Tuesday, March 20, 2012

Basi la Prince Muro lapata ajali Usiku wa kuamkia Leo Tunduma

Basi la Kampuni ya Prince Muro lenye namba za usajili T 485 BQV lililokuwa likifanya safari yake ya kutoka Dar es Salaam kuelekea Tunduma mkoani Mbeya limepoata ajali na kupinduka usiku wa kuamkia leo.

Ajali hiyo iliyotokea wakati dereva wa basi hilo akijaribu kulipita Lori katika maeneo ya Senjele wakati likielekea Tunduma na kusababisha kifo cha mtu mmoja na kujeruhi wengine 14.

Hivi ndivyo zinavyo onekana Damu na viti kuharibika vibaya baada ya ajali hiyo iliyo tokea jana usiku

Baadhi ya mabaki ya vitu baada ya ajali hiyo jana usiku

Hili Ndilo Gari la mizigo ambalo basi la Price muro lilitaka kulipita, na  baadae kushindwa na kupinduka baada ya kukutana na Gari lengine mbele yake


Shimo hili limechimbika wakati wa ajali hiyo ilipo tokea jana usiku.
Picha zaidi  MBEYA YETU BLOG

Lowasa , Mwinyi waongoza sherehe za kuzaliwa jimbo jipya la Kanisa Katoliki Ifakara


Mh. Lowassa akiwapungia mkono wakazi wa Ifakara wakati alipohudhuria sherehe za uzinduzi wa Jimbo jipya la Kanisa Katoliki Ifakara.
Waziri Mkuu Mstaafu,Mh. Edward Lowassa akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro,Mh. Joel Bendera wakati alipokuwa akiwasili kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kilombero,kabla ya safari ya kuelekea kwenye Sherehe ya Kuzinduliwa kwa Jimbo Jipya la Kanisa Katoliki Ifakara na kusimikwa kwa Askofu Mpya wa Jimbo hilo.
Waziri Mkuu Mstaafu,Mh. Edward Lowassa akiongozana na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro,Mh. Joel Bendera wakati wakielekea kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kilombero leo.Watatu Kulia ni Mke wa Waziri Mkuu Mstaafu,Mama Regina Lowassa.
Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili,Mh. Ally Hassan Mwinyi (kushoto) na Mkewe Mama Sitti Mwinyi (katikati) wakiwa kwenye mazungumzo na Waziri Mkuu Mstaafu,Mh. Edward Lowassa (wa pili kulia) pamoja na Mkewe Mama Regina Lowassa (kulia) kabla ya kuanza safari ya kuelekea kwenye Sherehe ya Kuzinduliwa kwa Jimbo Jipya la Kanisa Katoliki Ifakara na kusimikwa kwa Askofu Mpya wa Jimbo hilo,Muhashamu Salitaris Melchior Libena iliyofanyika leo Ifakara,Wilayani Kilombero Mkoani Morogoro.
Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowasa akisalimiana na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Hadji Mponda kutoka kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Joel Bendera na Mzee Alli Hassan Mwinyi.
Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili,Mh. Ally Hassan Mwinyi akihutubia kwenye Sherehe hizo.
Mh. Lowassa akibadirishana mawazo na Askofu Mkuu wa Jimbo la Songea.
Waziri Mkuu Mstaafu,Mh. Edward Lowassa akisalimiana na Muadhama Polycarp Kardinali Pengo mara baada ya kumalizika kwa Sherehe ya Kuzindua Jimbo Jipya la Kanisa Katoliki Ifakara na kusimikwa kwa Askofu Mpya wa Jimbo hilo iliyofanyika leo Ifakara,Mkoani Morogoro.
Mh. Lowassa akizungumza na Mmoja wa wananchi wa Mji wa Ifakara.
Waziri Mkuu Mstaafu,Mh. Edward Lowassa akitoa salamu kwa wakristo waliofika kwenye Sherehe hizo leo,ambapo ameliomba Kanisa Katoliki kuisaidia serikali katika kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana.
Askofu Mkuu Mpya wa Jimbo la Ifakara,Muhashamu Salitaris Melchior Libena akiongoza ibada yake ya kwanza akiwa ni Askofu wa Jimbo Jipya la Ifakara mara baada ya kusimikwa leo.
Askofu Mkuu Mpya wa Jimbo la Ifakara,Muhashamu Salitaris Melchior Libena akitoa baraka zake kwa Viongozi wa Serikali waliohudhulia Sherehe hizo za kusimikwa kwake leo.
Waumini wa Kanisa Katoliki Ifakara wakiwa katika ibada hiyo.
Kwaya ya Watoto ikiimba katika ibada hiyo.

