habari: Mashaka Baltazr wa Global Publisher, Mwanza

SALMA Hamidu, mkazi wa Igogo, jijini Mwanza ameibuka na kudai amezaa na marehemu Steven Kanumba mtoto wa kike aitwaye Treasure Steven Charles Kanumba (2), Ijumaa linashuka na maneno ya kinywa chake.

Akizungumza na mwandishi wetu, Salma anayefanya kazi kwenye Ofisi ya Uwakili ya Law Consultancy jijini Mwanza, alidai alianza kufahamiana na marehemu mwaka 2006 wakati yeye akiwa kwenye Kundi la Nyakato Arts chini ya Mwalimu Joseph.

CHANZO CHA UHUSIANO
Salma akasema kuwa, uhusiano wao uliunganishwa na Mwalimu Joseph ambaye alimpa marehemu namba zake za simu wakati alipopeleka filamu za Machozi Yangu na Siri Yangu kuifanyia uhariri (editing) jijini Dar es Salaam katika studio alizokuwa akifanyia kazi marehemu.

“Marehemu alipoona picha zangu kwenye filamu hizo alivutiwa na mimi katika kuigiza, akaomba namba zangu za simu kwa Mwalimu Joseph,” alisema Salma.

Mrembo huyo aliendelea kuweka wazi kuwa, baadaye Mwalimu Joseph alirejea Mwanza na kumtaka radhi kwa kumwambia alimpa Kanumba namba zake za simu.

SIMU YA KWANZA YA KANUMBA KWA SALMA
“Baada ya wiki mbili nilipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha ni Kanumba. Aliuliza kama huwa nasafirisafiri.

“Nilimjibu si sana kwa sababu nasoma. Wakati huo nilikuwa nasomea kompyuta kwenye Chuo cha English Kingdom Nyakato,” alisema Salma.
Akaongeza: Marehemu alinielewa, lakini akaniomba niwe mwenyeji wake punde atakapokuja Mwanza, nikaridhia ombi lake, alikata simu, lakini tukaendelea kuwasiliana kwa simu kila mara.

Salma alisema mawasiliano yake na Kanumba yalidumu kwa mwaka mmoja bila kuonana ‘laivu’.

Aidha, alidai kuwa siku moja marehemu alimpigia simu akimtaka kujiunga na kundi lake lililopo Dar, akamkubalia lakini tatizo likawa umbali. “Lakini marehemu akaniambia nisiwe na wasiwasi kuhusu hilo,” alisema Salma.

Akizidi kumwaga data za uhusiano wao ulivyoanza, Salma alisema:
 (Salma Hamidu aliyezaa na marehemu Steve Kanumba.)

LAIVU KWA MARA YA KWANZA
“Mwaka 2007, Kanumba aliniita Dar, alinitumia tiketi ya ndege ya Precision Air, kwetu niliaga nakwenda kumsalimia mama mkubwa anayeishi Tabata.

“Nilipofika Dar, nilimpigia simu Kanumba kumtaarifu nimefika, akanitaka tukutane Ubungo Plaza Hotel (Blue Pearl),” alisema Salma.

Pale Ubungo Plaza, marehemu kwa mara ya kwanza alimtamkia lililo moyoni mwake kwamba ametokea kumpenda na akamuomba wawe wapenzi.
“Sikuwa na uamuzi wa haraka, lakini kutokana na ushawishi wake nilikubali, baadaye nilirudi Tabata kwa mama mkubwa.

“Usiku alinipigia simu, akaniomba kesho yake tusafiri kwenda Zanzibar, nilikubali, asubuhi niliaga kwa shangaza tukaenda Zanzibar.

“Tulifikia Bwawani Hoteli. Tulikaa kwa siku tatu na kwa mara ya kwanza nilikutana na marehemu kimwili. Tuliporudi Dar mimi nikarejea Mwanza,” alisema Salma.

