Tuesday, April 24, 2012

YANGA YAOMBA RADHI MKUTANO MKUU


Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga ambaye pia mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF akiwakilisha klabu za Mkoa wa Dar es Salaam, Mohamed Bhinda aliwaomba radhi wajumbe wa Mkutano Mkuu kwa kitendo cha wachezaji wake kumpiga mwamuzi Israel Nkongo kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom dhidi ya Azam iliyochezwa Machi 10 mwaka huu.

Pia alimuomba Rais wa TFF, Leodegar Tenga kutoa msamaha wa adhabu ya kulipa faini iliyotolewa na Kamati ya Ligi ya TFF kwa wachezaji wawili wa Yanga ambao mpaka sasa hawajalipa faini hiyo.

Rais Tenga alimshukuru Bhinda kwa ujasiri alioonesha wa kuomba radhi mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kwa kitendo kile.

Aliongeza kuwa kwa vile yeye ni muumini wa kanuni, na adhabu hizo zimetolewa kwa mujibu wa kanuni hawezi kutoa msamaha, hivyo wachezaji hao walipe faini hizo.

Pia Rais Tenga alisema binafsi haziingilia kamati za TFF katika uamuzi ambao zinafanya kwa vile zina watu waadilifu, na angekuwa yeye binafsi ndiye anayetoa adhabu, angetoa adhabu kali zaidi kwa vile vitendo vya kupiga waamuzi havikubaliki katika mchezo wa mpira wa miguu.

No comments:

Post a Comment