Tuesday, December 13, 2011

POLISI MKOA WA TANGA WAPONGEZWA KWA KUDHIBITI UHALIFU NA AJALI ZA PIKIPIKI


Na Mohammed Mhina, Handeni Wananchi wa Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga, wamepongeza juhudi zinazochukuliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo katika kukabiliana na uhalifu wa utekaji wa magari na makosa ya usalama barabarani.
Wakizungumza katika kikao cha maendeleo ya Kijiji cha Makanya, Mzeri wilayani Handeni, wananchi hao wamesema kuwa uhalifu wa utekaji wa magari na kuporwa mali za abiria uliokuwepo siku za nyuma wilayani Handeni hivi sasa vimekoma kabisa kutokana na kuimarishwa kwa doria hizo za barabarani.
Mzee Hussein Ramadhani, amesema kuwa kuimarishwa kwa doria hizo, pia kumepunguza matukio ya ajali za barabarani zikiwemo zile zinazosababishwa na uendeshaji wa pikipiki maarufu kama bodaboda bila ya leseni ama kuvaa kofia ngumu za kujikinga na ajali.
Wananchi hao wamesema mikakati ya pamoja inayochukuliwa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga ACP Costantino Masawe na Mkuu wa Upelelezi wa mkoa huo SSP Jaffari Mohammed zimewezesha hali ya wilaya ya Handeni na mkoa mzima wa Tanga kuwa shwari.
Wamesema juhudi za pamoja zinazofanywa na Mkuu wa Polisi wa wilaya ya Handeni SSP Seith Mwakajinga, Mkuu wa Upelelezi SP Aziz Kimata na Mkuu wa Kituo cha Polisi Handeni ASP Peter Ngoro, zimepelekea kuimarika kwa hali ya Ulinzi na Usalama wilayani humo.
Naye Mzee Mwinjuma Rashidi Tilibwinda, amewataka Polisi kutowaoenea haya wale wote wanaoendesha pikipiki na kubeba abiria huku wakiwa hawana leseni za udereva ama kuvaa kofia ngumu vichwani za kuwakinga na madhara wapatwapo na ajali ili kupunguza ajali za barabarani zitokanazo na uendeshaji mbaya wa pikipiki.
Amesema kuwa mara nyingi wanaoendesha pikipiki hizo ni vijana wadogo ambao uwezo wao wa kufikiri na kuchukua tahadhari za kujiepusha na ajali ni mdogo.
Pamoja na pongezi hizo, za kuwadhibiti wapanda pikipiki, lakini Mzee Tilibwinga amependekeza kuwepo na elimu juu ya matumizi salama ya vyombo vya moto kwa vijana hao kwa lengo la kuwaepushia na matukio ya ajali za barabarani.
Wamesema kama mikoa mingine ingeweza kuiga mfano huo, ni wazi kuwa uhalifu na ajali za barabarani hapa nchini ungeweza kukoma kabisa.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoani Tanga ACP Costantino Masawe, amesema kuwa Jeshi la Polisi mkoani humo litaendelea kuimarisha doria katika barabara mbalimbali ili kuwahakikishia wananchi usalama wao.
hata hivyo Kamanda Masawe ametoa wito wananchi wanaoishi kandokando mwa barabara kuu mkoani humo, kutoa taarifa Polisi wanapoona dalili za kuwepo kwa vitendo vya kihalifu vikiwemo vya madereva kuendesha mwendo wa kasi ili kunusuru abiria hasa katika kipindi hiki cha kuelekea siku kuu za mwisho wa mwaka.

No comments:

Post a Comment