Friday, March 16, 2012

LOWASSA; NIPO FITI


Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, mara baada ya kuswasili jana kwenye Uwanja wa Kimatiafa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, akitokea kufanyiwa check up jicho Ujerumani na kueleza kuwa yuko fiti kimwili. Kushoto ni Mke wake Rejina.
 
ALIYEKUWA Waziri Mkuu, Edward Lowassa, amesema amerejea nchini salama kutoka Ujerumani na afya yake ni nzuri tofauti na watu walivyomzushia.

Lowassa alisema hayo jana Dar es Salaam mara aliporejea na kuzungumza na waandishi wa habari, huku akikanusha taarifa kwamba anaumwa sana na amepatwa na kiharusi na ndiyo maana ya kwenda kutibiwa Ujerumani.

“Yote haya yaliyoandikwa kwenye mitandao, magazeti na blogu kuhusu afya yangu kuwa mbaya, ni uongo wa kutupwa, kama mnavyoniona, afya yangu ni nzuri na niko ‘fit’ kwa mapambano,” alisema Lowassa.

Akielezea kilichompeleka Ujerumani, Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, alisema miaka mitatu iliyopita, alikwenda huko kutibiwa macho na kufanyiwa upasuaji.

Alisema Profesa aliyemfanyia upasuaji huo, alishauri aende mara kwa mara kuchunguzwa jicho lake ambalo Profesa huyo hakuridhika na maendeleo yake.

“Nimechunguzwa na limekutwa jicho linaendelea vizuri na sina tatizo lolote, lakini pia nikiwa huko, nilipima afya yangu na inaendelea vizuri, mapigo ya moyo wangu ni 120 kwa 80 ambayo ni kawaida, sina shinikizo, kisukari wala lehemu,” alisisitiza.

Alisema ameamua kuzungumzia afya yake, ili wananchi wajue ukweli, kwa sababu kutokana na uzushi kuwa hali yake ni mbaya, baadhi ya watu walishtuka na kumpigia simu hata baadhi ya maaskofu kuamua kumwombea ili apone haraka.

“Nawashukuru wote walionipigia simu na kunitumia ujumbe mfupi kutaka kujua hali yangu pamoja na walioniombea, ila nawaambia kuwa niko salama kabisa,” alisema.

Alipoulizwa swali kuhusu uhusiano wake na mgombea ubunge katika uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki kupitia CCM, Sioi Sumari na ushiriki wake katika kampeni, alikataa kuzungumzia suala hilo, huku akisisitiza kuwa akizungumza lolote kuhusu uchaguzi huo, ataharibu suala zima la afya yake.

“Kuhusu hili la Arumeru ninachojibu ni kwamba niko kimya na wala sitajibu ila kwa wale wanaotaka kuniona baada ya hapa tukutane Arumeru na Ifakara,” alisisitiza. Mkewe, Regina, alisisitiza kuwa hali ya mumewe kiafya ni nzuri na hana tatizo lolote.

Hivi karibuni zimekuwapo tetesi na taarifa kwenye baadhi ya vyombo vya habari, kwamba kiongozi huyo anaumwa sana na amepatwa na kiharusi hali iliyosababisha akimbizwe Ujerumani kutibiwa.

No comments:

Post a Comment