KANUMBA PENZI LAKOLEA, ATUA MWANZA
“Baada ya kama miezi minne na siku kadhaa hivi, marehemu alinipigia simu akasema yuko Mwanza, anataka kuja chuoni kuniona. Alikuja akiwa ameongozana na marafiki zake wawili, Credo na Theonist Rutashoborwa.

“Walikuja hadi chuoni, mimi nilitoka tukaenda kukaa kwenye baa ya Shentemba. Ilipofika saa 2 usiku, tukahamia Isamo Hotel,” alisema Salma.

Salma aliendelea kusema kuwa, pale Isamo walipata chakula kabla ya kujitupa kitandani lakini siku hiyo muda mwingi alikuwa akijisikia vibaya, marehemu akamtaka asubuhi akapime.

“Asubuhi nilikwenda kwenye Kliniki ya Dokta Ng’walida, daktari bingwa wa magonjwa ya akina mama na watoto. Vipimo vilionesha nilikuwa na ujauzito wa miezi minne.

“Nilimwonesha marehemu majibu yale, hakuonekana kukubali wala kukataa, lakini baadaye akasema kazi yake haimruhusu kuwa na mtoto wala familia hadi atakaponiambia. 

“Baada ya siku mbili, aliaga kurejea Dar pamoja na marafiki zake. Siku chache baadaye huku nyuma kwa bahati mbaya ujauzito ulitoka, nilikwenda kwa daktari mmoja Nyakato National ambaye alithibitisha hilo. Huo ulikuwa mwaka 2008.

UJAUZITO WA PILI
Salma alisema kuwa mawasiliano na marehemu yaliendelea. Kuna siku alimpigia simu akimtaka wakutane jijini Arusha.

Alipofika alipokelewa na Kanumba mwenyewe kabla ya kwenda kupiga kambi kwa rafiki yake mmoja aliyekuwa akiishi peke yake.

Akasema kukutana kwao kimwili kwa safari hii, ndiko kulimpa ujauzito na hatimaye kujifungua binti anayeitwa Treasure au Tunu.
Arusha waliondoka na ndege hadi Mwanza ambapo walifikia Ladson Hotel, ipo Bwiru na kukaa kwa siku mbili kabla ya kumruhusu kurejea nyumbani kwao Igoma.

Akiwa na ujauzito huo, Kanumba alimtumia nauli akimtaka wakutane mjini Morogoro.

“Nikiwa na tumbo langu, aliniita Morogoro, nilisafiri kwa basi hadi kule, nilifikia kwa shangazi yangu yeye alipanga kwenye hoteli ipo jirani na Kituo cha Mabasi cha Msamvu.

KANUMBA ATOA ONYO
“Kulitokea kutokuelewana kidogo na marehemu kwa sababu ya ujauzito ule, akirejea mazungumzo yake ya awali kuwa, kazi yake haimruhusu kuwa na mtoto wala familia, lakini nilimwambia sina namna ya kufanya kuhusu ujauzito ule.

“Hata hivyo, marehemu alinionya nisimwambie mtu kuhusu ujauzito kuwa ni wa kwake, iwe siri yangu na yake kwa sababu hakutaka habari hiyo ifike kwenye magazeti,”alisema Salma.

Akaongeza: Baada ya hapo, alinipa shilingi 150,000 nikarudi nyumbani Mwanza.

“Nikiwa Mwanza alikuwa akinipigia simu akitaka kujua naendeleaje na tumbo langu na kunitaka nijiandae kwa safari ya Dar, atanitumia tiketi ya ndege.

“Nilisafiri, nilipofika Dar nilimjulisha, akasema tusikae Dar, twende Zanzibar. Kule tulifikia tena Bwawani Hotel. Tulikaa kwa siku nne, kisha tukarejea Dar.
Lakini tukiwa Zanzibar kuna mtu alinipigia simu na yeye akiwepo, alikasirika sana na kuninyang’anya simu, akachukua namba kisha akampigia mtu huyo, waligombana kwenye simu. Aliipasua simu yangu, akaenda kuninunulia nyingine.

