MWIMBAJI mahiri wa muziki wa Injili, Rose Muhando amelalamika kuwa albamu yake ya Kamata Pindo la Yesu Albamu anayotarajia kuizindua Jumapili wiki hii imeingizwa mtaani na wezi wa kazi za wasanii, hivyo kuonya wananchi wawe makini kwani albamu yake halisi itatoka Jumapili.
Taarifa kwa vyombo vya habari aliyoitoa Muhando jana, ilieleza kuwa albamu yake halisi bado haijaingia mtaani na kwamba hiyo wanayoiona wananchi sasa ni bandia na mtu atakayewauzia wamripoti polisi.
“Albamu ya Kamata Pindo la Yesu itaanza kuingia mtaani baada ya uzinduzi wangu kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee Jumapili wiki hii. Albamu yangu ina nembo ya TRA (Mamlaka ya Kodi ya Mapato nchini).
“Hizi CD zinazouzwa hivi sasa si zangu, hao ni matapeli na nawaomba wananchi tushirikiane kudhibiti wizi. Hao ni maharamia wa kazi za wasanii wanataka kunyonyajasho langu, naomba sana wananchi mnisaidie.“Nasisitiza albamu yangu sijaiachia sokoni bado mpaka uzinduzi ukamilike, Watanzania wenzangu na mashabiki wangu kote duniani mnielewe na naomba tusaidiane katika hili maana CD feki zimezagaa,” alisema Muhando na kuongez akuwa tayari ameripoti taarifa hiyo kwa vyombo vya dola.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions inayoratibu uzinduzi huo, Alex msama naye katika taarifa hiyo ya pamoja alionya wote watakaobanika kuwa CD za albamu ya Rose Muhando watakumbana na mkono wa sheria.
“Inasikitisha sana kuona baadhi ya watu wanataka kutumia jasho la wengine kujinufaisha. Watanzania kuweni macho, msubiri albamu yenyewe ya Rose Muhando Jumapili pale ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam,” alisema Msama.
Albamu hiyo ya Muhando itakayozinduliwa Jumapili ina nyimbo za Bwana Niongoze, Wewe Waweza, Usiniache, Nibariki, Muongo, Kwema, Kamata Pindo la Yesu na Facebook.
Hivi sasa Rose anatamba na albamu yake ya Utamu wa Yesu, ambapo pia amewahi kutamba na albamu za Uwe Macho, Nyota ya Ajabu (Zawadi ya Krismasi), Jipange Sawasawa, Kitimutimu, Mungu Anacheka na Wololo.
No comments:
Post a Comment