Friday, March 16, 2012

Maonesho ya Wiki ya Maji yaanza Iringa


Katika banda la Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) kuna mambo mazuri kama haya.kama yanavyoneshwa na Wafanyakazi wa Kampuni hiyo kutoka kushoto ni Afisa Mauzo wa SBL mkoani Iringa, Elias Amani, Mkurugenzi wa Mahusiano na Mawasilino wa SBL, Teddy Mapunda, Meneja Maneja Mawasiliano wa SBL, Iman Lwinga na Meneja wa Mahusiano ya Jamii wa SBL, Nandi Mwiyombela wakiwa katika banda hilo ndani ya viwanja vya Samora mjini Iringa kunakofanyika maonesho ya wiki ya Maji 2012 kitaifa. SBL imedhamini maadhimisho hayo mwaka huu. 
 Washiriki wakiendelea na kuandaa mabanda yao.
Washiriki Mbali mbali wa maonesho ya maadhimisho ya Wiki ya Maji duniani wakiwa tayari wameweka sawa mabanda yao katika Uwanja wa Samora mjini Iringa.

Sioi azidi kuwashika Arumeri Mashariki



 Sioi akiomba kura kwa wananchi wa Makiba. Kushoto ni Mbunge wa Simanjiro Christopher Ole Sendeka  na kulia  Mratibu wa kampeni za CM jimbo la Arumeru Mashariki Mwigulu Nchemba.
Wananchi wakimbeba kumpeleka jukwaani kuhutubia mkutano wa kampeni za CCM uliofanyika Kijiji cha Makiba kata ya Makiba, Arumeru Mashariki jana
 Katibu wa NEC, Oganaizesheni CCM, Asha Abdalla Jma akihutubia mkutano wa kampeni uwanja wa mpira wa kijiji cha Makiba.
 Mbunge wa Mtera, Mjumbea wa NEC ya CCM,  Livingstone Lusinde aka Kibajaji akihutubia Makiba.
Meja Jenerali Mstafu Mirisho Sarakikya akizungumza kwa niaba ya wazee katika mkutano wa kampeni uliofanyika kata ya  Makiba
Hafsa Kazinja wa TOT akikamua Uwanja wa mpira wa Makiba
Shabiki wa CCM wa Kata ya Makiba akishangilia mkutanoni
Maelfu ya watu mkutano wa kampeni za CCM Makiba
Nchemba akihutubia Makiba

Mazishi ya Mwakilishi jimbo la Bububu Zanzibar yafanyika leo



Mamia ya wananchi wa Zanzibar kesho asubuhi wanatarajiwa kushiriki katika mazishi ya aliekuwa Mwakilishi wa Jimbo la BUBUBU Marehemu Salum Amour Mtondoo aliefariki Dunia leo katika Hospitali mkuu ya Mnazi Mmoja Mjini Zanzibar baada ya kusumbuliwa na maradhi ya kichwa. 
 
 Kwa mujibu ya ratiba ya shughuli za Mazishi iliotolewa na Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Zanzibar imeeleza kuwa mnamo sasa tatu za asubuhi maiti ya Marehemu itaondoka Mijini kuelekea Bumbwini Kijijuini kwao kwa kusaliwa na baadae kuzikwa. 
 
 Katika Mazishi hayo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Mohamed Aboud atasoma risala na baadae Baraza la Wawakilishi Zanzibar itatoa risala yake itakayosomwa na Spika wa Baraza hilo Pandu Ameir Kificho na baadae Familia ya Marehemu Salum Amour Mtondoo itatowa tamko la shukrani. 
 
 Tangu Uchaguzi Mkuu Kumalizika wa Mwaka 2010 huyu atakuwa Mwakilisdhi wa pili kufariki Dunia ambapo Mwakilishi wa kwanza kufariki ni Mwakilishi wa Jimbo la Uzini ambae pia alikuwa Mbunge aliechaguliwa na Baraza la Wawakilishi Marehemu Mussa Khamis Silima wote hao wawaili ni kutoka chama cha Mapinduzi.