“Alikuwa mtu mwenye hasira, hakutaka kusikia unazungumza na simu hasa ikiwa ni sauti ya kiume. Ugomvi huo ulisababisha aikane mimba, akasema namsingizia ni ya mwanaume aliyenipigia simu. Ilifika mahali akasema kila mtu aishi kivyake.

“Hata hivyo, alikuja kuniomba msamaha huku akizidi kunionya kuwa ole wangu nitangaze nina mimba yake.”

Alisema ugomvi wake na Kanumba ulitokana na ujauzito na ilifika mahali Salma alimweleza mama yake ambaye alimlaumu kwa kujiingiza kwenye uhusiano na mwanaume huyo.

MISAADA KUTOKA KWA KANUMBA
Kwa upande wa misaada, Salma alisema akiwa mjamzito, marehemu alimtumia shilingi Milioni mbili na laki mbili kwa ajili ya kununua kiwanja.

Baadaye alimtumia shilingi Milioni moja za kupanga nyumba. Fedha hizo alizituma kupitia Benki ya Standard Chartered Tawi la Mwanza.
Baada ya kutuma fedha hizo, marehemu aliwahi kwenda Mwanza na kufikia kwenye Hoteli ya Ryans Bay. Wakati huo mimba ilikuwa na umri wa miezi saba.

HAKUTAKA KUPIGA NAYE PICHA
Salma anasema: Nilimtaka tupige picha ya ukumbusho akakataa, lakini nilipojifungua alikuja na kumpiga picha mtoto kwa kutumia simu yake akisema, ‘mtoto mama yangu mtupu kwani amefanana naye sana.’

Aliongeza kuwa alipojifungua Kanumba alimtumia shilingi 500,000 za matumizi ya mtoto kupitia simu ya mama yake mzazi na Salma (hakumtaja jina).

Aliendelea kusema kulijitokeza sakata wakati wa kumpa jina mtoto, Kanumba akitaka amwite jina la mama yake, huku Salma naye akitaka kumwita la mama yake, ndipo wakakubaliana mtoto aitwe Treasure au Tunu ili kumaliza mzozo wa kugombea kumwita mtoto jina la upande mmoja.

“Treasure alipofikisha miezi saba alisema nimpige picha nimtumie ili amwone alivyofikia, nilifanya hivyo. Siku moja akaniambia angetunga filamu kuhusu maisha yetu ambayo alipendekeza iitwe My Gift.

“Siku chache kabla ya kifo chake alinipigia simu pamoja na mtoto akisema alitaka kusafiri na asingekuwepo kwa mwezi wote wa Machi mwaka huu, alimsamilia mwanaye. Lakini cha kushangaza siku chache nikapewa taarifa za kifo chake,” alisema Salma.

KWA NINI USIRI?
Salma alisema mpaka sasa anashindwa kuelewa ni kwa nini marehemu alitaka uhusiano wao uwe wa siri. Lakini baadhi ya marafiki zake walikuwa wakifahamu uhusiano huo.

NENO LA MWISHO LA SALMA
“Kanumba kaniacha njia panda, sijui la kufanya, lakini ni vyema kama angemtambulisha mwanaye kwa ndugu zake kuliko hivi sasa ambapo mengi yatazuka kuwa pengine natafuta fedha za marehemu.

“Sijaweka wazi ili nipate chochote, bali nahisi dhambi kuficha kwa sababu huyu mtoto si damu yangu peke yangu.

“Nitakuwa mbaya kwa Mungu kama nisiposema ukweli. Angekuwepo mwenyewe nisingesema kwa sababu yeye ndiye alikuwa kiongozi wa maisha ya mtoto.

“Narudia tena, nina uwezo wa kumlea na wala sihitaji mtoto achukuliwe na kwenda kuishi kwa baba, ila familia ijue kuna damu yao kwangu.

“Kama hawataamini, niko tayari kufika Dar na kupima DNA ili familia ya marehemu ijiridhishe,” alisema Salma.

Hata hivyo, Salma alikiri kufanya kosa la kutowahusisha marafiki wa Kanumba kumtegulia kitendawili hicho na kudai pengine umri mdogo ulichangia. Salma alizaliwa mwaka 1987.

