Wednesday, April 4, 2012

YANGA YAPINGA ADHABU YA TFF KUWAPOKA POINTI ZAO

Uongozi wa Yanga umepinga hatua ya Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania(TFF)  kuipora   pointi tatu na mabao matatu kutokana na kitendo chake cha kumtumia, beki Nadir Haroub'Canavaro' wakati wa mechi ya ligi kuu dhidi ya Coastal Union.

Ofisa habari wa TFF, Boniface Wambura  alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa,Kamati ya Ligi kuu iliyokutana April 2 ilifikia uamuzi huo kwa kuzingatia kanuni ya 25 ya udhibiti wa wachezaji.

Alisema kuwa  kamati hiyo ilibaini kuwa Canavaro alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja kwa kumshambulia mwamuzi Israel Nkongo wakati wa mechi ya ligi kuu dhidi ya Azam iliyofanyika Machi 10,hivyo kwa kuzingatia kanuni ya 25,beki hiyo alipaswa kukosa mechi tatu.

Kutokana na uamuzi huo wa kamati ya ligi,Yanga  itaendelea kubakia katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi licha ya pointi zake kushuka mpaka 43 baada ya kushuka dimbani mara 21.

Simba ndio inaongoza ligi ikiwa na pointi 48 ikifuatiwa na Azam iliyojikita katika nafasin ya pili ikiwa na pointi 47.Katibu Mkuu wa Yanga,Selestine Mwesigwa alisema jana kuwa klabu yake imeshangazwa na uamuzi huo wa kamati ya ligi, na kudai kwamba  haukuwa halali  kwavile rufaa yao bado haijatolewa uamuzi na kamati ya nidhamu."Uamuzi wao unadhihirisha kwamba kamati ya ligi haina sifa za kushughulia masuala ya utovu wa nidhamu,ipo ipo tu haina  faida yoyote,"alisema Mwesigwa.   
Alisema kuwa wao walishakata rufaa kupinga adhabu ya vifungo kwa wachezaji wao,Jerryson Tegete,Stephano Mwasika, Omega Seme,Nurdin Bakar na Canavaro, lakini jambo lililowashangaza kamati ya ligi kuchukua uamuzi wao badala ya kusubiri ule wa kamati ya nidhamu

"Ukumbuke kwamba Yanga ilishakata rufaa baada ya kamati hiyo hiyo kuwafungia wachezaji wetu watano,Jerryson Tegete, Stephano Mwasika, Omega Seme, Nurdin Bakar na Canavaro."Tibaigan(Alfred,Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu na Maadali)akasimamisha adhabu kwa siku 14 na kuwaruhusu tuwatumie, leo wanatuhukumu kwa suala hilo hilo la Canavaro, hapo ni sawa?,"alisema Mwesigwa na kuongeza kuwa:

"Adhabu ya kadi nyekundu inayotolewa na mwamuzi ni kukosa kadi mbili hiyo ya tatu ni lazima iidhinishwe na kamati, sasa kama kamati ilitoa adhabu hiyo ambapo ilikuja kusimamishwa na kamati ya nidhamu uhalali upo wapi?,".

Aliongeza kwa kusema kilichowashangaza zaidi ni namna uamuzi huo ulivyotolewa wakati tayari Coastal Union walishakata rufaa ambayo badala ya kutolewa uamuzi na kamati ya nidhamu ama rufaa umetolewa na kamati ya ligi.

"Sisi tunasubiri barua rasmi baada ya hapo tutajua nini cha kufanya,Coastal walishakata rufaa ambayo kama ilifika TFF basi ni jana,sasa kazi ya kamati ya ligi ni kusikiliza rufaa na kutoa uamuzi?,".

Si sahihi kabisa je kamati ya nidhamu ikitoa uamuzi kwamba Canavaro hakumpiga mwamuzi nja na wao wametumia kigezo hicho itakuwaje,huku ni kuingilia uhuru  wa chombo kingine,"alisema Mwesigwa.

No comments:

Post a Comment