Monday, April 16, 2012

SUNZU - SIMBA TUTACHUKUA KOMBE LA SHIRIKISHO NA KUWEKA HISTORIA


Mshambuliaji wa Simba raia wa Zambia, Felix Sunzu amesema kuwa Simba itatwaa ubingwa wa ombe la Shirikisho la soka Afrika, CAF yeye anataka kiatu cha dhahabu cha mfungaji bora wa kombe hilo.

Sunzu alisema kuwa mbali na kutwaa Kombe la Caf, hana wasiwasi Simba itatwaa ubingwa wa Ligi Kuu na ufungaji bora na ndivyo vitakavyompa nafasi ya kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Zambia, Chipolopolo kinachowania kucheza Fainali za Kombe 2014.

Sunzu aliliambia Gazeti la Daily Mail la Zambia, kuwa ameshafunga mabao matano ya Kombe la Shirikisha na 13 ya ligi hivyo anatafuta nafasi zaidi kuitumikia timu ya taifa.

 “Nitafurahi sana kutwaa ubingwa wa Bara tena tutauchukua mikononi mwa wapinzani wetu (Young Africans) nina uhakika na pia nataka kuibuka mfungaji bora wa Kombe la Shirikisho,” Sunzu alisema.

Alisema kuwa kiwango chake kiko juu na ana imani kocha wa timu ya taifa ya Zambia, Herve Renard atamuita kwa ajili ya mechi za kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2014 na mechi za kuwania kucheza Fainali za Afrika 2013.

 “Kuna ushindani mkubwa kupata namba Chipolopolo, hasa baada ya kutwaa ubingwa wa Afrika, na hiyo ni sababu ya mimi kujituma, nataka kuitwa tena kwenye kikosi hiki,” alisema.

Sunzu mmoja wa wachezaji wanaocheza soka ya kuvutia, amekuwa akiwindwa pia na El Merreikh ya Sudan na Yanga na kusema kuwa pamoja na kuchezea Simba, amevutiwa na klabu nyingine na ndiyo maana wanataka kumchukua.

Simba wiki iliyopita, iliiondosha Entente Setif ya Algeria na sasa itakutana na  Al Ahly Shandy ya Sudan.

Setif, ilifungwa na Simba mabao 2-0 mchezo wa kwanza uliochezwa Dar es Salaam na ikashinda mabao 3-1 mjini Setif na Simba kufuzu kwa faida ya bao la ugenini.

Mara ya mwisho, Sunzu kuitumikia Chipolopolo ilikuwa katika michuano ya 2010 ya Kombe la Chalenji la Cecafa lililofanyika Tanzania na alifunga mabao matano na kuibuka mfungaji bora. Mchezaji huyo ni kaka mkubwa wa beki wa TP Mazembe na Chipolopolo, Stopilla.

No comments:

Post a Comment