Sunday, January 15, 2012

WAKONGO WAMFUNIKA CHARLES BABA



Na Mwandishi Wetu MWIMBAJI nguli nchini aliyeihama bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta' na kutua Mashujaa Musica, Charles Gabriel 'Chaz Baba', ameanza vibaya kutambulishwa katika bendi yake mpya, kutokana na 'kufikikwa' na wanamuziki wenzake ambao wengi wanatoka Jamhuri ya Kidemokarsia ya Congo. Onesho hilo lililoshirikisha bendi tatu mahasimu za Mashujaa Musica, Mapacha Watatu na Extra Bongo, lengo likiwa ni kuungana 'kuiua' Twanga Pepeta, lilifanyika jana usiku kwenye ukumbi wa Business, Dar es Salaam, likijaza mashabiki kochokocho ambao wengi walikwenda kumuona Chaz Baba kwa mara ya kwanza tangu ajiunge na bendi hiyo. Hata hivyo, tofauti na matarajio ya mashabiki wengi kwamba Chaz Baba angeingia na mambo mapya, alijikuta akifunikwa na waimbaji wenzake wa Mashujaa waliotawala jukwaa. Waimbaji wa Mashujaa wakiongozwa na Jado Field Force, Mirinda Nyeusi, Pasia Budansi 'BlackBerry', Raja Radha, Kajo Litungu, Sauti ya Radi, Kelvin Ulaka, Maga One Star, Thelathini na Tatu '33' na wengine, ndio waliong'ara katikla hilo lililokuwa maalumu kumtambulisha Chaz Baba. Chaz Baba aliingia ukumbini kwa mbwembwe, huku akisindikizwa na mashabiki wake waliokuwa wamebeba bango la kumkaribisha katika bendi hiyo inayomilikiwa na Mkurugenzi wa Mashujaa Group, Sakina Mbange 'Mamaa Sakina' akishirikiana na mumewe, Hoseah Hopaje 'Maisha'. Awali, kabla ya Mashujaa kupanda jukwaani, bendi ya Extra Bongo chini ya Ally Chocky ilipanda jukwaani na kupiga nyimbo za Mtenda Akitendewa, Fisadi wa Mapenzi na Falsafa. Kivutio kikubwa kwa Extra Bongo alikuwa Ramadhan Masanja 'Banza Stone', aliyelimudu jukwaa vyema na kuwafanya mashabiki wa muziki wa dansi kupagawa kutokana na uimbaji wake. Bendi ya Mapacha Watatu, ilipanda jukwaani ikiwa na Khalid Chuma 'Chokoraa', Jose Mara, Kalala Junior na walimkaribisha Chaz Baba kuimba naye. Hata hivyo, mpangilio wa upangaji ratiba ulionekana 'kuwaboa' baadhi ya mashabiki, huku washereheshaji wakiongozwa na Meneja wa Mapacha Watatu, Hamis Dacorta, wakichombeza majigambo mengi na kuinyima Extra Bongo nafasi ya kutumbuiza kwa ufasaha, hali iliyomkera Chocky na kuondoka ukumbini mapema. Chaz Baba alijiengua Twanga Pepeta wiki iliyopita akidai kwamba alikuwa ikifanya kazi ya 'deiwaka', bila kuwa na mkataba, lakini kwa sasa amesaini mkataba wa miaka miwili Mashujaa inayodaiwa kumpatia sh. milioni 10 na gari aina ya Noah.

No comments:

Post a Comment