Monday, January 16, 2012

Serikali yapewa saa 72 kuwarejesha madaktari Muhimbili

CHAMA cha Madaktari Tanzania (MAT), kimeipa Serikali saa 72, kuwarejesha Hospitali ya Taifa Muhimbili, Wanafunzi waliofuzu udaktari waliondolewa hapo baada ya kugoma wakidai malipo yao. Tamko hilo lilitolewa na Rais wa chama hicho, Dk Namala Mkopi katika mkutano na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana. Chama hicho kimemuomba Rais Jakaya Kikwete, kuwatafutia kazi nyingine, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Deo Mtasiwa kwa kosa la kumshauri vibaya Waziri wa wizara hiyo, Dk. Hadji Mponda. Alisema Dk. Mponda anasamehewa kwani hajui alitendalo ila inatakiwa awaombe radhi kwa kuwaita madaktari wenzao kuwa si madaktari bali bado wangali wanafunzi. Rais wa MAT, Dk. Mkopi, pia alitangaza kuwa kimefutia uanachama kwa mwaka mmoja, Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Mtasiwa kwa kosa lake la kuusaliti udaktari kutokana na kukiuka kiapo cha udakatari kinachosema kuwa Madaktari wote ni ndugu na nitawatendea haki kama dada na kaka. Alisema endapo Dk. Mtasiwa atanendelea na tabia hiyo ya kudharau taaluma ya udakatari, basi chama kitaamua kumfukuza kabisa na kumuweka kwenye mtandao wa madaktari duniani, ili iwe fundisho kwa madaktari wengine wenye tabia hiyo. Dk. Mkopi alisema kuwa chama kimesikitishwa sana na kwamba hawaoni ni kwa nini Serikali imeamua kuwaadhibu madaktari wenzao waliokuwa wakidai haki ya msingi, na kuwaacha kuwaadhibu watu waliosababisha ucheleweshaji wa makusudi wa kutowalipa malipo yao madaktari. Kwa habari zaidi soma hapa: http://richard-mwaikenda.blogspot.com/

No comments:

Post a Comment