Rais msaafu Ali Hassan Mwinyi (aliyevaa suti ya kijivu) akipewa maelezo mafupi na Ofisa Uhusiano wa Benki ya Posta Tanzania (TPB), Noves Mosses (wa kwanza kulia) alipotembelea banda la benki hiyo leo katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere-Sabasaba jana. Kutoka kushoto ni Msemaji Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Ingiahedi Mduma akifuatiwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Ramadhani Khijjah.
BENKI ya Posta Tanzania (TPB) mwakani imejipanga kuhakikisha inaweka utaratibu mzuri utakaowawezesha wananchi vijijini hasa wakulima kuweza kutumia huduma za kibenki maeneo ya vijijini.
Akizungumza na Thehabari.com leo jijini Dar es Salaam kuelezea mafanikio ya TPB ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, katika maonesho ya maadhimisho ya sherehe hizo, Ofisa Uhusiano wa Benki ya Posta, Bi. Noves Moses amesema lengo la taasisi hiyo ni kuhakikisha huduma zao zinamfikia Mtanzania wa kawaida vijijini.
Alisema kwa sasa Benki ya Posta inatoa huduma za kibenki katika wilaya zote nchini ambayo imeweza kuwanufaisha baadhi ya wananchi wa kawaida wakiwemo wakulima vijijini.
“Benki ya Posta kwa sasa tuna matawi 28 nchi nzima, hii ni kwa maana ya mikoa yote...na pia tunatoa huduma zetu za kibenki kwa mawakala 151 wa Shirika la Posta na Simu nchini, hivyo huduma zetu kwa kiasi kikubwa zinawanufaisha hata wakulima wa vijijini tofauti na benki nyingine zinazoishia mijini,” alisema Bi. Moses.
Aidha akizungumzia mafanikio ya Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, alisema TPB imepiga hatua kubwa kwa sasa kwa kipindi hicho hasa katika kuongezeka kwa mtandao wa utoaji huduma kutoka tawi moja hadi kufikia matawi 28. alisema maeneo mengine ni pamoja na kuifanya benki hiyo kutoa huduma za kisasa zinazoenda na wakati.
“Awali TPB wateja walikuwa wanatumia vitabu vidogo, ambapo kila mteja alikuwa akipewa huduma na kumbukumbu zake kuhifadhiwa kwenye kitabu chake na benki…sasa hivi hatutumii tena vitabu mteja anatumia kadi ambayo pia imeunganisha katika mitandao mingine ya benki (Umoja Switch) hivyo kumuwezesha mteja wetu kupata huduma za ATM katika wigo mpana,” alisema Ofisa Habari huyo.
Pamoja na huduma hizo, pia ameongeza kuwa TPB inatoa huduma za haraka kwa wateja wake na nafuu ukilinganisha na benki nyingine nchini hivyo kuwataka Watanzania kujitokeza na kujiunga na benki hiyo ya Kizalendo ambayo inamilikiwa kwa asilimia kubwa na Serikali yenyewe.
“Watanzania wana kila sababu ya kutuunga mkono maana hii ni benki yao, inamilikiwa na Serikali kwa asilimia 75. Lengo letu ni kuhakikisha tunamfikia Mtanzania wa kawaida kijijini, tumeanza na TPB Popote yaani huduma inayotoa huduma zote za kibenki kwa wateja wetu kupitia simu ya mkononi,” alifafanua Bi. Moses.
No comments:
Post a Comment