LOWASSA; NIPO FITI


Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, mara baada ya kuswasili jana kwenye Uwanja wa Kimatiafa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, akitokea kufanyiwa check up jicho Ujerumani na kueleza kuwa yuko fiti kimwili. Kushoto ni Mke wake Rejina.
 
ALIYEKUWA Waziri Mkuu, Edward Lowassa, amesema amerejea nchini salama kutoka Ujerumani na afya yake ni nzuri tofauti na watu walivyomzushia.

Lowassa alisema hayo jana Dar es Salaam mara aliporejea na kuzungumza na waandishi wa habari, huku akikanusha taarifa kwamba anaumwa sana na amepatwa na kiharusi na ndiyo maana ya kwenda kutibiwa Ujerumani.

“Yote haya yaliyoandikwa kwenye mitandao, magazeti na blogu kuhusu afya yangu kuwa mbaya, ni uongo wa kutupwa, kama mnavyoniona, afya yangu ni nzuri na niko ‘fit’ kwa mapambano,” alisema Lowassa.

Akielezea kilichompeleka Ujerumani, Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, alisema miaka mitatu iliyopita, alikwenda huko kutibiwa macho na kufanyiwa upasuaji.

Alisema Profesa aliyemfanyia upasuaji huo, alishauri aende mara kwa mara kuchunguzwa jicho lake ambalo Profesa huyo hakuridhika na maendeleo yake.

“Nimechunguzwa na limekutwa jicho linaendelea vizuri na sina tatizo lolote, lakini pia nikiwa huko, nilipima afya yangu na inaendelea vizuri, mapigo ya moyo wangu ni 120 kwa 80 ambayo ni kawaida, sina shinikizo, kisukari wala lehemu,” alisisitiza.

Alisema ameamua kuzungumzia afya yake, ili wananchi wajue ukweli, kwa sababu kutokana na uzushi kuwa hali yake ni mbaya, baadhi ya watu walishtuka na kumpigia simu hata baadhi ya maaskofu kuamua kumwombea ili apone haraka.

“Nawashukuru wote walionipigia simu na kunitumia ujumbe mfupi kutaka kujua hali yangu pamoja na walioniombea, ila nawaambia kuwa niko salama kabisa,” alisema.

Alipoulizwa swali kuhusu uhusiano wake na mgombea ubunge katika uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki kupitia CCM, Sioi Sumari na ushiriki wake katika kampeni, alikataa kuzungumzia suala hilo, huku akisisitiza kuwa akizungumza lolote kuhusu uchaguzi huo, ataharibu suala zima la afya yake.

“Kuhusu hili la Arumeru ninachojibu ni kwamba niko kimya na wala sitajibu ila kwa wale wanaotaka kuniona baada ya hapa tukutane Arumeru na Ifakara,” alisisitiza. Mkewe, Regina, alisisitiza kuwa hali ya mumewe kiafya ni nzuri na hana tatizo lolote.

Hivi karibuni zimekuwapo tetesi na taarifa kwenye baadhi ya vyombo vya habari, kwamba kiongozi huyo anaumwa sana na amepatwa na kiharusi hali iliyosababisha akimbizwe Ujerumani kutibiwa.

Monday, March 12, 2012

MASHINE YA UINUA MATITI YA WANAWAKE YAINGIA NCHINI TANZANIA




*WANAWAKE WAFURIKA KUPATA HUDUMA

BIASHARA huria imezua mengi. Hali kadhalika Sayansi na Tekenolojia nayo, imeleta mengi. Katika kuwaondolea kero  wanawake wenye matiti yaliyosinyaa hapa nchini, wataalamu kutoka China wameanza kutoa huduma ya kunyanyua matiti hayo kwa kutumia mashine maalumu.

Wachina wamejipatia umaarufu katika kuleta bidhaa mbalimbali hapa nchini, zikiwamo za kuongeza nguvu za kiume, kupunguza uzito, kuotesha nywele, kujichubua (kumfanya mtu mweusi awe mweupe), kuongeza makalio nk.

Huduma hiyo ya kusimamisha matiti yaliyolala, imeanza kutolewa katika Saluni ya Blue Palace, iliyopo nyuma ya Shule ya Mapambano, Sinza jijini Dar es Salaam.

