Friday, December 23, 2011

RAIS KIKWETE AKATISHA MAPUMZIKO KUWAJULIA HALI WALIOKUMBWA NA MAFURIKO DAR

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Sadick (katikati) na Meya wa Ilala, Jerry Silaa wakimuonesha Rais Kikwete eneo la Jangwani lililoathirika kwa mafuriko.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Alhamisi, Desemba 22, 2011, amekatisha mapumziko yake ya sikukuu kurejea Dar es Salaam kujionea mwenyewe madhara na uharibifu wa mafuriko pamoja na kutoa mkono wa pole kwa waliopoteza ndugu zao, kuumia ama kuharibiwa nyumba zao na mafuriko hayo.

Mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius K Nyerere akitokea kwenye Mbuga ya Wanyama ya Serengeti, mkoani Mara, ambako alikuwa anapumzika, Rais alilakiwa na mawaziri na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Said Mecky Sadiq.

Mheshimiwa Sadiq amemweleza Mheshimiwa Rais kuhusu hali halisi ya mafuriko katika Mkoa wa Dar es Salaam na madhara yake akisema kuwa mpaka sasa watu 20 wamethibitishwa kupoteza maisha na watu wengine 68, wakiwamo wakazi 66 wa Wilaya ya Ilala, wamejeruhiwa kutokana na mafuriko hayo.

Mkuu huyo wa Mkoa pia amemweleza Rais Kikwete kuwa watu 4,909 wamepatiwa hifadhi ya muda katika sehemu mbalimbali, hasa katika shule za msingi na sekondari, baada ya nyumba zao kuharibiwa katika mafuriko hayo yaliyotokana na mvua zilizoanza kunyesha tokea usiku wa kuamkia Jumatatu, Desemba 19, mwaka huu hadi jana.

Amemwambia Rais Kikwete kuwa kata zote 30 katika wilaya zote tatu za Mkoa wa Dar es Salaam zimeathiriwa na mafuriko hayo na kuwa wengi wa watu ambao nyumba zao zimeharibiwa na kubomolewa katika mafuriko hayo wamehifadhiwa na wanapatiwa huduma na Serikali.

Mara baada ya kupatiwa maelezo hayo, Rais Kikwete amepanda helikopta kukagua maeneo yote yaliyoathiriwa na mafuriko hayo hasa yale yaliyoko katika Bonde la Mto Msimbazi na baada ya ukaguzi huo alikwenda kuwapa mkono wa pole na kuwajulia hali wananchi waliopewa hifadhi katika Shule ya Msingi ya Mchikichini katika Wilaya ya Ilala.

Kuna kiasi cha watu 1,900 katika shule hiyo na akizungumza nao, Rais Kikwete amesema kuwa alikuwa amefika kuwapa pole kwa matatizo yaliyowafika. “Nimekuja kuwapeni pole na maafa yaliyowafika. Nimekuja kuwahakikisheni kuwa tupo, tuko nanyi na tutahakikisha kuwa mnapata huduma zote za msingi za chakula, za afya, za usafi kwa maana ya kila aliyeko hapa kupatiwa godoro, blanketi na chakula.”


Rais Kikwete pia ametumia nafasi hiyo kuwaagiza wote wanaohusika na mipango ya miji na usalama wa wananchi kuhakikisha kuwa wanatafuta na kupata majawabu ya kudumu ya watu kuathiriwa mara kwa mara na mafuriko kwa sababu ya kujenga na kuishi katika maeneo ya mabonde.

“Fanyeni uamuzi wa kutokujenga tena ama kutokurejea tena katika maeneo ya mabonde. Fanyeni uamuzi wa kutokuishi katika mazingira ya mashaka ya usalama wenu na wa familia zenu kila mvua inaponyesha. Hasara mnaijua zaidi nyie, hasara za kujenga upya, hasara za kusafisha tope, hasara za kununua samani mpya kila mvua inaponyesha,” Rais Kikwete amewaambia wananchi hao.

Rais amewaagiza maofisa wanaohusika kuwasaidia watu wanaoishi mabondeni kuhamia sehemu nyingine. “Napenda kuwahakikishieni kuwa tutawapatia maeneo ya kuishi nje ya mabonde na maofisa wote wanaohusika wako hapa wamenisikia.”

Rais Kikwete pia amesimama kwa muda kwenye Barabara ya Morogoro na kuwajulia hali walioathiriwa na mafuriko katika eneo hilo ambao wameweka makazi yao kwenye miti iliyoko barabarani hapo baada ya nyumba zao kuzingirwa na kuharibiwa na maji katika eneo hilo.


Kwa mujibu wa uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam eneo la ekari 200 na lenye uwezo wa kutoa viwanja 2,800 limeainishwa katika eneo la Mbopo, Wilaya ya Kinondoni, kwa ajili ya kutoa viwanja kwa walioathiriwa na mafuriko hayo baada ya wenye viwanja hivyo kulipwa fidia.

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,

Ikulu,

DAR ES SALAAM.

22 Desemba, 2011

No comments:

Post a Comment