Na Mindi Kasiga,Wisiconcin,Marekani
Meya wa Milwaukee kwenye Jimbo la Wisconsin amemtunukia Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mhe. Mwanaidi Sinare Maajar hati ya kuitambua siku ya tarehe 20.02.2012 kama siku ya Tanzania mjini Milwaukee.
Mayor Thomas Barrett ametangaza siku hiyo ofisini kwake leo (jana) kama sehemu ya kuipongeza Tanzania kwa kutimiza miaka 50 ya uhuru na kuendeleza ushirikiano baina ya miji dada (sister cities) ya Milwaukee nchini Marekani na Morogoro nchini Tanzania.
Katika hafla hiyo fupi iliyohudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo waandishi wa habari, Meya Barrett na Balozi Maaajar walikubaliana kuendeleaza ushirikiano baina ya miji hii miwili, ulioanzishwa mwaka 2006, na pia kushawishi wawekezaji na wafanya biashara wa ukanda huu wa Marekani kuwekeza Tanzania.
Balozi Maajar yuko Jimboni Wisconsin kwenye ziara ya kikazi ya siku tatu iliyoandaliwa na muasisi wa ushirikiano wa miji ya Milwaukee na Morogoro Bw. Ryan Skyfe, ambapo anakutana na taasisi za elimu, biashara na wawekezaji mbalimbali kwa nia ya kuangalia maeneo ya ushirikiano wenye tija ili kuleta maendeleo kwa manufaa ya wananchi wa nchi hizo mbili.
Baadhi ya taasisi alizofanya nao mazungumzo ni Milwaukee Area Technical College walioko kwenye Jimbo la Wisconsin mjini Milwaukee ambao wamekubali kushirikiana na mojawapo ya chuo cha Tanzania na kutoa elimu inayolingana na mitaala ya chuo hicho ambacho kinaongoza kwenye Jimbo hili kwa kutoa elimu ya vitendo kwenye sekta ya nishati ya umeme inayowasaidia Wamerekani kupata ajira.
Wengine ni Phoenix Financial & Investment Services walioko Jimbo la Illinois mjini Chicago na Helios Solar Works walioko Jimbo la Wisconsin Mjini Milwaukee. Balozi Maajar pia alipata fursa ya kutoa mada kwenye mkutano uliovutia wakuu wa biashara na wawakilishi wa makampuni wapatao thelathini kutoka kwenye Jimbo la Wisconsin wenye nia ya kuwekeza nchini Tanzania.
Aidha Balozi Maajar alitumia fursa hiyo kuirajamu Tanzania na kutangaza fursa mbalimbali zilizopo baina ya serikali za nchi hizi mbili kwa wananchi wake kuwekeza na kuendeleza ushirikiano kwa manufaa yao.
Kila mwaka Balozi wa Tanzania nchini Marekani huandaa ziara mahsusi kwa ajili ya maafisa wakuu wa makampuni ya kimarekani kutalii Tanzania na kuangalia fursa za uwekezaji na biashara nchini Tanzania. Ziara hiyo ambayo inachanganya biashara na utalii (business and leisure) imekuwa mashuhuri sana miongoni mwa wafanyabiashara wa Kimarekani ambapo mwaka huu inatarajiwa kufanyika tarehe 22 Juni – 02 Julai, 2012.
Balozi Maajar tarehe 21.02.2012 alitarajia kukutana na Gavana wa Jimbo la Wisconsin Mjini Madison na baadae kuendelea na ziara yake kwenye miji ya La Farge na La Crosse Jimboni Wisconsin kabla ya kurejea mjini Washington, jimbo la District of Columbia.
No comments:
Post a Comment