Saturday, October 9, 2010

kufanya kampeni kwa kutumia udini na ukabila ni kuhatarisha amani - mama salma kikwete

Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), Mama Salma Kikwete

NA MWANDISHI MAALUMU, KIGOMA

MWENYEKITI wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), Mama Salma Kikwete, amesema kufanya kampeni kwa kutumia udini na ukabila ni kuhatarisha amani.

Alisema hayo juzi na jana alipozungumza kwa nyakati tofauti na wanachama wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) mkoani hapa, alipokuwa akiwaombea kura wagombea wa Chama Cha Mapinduzi katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 31, mwaka huu.

Mama Salma alisema kuwagawa Watanzania kwa misingi ya udini na ukabila ni kutaka kutowesha amani ambayo imedumu nchini kwa miaka mingi.

“Udini na ukabila utatutenganisha, tutahasimiana kwa sababu huyu ni mkristo na yule ni muislamu, haya ni yale yale ya huyu ni Mtutsi na yule ni Mhutu, jamani kina mama huko ndiko tunataka kwenda ?” Alihoji na kujibiwa “hapana”.

Mama Salma alisema, wanachama wa vyama vya siasa wana dini zao, lakini usajili wa vyama hivyo haufanyiki kwa kuangalia dini na kabila, hivyo kufanya kampeni kwa vigezo hivyo ni ukiukaji wa sheria.

Wakati akizungumzia hilo, kina mama hao walikuwa wakimwitikia kwa kusema “sema mama usiogope” kuashiria kuna baadhi ya watu wanafanya kampeni za kibaguzi kwa kutumia udini na ukabila.

Mwenyekiti huyo wa WAMA ambaye ni mke wa mgombea urais wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, alitahadharisha kwamba, amani kuvunjika ni rahisi, kuirejesha ni kazi kubwa na mifano ipo katika baadhi ya nchi za Afrika ambazo ziliichezea na haijarejea.

Aliwaambia wananchi wa Kigoma kwamba wao ni mashahidi wa namna nchi jirani zilivyoathirika kutokana na machafuko chanzo kikiwa ni siasa za kibaguzi zilizojiegemeza kwenye udini na ukabila.

Mama Salma aliwaombea kura wagombea ubunge kwa tiketi ya CCM; Injinia Christopher Chiza (Buyungu), Jamal Tamimu (Muhambwe), Daniel Nsanzugwanko (Kasulu Vijijini), Raphael Neka (Kasulu Mjini), Robson Lembo (Kigoma Kaskazini), Peter Serukamba (Kigoma Mjini) na Gulamuhussein Kifu (Kigoma Kusini).

No comments:

Post a Comment