Na Mwandishi Wetu
BENKI ya Exim Tanzania imepanga kutumia mpaka sh. bil 36/- kila mwaka katika mpango wake wa mikopo ya nyumba za gharama nafuu kwa wateja wake na watanzania watakaoweza kukidhi vigezo katika maeneo yote nchini.
Benki ya Exim Tanzania mwezi Oktoba mwaka huu pamoja na benki nyingine sita nchini zilitia saini makubaliano ya kifedha ya ujenzi wa nyumba na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambayo yatasaidia wananchi kupata nyumba nzuri kupitia mpango huu wa kuwawezesha.
Akizungumza Dar es Salaam jana kuhusu huduma hiyo, Meneja Masoko na Mahusiano Linda Chiza alisema ukosefu wa mfumo mzuri wa fedha kwa kipindi kirefu umekuwa ukiwalazimisha watu kujijengea nyumba kupitia fedha wanazojitunzia wenyewe na kuwa inamchukua karibia miaka 10 kwa mtanzania wa kawaida kujenga nyumba kwa kutumia fedha anayohifadhi mwenyewe.
“Bidhaa tunayoizindua leo itasaidia kupunguza makali ya umiliki wa nyumba, bidhaa yetu ni ya pekee, ni ya gharama nafuu, ni rahisi na inayoendana na teknolojia ya kisasa na inatoa mianya mbalimbali kwa mteja,” alisema Chiza.
Alisema kuwa benki yake itakuwa katika nafasi ya kutoa kati ya sh. mil 30/- mpaka sh. mil. 350/- kwa wateja walio tayari kunua nyumba au kuzifanyia ukarabati watakapoweza kukidhi vigezo husika ambavyo ni pamoja na kuwa na hati ya mali isiyohamishika kama nyumba au shamba.
“Mkopo huu utatolewa ukiendana na riba ya kiushindani bila kuwa na gharama nyingine zilizojificha na tumeamua kutoa kipindi kirefu cha marejesho mpaka miezi 180 ili kuwapunguzia wateja mzigo nzito wa urejeshaji. Lengo letu kubwa ni kuwezesha matabaka tofauti ya watu nchini kuweza kumiliki nyumba bila kupata shida zaidi.
“Benki ya Exim katika jitihada za kuhakikisha inatoa mikopo ya muda mrefu imekuwa ni moja kati ya wadau wa kampuni ya Tanzania ya JMortgage Refinance (TMRC) kampuni mama Tanzania inayojihusisha na ujenzi wa makazi,” aliongeza.
Chiza aliongeza kuwa mbali na kuwa mbele katika utoaji wa huduma za kipekee za kibenki, benki yao pia imekuwa na mpango madhubuti wa kujitanua zaidi ili kuiwezesha benki kuwa na matawi mengi zaidi katika mikoa mingine ifikapo mwaka ujao.
“Tumekuwa benki ya kwanza nchini kuanzisha matawi nje ya nchi. Mpaka sasa tayari tuna matawi nchini Comoro na Djibouti. Sasa tuna mipango ya kufungua matawi mapya nchi nzima ili tuwe benki bora zaidi nchini,” alisema Chiza.
Benki ya Exim hivi karibuni iliinguia katika mfumo mpya na wa kisasa wa kujiendesha kutoka Kampuni ya M/S Polaris Software Labs Ltd, moja kati ya makampuni ya kibenki yanayoongoza katika utoaji wa huduma za teknolojia ya habari katika soko la dunia ambayo imeisadia benki kutoa huduma katika ubora na ufanisi.
Benki ya Exim ni benki ya sita kwa ukubwa Tanzania, ikiwa na matawi 21 nchi nzima pamoja na mashine za kutolea fedha (ATMs) 48 nchi nzima.
No comments:
Post a Comment