Aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa Mtibwa Sugar msimu uliopita na sasa amejiunga na Simba sc, Shaaban Kisiga ‘Malone’ (kushoto) akimiliki mpira mbele ya wachezaji wa Yanga, Athuman Idd ‘Chuji’ (katikati) na Mbuyu Twite (kulia)
Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam,
Miaka 12 iliyopita katika uwanja wa Nambole, jijini, Kampala, timu ya Simba SC ilikuwa katika kiwango cha juu katika michuano ya kombe la Kagame. Simba ambayo ilifika robo fainali ya ligi ya mabingwa Afrika mwaka mmoja baadaye chini ya Mwalimu, Mkenya, James Siang’a timu hiyo ilikuwa kamili kila idara na ilikaribia kuvunja rekodi yao mbaya kama mabingwa mara nyingi wa klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati ( mabingwa mara sita) ambao hawajatwaa taji lolote nje ya ardhi ya Tanzania.
Simba ilipoteza mchezo wa fainali mbele ya wenyeji, timu ya Sports Club Villa kwa bao 1-0. Shaaban Kisiga ‘ Malone’ aliwatesa viungo wa Simba kama Suleimani Matola, Shekhani Rashid, Kisiga akichipukia. Kiungo huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania alipiga pasi ya mwisho kwa Bernad Mwalala na mshambuliaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Kenya akafunga bao pekee. Licha ya kuonyesha kiwango cha juu katika michuano, Kisiga hakutulia nchini Uganda kutokana na mambo ya kiusalama.
Siang’a alipendekeza mchezaji huyo pamoja na Primus Kasonso wasajiliwe kwa ajili ya msimu wa mwaka, 2003, ila hakufanikiwa kumpata, Kisiga na badala yake aliwapata Christopher Alex na Ulimboka Mwakingwe kutoka Reli FC ya Morogoro na Primus kutoka Tanzania Prisons ya Mbeya. Simba ilifanya kwa mwaka wote wa 2003, na wakati wa usajili ulipofika kwa ajili ya msimu wa mwaka 2004. Kisiga alikuwa ni miongoni mwa wachezaji waliosajiliwa wakati huo.
Kisiga alicheza Simba kwa miaka miwili. Msimu wake wa kwanza ulikuwa na mafanikio makubwa, licha ya kuwa kiungo mbunifu katikati ya uwanja, Kisiga ni mshambuliaji mzuri wa pili, namaanisha namba 10. Kutokana na utitiri wa vipaji katika nafasi ya kiungo, Mwalimu, Siang’a mara nyingi alikuwa akimtumia kama mshambulizi wa pili sambamba na Athumani Machuppa. Alipoondoka, Siang’a alikuaja, Mzambia, Patrick Phiri ambaye alikuwa akimtumia zaidi Kisiga kama kiungo wa pembeni au mshambuliaji wa pili.
Trott Moloto, kocha raia wa Afrika Kusini alipochukua nafasi ya Phiri kama kocha mkuu wa Simba mwanzoni mwa mwaka, 2005 alisema wazi kuwa hatowatumia Machuppa na Kisiga kama washambuliaji na katika mchezo wake wa kwanza wa mashindano dhidi ya Enyimba ya Nigeria katika klabu bingwa Afrika katika uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Moloto aliwaweka benchi Kisiga na Machuppa huku mshambulizi mwenye umbo kubwa, Nurdin Msiga akiongoza safu ya mashambulizi. Simba ililazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 huku Nurdin akifunga bao pekee la Simba ambalo lilikuwa la kusawazisha.
Mashabiki walikuja juu kutokana na kitendo cha wachezaji hao kuanzia benchi na kupangwa katika nafasi tofauti. Moloto alisema kama Simba ilikuwa ikihitaji kufanya vizuri katika michuano ya vilabu barani Afrika ni kutowachezesha, Kisiga na Machuppa kama washambuliaji pekee kutokana na maumbo yao madogo.
Moloto alipangiwa timu katika mchezo wa marejeano, Aba, Nigeria huku Kisiga na Machuppa wakirudishwa katika majukumu ya ufungaji na Simba ikatandikwa mabao 4-0. Mwalimu huyo raia wa Afrika Kusini akaondoka zake lakini Simba haikuweza kunyanyuka hata ilipokuwa chini ya Mwalimu wa muda, Jamhuri Kiwelo ‘ Julio ‘. Kisiga aliondoka Simba na kwena kucheza soka la kulipwa nje ya nchi mara baada ya kumalizika kwa msimu wa mwaka, 2005.
ARUDI SIMBA SC BAADA YA MIAKA TISA. ……
Kiwango cha juu ambacho alikionyesha katika msimu uliopita akiwa na timu ya Mtibwa Sugar bila shaka kimekuwa na mafanikio huku akipata heshima kama mmoja wa viungo bora wachezesha timu nchini. Aliwafunika chipukizi wa Simba kama Jonas Mkude na Said Ndemla katika mchezo wa Mwezi Februari na akaendelea kuwa bora katika mchezo dhidi ya Yanga, hiyo si sababu ya kusajiliwa tena na Simba, bali mchezaji huyo atatumika kuimarisha timu inayojipanga kwa kutumia wachezaji vijana zaidi. Kwa misimu miwili iliyopita Kisiga amekuwa mchezaji wa kiwango cha juu katika timu ya Mtibwa. Siku zote anacheza vizuri zaidi katika mechi kubwa jambo ambalo linafanya kuwepo na sababu muhimu ya kumsaini.
Msimu uliopita, Simba haikupata ushindi wowote katika michezo sita dhidi ya timu za Azam FC, Yanga na Mbeya City FC hivyo ni wazi kuwa kuna maeneo timu hiyo ilikuwa ikizidiwa, eneo la kiungo ni sehemu ya kwanza. Kisiga hatocheza mechi zote, ila anaweza kucheza mechi zote muhimu na kutoa matunda mazuri. Kisiga amesajiliwa kwa sababu ya uwezo wake, pia maisha yake marefu katika soka, na jinsi anavyojiandaa na kupenda kwake mchezo wenyewe. Huyu ni sehemu ya mfano wa kuigwa kwa vijana wa Kitanzania,
Kisiga si yule wa SS Villa vs Simba SC, 2002, ila amekuwa na mchezo uleule, wachache wamejitunza kwa muda mrefu kama huo. Kisiga ni mchezaji wa Simba, alivyo, kiuchezaji. Kisiga ni kiungo bora wa kupiga pasi za mwisho na mchezaji anayejiamini muda wote uwanjani.
No comments:
Post a Comment