Haikuwa rahisi kuweza kuamini kuwa vitu kama hivi vinaweza kupatikana Tanzania. Mwananchi Jumapili lilifunga safari mpaka kwenye saluni hiyo inayomilikiwa na Sarafina Mtweve, kujionea jinsi teknolojia hiyo inavyofanya kazi.
Mbali na meneja wa saluni hiyo, Trust Mwembe, pia alikuwepo mtaalamu kutoka China aitwaye, Ciisy Pang, ni binti wa miaka 23 tu, lakini anasema kwa miaka minne amefanya kazi hiyo na kuwasaidia wanawake mbalimbali waliokuwa wakikerwa na matiti yaliyolegea au kuanguka.

Pang na kundi lake wanatoa huduma hii kwa gharama ya Sh150,000 kwa kuanzia, ingawa wanahisi gharama hizo zitapanda katika siku chache zijazo.

 Jinsi matiti yanavyosimamishwa
Mashine hiyo inayoitwa ‘Beauty Machine’ ina uwezo wa kusimamisha matiti ya kila saizi kwa kuwa huambatanishwa na vibakuli (cups) kama unavyoona pichani.

Kazi kubwa ya mashine hiyo ni kuamsha misuli ambayo hushikilia nyama za matiti.
Pang anasema, zoezi la kusimamisha matiti huchukua wiki tatu mpaka sita, inategemea aina ya mteja na wakati mwingine juhudi zake.

Mtaalamu huyo ambaye anazungumza Kichina na kutafsiriwa na meneja wa saluni hiyo, anaelezea namna anavyofanya kazi ya kuyarudisha matiti  kwa muda huo.

 “Kwanza unapaswa ujue kuwa hatutumii dawa yoyote katika zoezi hili, mteja wetu akifika hapa, kinachotumika ni mashine tu ambayo hutumia umeme kama zilivyo dryer  za nywele,
“Baada ya kumlaza katika kitanda kile, tunachukua kitu mfano wa bakuli (cups) mbili kulingana na ukubwa wa matiti yake, tunayatumbukiza humo, kisha tunawasha mashine,” anasema Pang.

Mtaalamu huyo anasema mashine hiyo ikiwashwa  inavuta kama ‘vacuum’, na inaweza kuongezwa kasi au kupunguzwa kama inavyofanyika kwenye mashine za kufanyia mazoezi.

“Tunaiwasha mashine kwa muda wa dakika 45, mteja atachagua siku mbili katika wiki za kufanya zoezi hili mpaka litakapokamilika,”anasema Pang.

Tangu mashine hiyo iwasili nchini, takribani mwezi mmoja uliopita, Pang anasema ana wateja wanane anaowahudumia kwa nyakati tofauti ambao wamekiri kuwa maendeleo yanatia moyo.

 Ni kweli mashine hii inasaidia?
 Akizungumza kwa njia ya simu, mmoja wa wateja anayepata huduma hiyo ambaye alijitambulisha kwa jina moja tu Irene anasema, ni wiki ya tatu sasa tangu aanze kupata huduma hiyo, anakiri kuwa matiti yake sasa yameanza kuwa magumu tofauti na mwanzo.

 “Kusema kweli nilikuwa na matiti yaliyosinyaa wala si kulala tu kama ulivyouliza, ila naona sasa yameanza kuwa magumu na kurudi juu kidogo,” anasema Irene.

 Akizungumzia ugumu anaoupata katika zoezi hilo, anasema safari za kila wiki saluni na zile dakika 45 za kukaa kwenye mashine zinamchosha, lakini kwa kuwa amedhamiria, amejitoa mpaka zoezi hilo litakapokamilika.
Matiti yanaweza kulegea tena?

Pang anasema kama matiti yanalegea kwa sababu fulani mfano uzazi wa watoto wengi, basi yanaweza kulegea tena kama mtu atajifungua na kunyonyesha kwa muda huo.Aidha anasema wanawake wenye matiti makubwa, ni rahisi kuanguka kama hawatayavalisha sidiria kwa muda mrefu.

 “Wanawake wenye matiti makubwa huwa nawashauri kuvaa sidiria hasa wakati wa mchana na usiku wanaweza kuacha kuzivaa, hii inasaidia kuimarisha misuli inayoyabeba matiti,” anasema Pang.

