Monday, January 30, 2012

GABON YASONGA MBELE ROBO FAINALI

Gabon ilifanikiwa kupata ushindi wa magoli 3-2 katika dakika ya mwisho, ilipocheza dhidi ya Morocco siku ya Ijumaa, na kufuzu kuingia robo fainali katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika. Mechi hiyo ilichezewa mjini Libreville.
Kwa muda mrefu, Morocco ilikuwa ikiongoza kwa bao 1-0 katika mchezo huo, bao ambalo lilikuwa limepatikana kupitia nahodha Houssine Kharjah katika kipindi cha kwanza.
Lakini kupitia magoli ya Pierre-Emerick Aubameyang na Daniel Cousin, wenyeji Gabon waliweza kuongoza, hadi mkwaju wa Kharjah ulipoiwezesha Morocco kupata nafasi ya kwanza, na ilielekea mechi itaishia kwa sare ya 2-2.
Lakini Morocco walipoadhibiwa kwa kucheza vibaya, Bruno Zita Mbanangoye alipiga mkwaju kwa ufundi mkubwa, na mpira ulipinda hadi kuingia wavuni, na bao hilo la wakati wa majeruhi likawa ndio kwaheri kwa timu ya Morocco.
Gabon sasa inajiunga na wenyeji wenzao Equatorial Guinea, katika hatua ya robo fainali.
Equatorial Guinea walifanikiwa kuiondoa Senegal siku ya Jumatano, taifa ambalo lilitazamiwa na wengi kuwa miongoni mwa nchi ambazo zilikuwa katika nafasi nzuri ya kuibuka bingwa katika mashindano ya mwaka huu.
Katika mechi ya awali siku ya Ijumaa, ambayo pia ilichezewa mjini Libreville, Niger iliondolewa na Tunisia, kwa kufungwa magoli 2-1.
Hata hivyo Niger ilikuwa bado na matumaini ya kusonga mbele, ikitazamia Morocco kuwafanyia kazi yao, kama ingeliweza kuishinda Gabon.
Lakini hayo hayakuwezekana, na hivyo basi Niger inajiunga na Morocco katika safari ya kurudi nyumbani.
Mechi za Jumamosi pia zinatazamiwa kuwa za kusisimua, wakati Botswana itakapokutana na Guinea, na Ghana nayo itacheza na Mali.
Mechi zote mbili ni za kundi D, na zote zitachezewa mjini Franceville.

               chanzo kamanda wa matukio

No comments:

Post a Comment