Alisema mtu pekee ambaye watu wanamfahamu na ndiye shahidi wa uhusiano wake na marehemu ni msanii wa maigizo, Ramadhan Malele ‘Swebe’ ambaye alikuwa akiwasiliana naye mara kwa mara.

Salma alisema kabla Kanumba hajafikwa na mauti, yeye aliwahi kukutana na Swebe jijini Mwanza ambapo alimsimulia hali ilivyo na akamshauri kusikiliza matakwa ya marehemu ya kutotoa siri ya kuwepo kwa mtoto huyo.

SIMAMIA ZOEZI LA KUMUONDOA WAZIRI MKUU MADARAKANI


Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Mh Zitto Kabwe amelitaarifu Bunge kuwa mchakato unaandaliwa kukusanya saini za wabunge 70 ili kuweza kupeleka hoja ya kulitaka Bunge kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu.

Zitto amesema zoezi zima la saini hizo linaanza kesho asubuhi Mlangoni ili kabla ya Jumatatu liwe limekamilika ili kuweza kuwasilisha hoja hiyo ili Wabunge na Bunge limshinikize Waziri mkuu kujiuzulu au vinginevyo mawaziri wote waliotajwa kuhusika na ubadhirifu wa fedha za umma katika ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wawe wamejiuzulu badala yake.

Hii imetokea jioni hii Bungeni Dodoma ambapo wabunge wengi bila kujali itikadi za vyama vyao wameonekana kukerwa na utendaji mbovu wa mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete.

TAMKO LA KITUO CHA SHERIA NA HAKI ZA BINADAMU KUHUSU WAJUMBE WA TUME YA KUKUSANYA MAONI YA KATIBA MPYA


Mkurugenzi  Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Bianadamu (LHRC) Bi. Hellen Kijo Bisimba akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa tamko kuhusiana na tume iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete.