 Jamii inazungumziaje jambo hili
Baada ya kusikia kuwepo kwa mashine hii nchini, wanawake mbalimbali wamesema wanatamani kupata huduma hiyo lakini wengine, walionyesha woga juu ya matokeo yake.

 “Ni kweli baada ya kunyonyesha watoto wawili sasa matiti yamelegea kabisa, natamani yarudi kama wakati ule wa usichana wangu, lakini nahofia huenda mbele ya safari nikapata madhara,” anasema Linda Masatu.

Linda anaongeza kusema kuwa ni vizuri mwanamke akawa na matiti yaliyojaa vizuri, lakini anahofia njia zinaweza kuwa na madhara, huku akisema kama ingetokea njia nyingine ya asili asingesita kuifuata.

Naye Batuli Famau, anasema mwanamke anapokuwa na matiti yaliyosinyaa mvuto wake hupungua, hata anapovaa sidiria anakuwa amebadili mwonekano wa nje tu, lakini ndani bado anakuwa vilevile.

“Mwanamke mrembo ni yule mwenye matiti mazuri, sasa inapobidi kutumia njia fulani ili yarudi kama tulipokuwa vigoli, tutafanya tu ili mradi kama njia hizo hazitatuangamiza,” anasema
Wanaume nao wameonekana kuunga mkono zoezi la kusimamisha matiti ingawa wengine hawaungi mkono utumiaji wa mashine hii.

Augustino Magara anasema: “Ni kweli mwanamke mwenye matiti magumu anavutia kuliko yaliolegea na kulala, lakini sasa tuwe makini kabla wake zetu hawajaumia katika mashine, hizi”

“Wote tunajua sababu zilizosababisha matiti ya wake zetu yalegee, sioni sababu ya kusema tunataka yaliyomagumu, tuwapende wake zetu hivi hivi na tuwape moyo,” anasema Nganara.

Dk Innocent Mosha wa Kitengo cha Patholojia Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, anasema ni vigumu kwa wataalamu wa afya kugundua madhara ya mashine hizo kwa haraka hadi pale uchunguzi utakapofanyika.

“Ingelikuwa mazoezi hayo yanachukua muda mfupi, kweli tungepata wasiwasi kwa kuwa, unapoisimamisha misuli kwa haraka ni lazima madhara yatokee, lakini hili la mazoezi, bado sifahamu,” anasema  Dk Mosha.
 Na Julieth Kulangwa, Gazeti la Mwananchi.

Lema na Zitto kivutio kampeni za Chadema Arumeru


Godbless Lema amekuwa kivutio kikubwa alipowasili jana hapa Usa river majira ya saa saba na nusu mchana kutokea Arusha. Alikuwa na maandamano makubwa ya magari,pikipiki,na waenda kwa miguu. Alipokaribia tu kufika vijana wa hapa walimbeba juu wakati wote na kufunga barabara kwa muda mpaka walipompeleka sehemu ambako wageni wanafikia. Baadaye  maandamano makubwa ya kupokea viongozi watakaozindua kampeni yakafuata
  
Mh Zitto Kabwe akiwasili eneo la tukio.
Umati wa watu ukiwa unaelekea eneo la mkutano katika viwanja vya shule ya Msingi Leganza.
Waendesha pikipiki hawako nyuma kama wanavyoonekana katika picha hii.
Barabara za kutokea Moshi na Arusha zimefurika watu wakija kwenye uzinduzi wa CHADEMA.
Picha na Habari na Mdau Maalum Wa Maggid Mjengwa-Arumeru

PINDA AKAGUA UJENZIKITUO CHA MIKUTANO CHA JULIUS KAMBARAGE NYERERE.



 Waziri Mkuu, Mizengo Pinda  akikagua ujenzi wa Kituo cha kimataifa cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Kambarage Nyerere kwenye Mtaa wa Shaaban Robert jijini Dar es salaam. Kushoto kwake ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Kulia kwake ni Balozi wa China nchini,  LV Youqing
Waziri Mkuu, Mzengo Pinda akijadili jambo na  Waziri wa mamboya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe (kulia) , Balozi wa China Nchini, LV Youqing baada ya kukagua ujenzi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere , Mtaa wa Shaban Robert jijini Dar es salaam. Wengine pichani na wahadisi  kutoka China wanaosimmia ujezi huo. 


WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amezitaka kampuni na taasisi zinazohusika na kutoa huduma muhimu katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwl. Julius Kambarage Nyerere ziharakishe kufanya hivyo ili ujenzi wake ukamilike mapema.
Ametoa kauli hiyo juzi mchana (Jumamosi, Machi 10, 2012) mara bada ya kupokea taarifa ya ujenzi wa kituo hicho na kukagua ujenzi wake katika mtaa wa Shaaban Robert jijini Dar es Salaam. 
Kampuni zinazotakiwa kufanya hivyo ni TANESCO kwa ajili ya umeme wa jengo hilo, Kampuni ya Simu (TTCL) kwa ajili ya mkonga wa mawasiliano na Idara ya Kodi ya Mapato (TRA).
Waziri Mkuu amesema ujenzi wa kituo hicho cha mikutano ni ishara ya urafiki wa muda mrefu ulikuwepo baina ya Tanzania na China na kwamba kukamilika kwake kutaboresha mandhari ya Jiji la Dar es Salaam.
Mapema, akitoa taarifa kuhusu ujenzi wa jengo ambalo litagharimu yen milioni 183.5 sawa na dola za Marekani milioni 30, Balozi wa China nchini Tanzania, Bw. Lv Youqing alisema ujenzi wa jengo hilo ulianza mara baada ya sherehe za uzinduzi Januari 15, 2010.
Awali, ujenzi wa jengo hilo ulitarajiwa kukamilika Aprili, 2012 lakini kutokana na uchelewashaji wa miundombinu hiyo muhimu hivi sasa linatarajiwa kukamilika Agosti, mwaka huu.
Litakapokamilika jengo hilo litakuwa na uwezo wa kuchukua watu zaidi ya 1,000; litakuwa na kumbi ndogo ndogo nne zenye uwezo wa watu zaidi ya 20, ukumbi wa chakula wa watu zaidi ya 700 na ofisi za watumishi wa ukumbi huo. Vilevile, kutakuwa na ukumbi mmoja ambao unaweza kugawanywa (partitioned) na kutengeneza ofisi za muda kwa watu wanaoendesha mkutano mkubwa katika ukumbi huo.
Naye Mkurugenzi wa mradi wa ujenzi wa kituo hicho, Bw. Huang Meiluan alisema ujenzi wa ghorofa ya chini umekamilika kwa asilimia 40 kwa sababu bado wanasubiri huduma muhimu zikamilike ili waanze kuweka sakafu. “Tunasubiri kuunganishwa na mkonga wa mawasiliano wa Taifa, bado hatujaweka njia kuu za umeme za kuingia katika jengo... kasi ya ujenzi imeathirika kutokana na kutokamilika kwa huduma hizi muhimu,” alisema.
Alisema ujenzi wa ghorofa ya kwanza na ya pili umekamilika kwa asilimia 90 na imebakia kazi ya kumalizia kuweka nakshi za ndani tu (interior decoration). “Kwa nje, kazi ya ujenzi imekamilika na tumeanza kuweka nakshi, kazi hii imekamilika kwa asilimia 75,” alisema.
Alisema wanakabiliwa na changamoto ya wizi wa vifaa vya ujenzi unaofanywa na vibaka kila mara na kwamba inawapa mtihani kwani itawalazimu kuagiza upya vifaa hivyo kutoka China. Aliomba polisi wawasaidie kuimarisha ulinzi katika eneo la ujenzi.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe alimweleza Waziri Mkuu kwamba wizara yake imeanza kushughulikia upatikanaji wa kifaa muhimu cha umeme ambacho kilishindwa kupatikana hapa nchini.
Alisema vyuma vilivyotumika katika hatua za awali za ujenzi wa kituo hicho ni tani nyingi, na kwamba yanahitajika malori ya kuvisomba na kibali kutoka TRA ili yaweze kupelekwa katika eneo jingine kwa kuhifadhiwa. Alimhakikishia Waziri Mkuu kwamba wizara yake inafuatilia suala hilo pia.
Kuhusu uwekwaji wa nyaya za mkonga wa mawasiliano ambao unapaswa kufanya na TTCL, waziri Membe aliomba apewe wiki moja zaidi kwani amekuwa akisumbuana nao kwa zaidi ya mwezi mmoja bila mafanikio yoyote. Suala la ulinzi pia alisema ameshaanza kulishughulikia.