Tuesday, December 13, 2011

Waumini wawili wa Adventisti (wasabato)wafa katika ajali Arusha


Na Gladness Mushi wa Fullshangwe- Arusha WAUMINI wawili wa kanisa la waadventisti(wasabato) tawi la chuo kikuu cha Arusha,wamefariki dunia papo hapo na wengine 18 kujeruhiwa katika tukio la Ajali iliyotokea katika barabara kuu ya Arusha Moshi eneo la kwa mrefu nje kidogo ya jiji la Arusha.
Kwa mujibu wa kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Arusha,Akili Mpwapwa tukio hilo limetokea majira ya saa 2 usiku katika eneo la kwa mrefu,aliwataja marehemu hao kuwa ni Anna Mseli(30) mwanafunzi wa chuo kikuu cha Arusha na Priscas Makiluri mfanyakazi wa chuo kikuu cha Arusha.
Alisema kuwa marehemu hao walikuwa kwenye gari ngilisho, aina ya Toyota Hiace lenye namba T 372 AYO likiendeshwa na dereva aliyetambaulika kwa jina Novatus Focua(28) mkazi wa Sanawari ,ambapo gari hilo liligongana na basi aina ya Hino lenye namba T 939 BVL lililokuwa linaendeshwa na dereva aliyetambuliwa kwa jina moja la Ally ambaye hata hivyo alikimbia muda mfupi baada ya ajali hiyo .
Kamanda alisema chanzo cha tukio hilo ni dereva wa basi aina ya Hino kuingia ghafla barabarani bila kuchukua tahadhari wakati gari aina ya Hiace lililokuwa limewapakiwa waumini hao likitokea Arusha mjini kuelekea chuoni Usa River na kugongana na basi hilo.
Aliwataja majeruhi kuwa ni,Lomayani Memiri(24),Alice Mkongo(46),Novatus Focus(28),Fransis Peter (52) Grace Maiga(46),Miriamu Maiga(9),Hawa John(30) na Manael Mwashiga(36)ambaye ni mama mchungaji katika chuo hicho.
Wengine ni Roda Kaduma(52),Janeth Mwakalira(24),Gibson Meshack(25) Kondakta wa Hiace,Grady Arego(23)Monica Mbega,Chamlio Martin(33),Herena Burilo(47)Neema Nziku(33)mama mchungaji chuo kiku cha Arusha na Frank Meshack(58) wote wakazi wa jiji Arusha.
Alisema majeruhi wamelazwa katika hospitali ya mkoa Mount Meru na hali zao zinaendelea vizuri ,huku miili ya marehemu imehifadhiwa chumba cha maiti katika hospitali ya Mount Meru.
Aidha alisema kuwa polisi inaendelea kumsaka dereva wa basi aina ya Hino ambaye alikimbia muda mfupi baada ya kusababisha ajali hiyo

No comments:

Post a Comment