Ndugu wanahabari na wananchi kwa ujumla,
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu tumefuatilia kwa makini sana mchakato wa Katiba mpya kuanzia ulipoanza mpaka hapa ulipofikia. Sote tunafahamu kwamba hatua iliyofikiwa kwa sasa ni kuteuliwa na kuapishwa kwa wajumbe wa tume ya kukusanya maoni juu ya mchakato mzima wa Katiba mpya na namna ambavyo wananchi wangependa iwe.
Tunependa kupompongeza sana Mheshimiwa Rais na Serikali kupitia wizara ya Katiba na Sheria kwa hatua iliyofikiwa mpaka sasa kwenye mchakato mzima. Tunatoa pongezi kwa uteuzi wajumbe wengi waliobobea katika fani mbalimbali za  Sheria, Siasa na Masuala ya kijamii. Tumefurahi kuona kuwa Mheshimiwa Rais amemteua  kuwa mwenyekiti wa Tume  Jaji Joseph Sinde Warioba ambae tulishaona kazi yake nzuri hususan pale alipoongoza vizuri tume ya Rais iliyohusu masuala ya Rushwa. Tuna imani kuwa ataongoza tume hii kufanya kazi nzuri. Wajumbe  wa Tume hii ni  32 (akiwemo mwenyekiti na makamu)  waliapishwa tarehe 13/04/2012.
Wajumbe hao ni kama ifuatavyo;
Mwenyekiti wa Tume ambaye ni Jaji Sinde Warioba na Makamu Mwenyekiti Jaji Mkuu  Mstaafu Agustino Ramadhani.Wajumbe wa tume toka Tanzania Bara ni Prof. Mwesiga L. Baregu, Nd. Riziki Shahari Mngwali, Dr. Edmund Adrian Sengodo Mvungi, Nd. Richard Shadrack Lyimo, Nd. John J. Nkolo, Alhaj Said El- Maamry, Nd. Jesca Sydney Mkuchu, Prof. Palamagamba J. Kabudi, Nd. Humphrey Polepole, Nd. Yahya Msulwa, Nd. Esther P. Mkwizu, Nd. Maria Malingumu Kashonda, Mhe. Al-Shaymaa J. Kwegyir (Mb), Nd. Mwantumu Jasmine Malale Na Nd. Joseph Butiku. 2 Wajumbe wengine  15 ni kutoka Tanzania Zanzibar. Wajumbe hao ni Dkt. Salim Ahmed Salim, Nd. Fatma Said Ali, Nd. Omar Sheha Mussa, Mhe. Raya Suleiman Hamad, Nd. Awadh Ali Said, Nd. Ussi Khamis Haji, Nd. Salma Maoulidi, Nd. Nassor Khamis Mohammed, Nd. Simai Mohamed Said, Nd. Muhammed Yussuf Mshamba, Nd. Kibibi Mwinyi Hassan, Nd. Suleiman Omar Ali, Nd. Salama Kombo Ahmed, Nd. Abubakar Mohammed Ali na Nd. Ally Abdullah Ally Saleh.
Mapungufu tunayoyaona;
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu tunaona mapungufu makubwa mawili kwa tume hii
i) Kuwemo kwa mbunge na mjumbe wa baraza la wawakilishi
ii) Uwakilishi finyu wa kijinsia na makundi mengine mfano vijana
Wawakilishi kuwa wajumbe
Kituo hakikubaliani kabisa na uteuzi wa wakilishi wa wananchi (Mbunge na Mjumbe wa Baraza la wawakilishi). Wajumbe hawa ni Mhe. Al-Shaymaa J. Kwegyir (Mb) Tanzania Bara na Raya Suleiman Hamada mwakilishi Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
Sababu kubwa za kutokukubaliana na uteuzi wa wajumbe hawa ni kuwa kwanza,
hawa watashiriki kama wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba (constituent assembly) kwa hiyo kuna ‘mgongano ulio dhahiri wa kimaslahi’. (kwa mujibu wa vifungu cha 6 na 22 (1) (a) na (b) vya sheria Namba 8 ya Mabadiliko ya Katiba, 2011)
Pili wananchi wanaowawakilisha watanyimwa haki yao ya kuwakilishwa kwa kipindi chote cha miezi 18 mpaka ishirini ambacho tume itafanya kazi kwa mujibu wa sheria.
Tatu, kuna majina mengi ambayo mheshimiwa Rais alipelekewa yenye sifa za kutosha angeweza kuwateua. Kulimbikiza kazi nyingi kwa watu wale wale si afya kwa demokrasia.
Uwakilishi finyu wa kijinsia na makundi mengine
Katika tume hii tumeona kuna uwakilishi finyu sana wa makundi kwa mfano wanawake wako 10 kati ya 32, yaani sawa na asilimia 27% tu! Tungetegemea asilimia 50% kwa 50% kwani Tanzania imesaini na kuridhia mkataba wa nyongeza wa maendeleo ya kijinsia kusini mwa Afrika yaani SADC Gender Protocol. Pia 3 Tanzania ina asilimia ya 51 ya idadi ya wanawake ambao miongoni mwao wengi wana utaalamu na sifa za kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume.
WITO
I) Tunapenda kutoa wito kwa serikali kuwa mchakato wa Katiba ni wa muhimu sana hautakiwi kuchukuliwa  kwa  wepesi. Mchakato huu unajenga mustakabali wa Taifa letu kwa miaka mingi ijayo. Hivyo katika maamuzi yote yanayochukuliwa, kuwe na jicho la HAKI ZA BINADAMU na utawala wa sheria.
II) Pia tunapenda kutoa wito kwa WANANCHI wote wa Tanzania, mijini na vijijini, wakulima, wafanyakazi na wafanyabiashara, TUSHIRIKI kwenye mchakato huu. Tunawasihi kuwa Tume ya Katiba itakapokuja kwenye
maeneo yetu tuhudhurie mikutano yote na kutoa maoni yetu juu ya Katiba Mpya. Wananchi katika makundi au mtu mmojamoja anaweza kupeleka maoni ya maandishi kwenye tume mara anuani itakapojulishwa kwa wananchi.
III) Mwisho tunatoa wito kwa tume kuhakikisha watu wote wanatoa maoni yao bila ubaguzi. Makundi yote ya jamii yafikiwe (Wanawake, wanaume, watu wenye ulemavu na watoto wenye umri wa kutoa maoni).
Asanteni kwa kunisikiliza,
Dr. Helen Kijo-Bisimba
Mkurugenzi mtendaji- LHRC

Wednesday, April 18, 2012

Maximo ashauri jinsi ya kupata wachezaji bora wa timu ya taifa

                                                                                                                                                                                                                                                                                           Kocha Kocha wa zamani wa Taifa Stars Marcio Maximo akisalimiana na  Rais Jakaya Mrisho Kikwete   alipokwenda kumsalimia Rais katika hoteli ya Tivoli jijini Sao Paulo
Kocha wa zamani wa Taifa Stars Marcio Maximo akimsalimu mke wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Mama Salma Kikwete alipokwenda kuwasalimia  katika hoteli ya Tivoli jijini Sao Paulo

Na Anna Nkinda – Sao Paul, Brazil
18/04/2012 Vilabu vya soka nchini vimeshauriwa kuwa na timu nzuri kuanzia ngazi ya watoto wenye umri wa miaka nane, vijana  na kuendelea ili kupata timu bora ya Taifa.
 Wito huo umetolewa na aliyekuwa kocha mkuu wa timu ya Taifa Star  Marcio Maximo wakati akiongea na waandishi wa habari mjini Sao Paul.
Maximo alisema kuwa timu nyingi ambazo ni bora na zinafanya vizuri katika mchezo wa soka zimekuwa zikiwaandaa watoto wenye vipaji vya mchezo huo wangali wadogo ili waweze kuwa wachezaji wazuri hapo baadaye.
Kocha Maximo pia alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Jakaya Mrisho kikwete, ambapo alimnshukuru sana Rais kwa ushirikiano wa hali ya juu aliompa wakati alipokuwa akiifundisha Taifa Stars miaka takriban mitatu iliyopita.
Kwa upande wake Rais Kikwete alimpongeza Kocha Maximo kwa juhudi zake za kuendeleza soka la Tanzania, akimwambia uwepo kwake Tanzania kuliasidia sana kuiweka nchi katika ramani ya mchezo huo.
Rais Kikwete alikubaliana na kocha huyo kwamba ili timu ya Taifa ifanye vyema ni lazima maandalizi yaanzie ngazi za chini, ikiwemo vilabu kuwa na timu za watoto na vijana ambao baadaye watakuwa hazina ya Taifa Stars.
 Kuhusiana na uvumi ulioenea kuwa anataka  kwenda kufundisha timu za Taifa Stars, Azam na Yanga alisema kuwa siyo kweli na wala hajawasiliana na timu hizo na hawezi kwenda kufundisha  kwani hivi sasa anamkataba wa kufundisha timu ya Democrata iliyopo nchini humo.
Rais alimshukuru Kocha Maximo kwa kuja kumsalimia na kumpa zawadi ya jezi ya timu ya Democrata anayofundisha, na kumtakia heri na fanaka katika kazi yake hiyo.
 “Timu ya Taifa Star ina kocha mzuri ambaye ninamuheshimu na ninaukubali ufundishaji wake hivyo basi kupitia kocha huyo ninaamini watanzania watazidi kuendelea katika soka na kufika mbali zaidi”, alisema.
 Maximo alimalizia kwa kusema kuwa  anamawasiliano mazuri na watanzania na anawapenda ndiyo maana kila mahali anapopita anajivuna na kusema  kuwa Tanzania ni nchi yake ya pili.
 Hivi sasa Maximo ni kocha wa timu ya  Democrata iliyopo nchini humo ambapo wiki ijayo inatarajia kuanza mashindano ya taifa yatakayopelekea kupata wachezaji bora watakaoshiriki mashindano ya kombe la Dunia yanayotarajia kufanyika mwaka 2014 nchini Brazil.