Tuesday, August 16, 2011

KUONDOA MGAO WA UMEME TANZANIA

Mpango mzuri, Fikra pungufu kidogo
Zitto Kabwe
Taifa zima lilikuwa linasubiri siku ya tarehe 13 Agosti 2011 ili kufahamu ni jambo lipi jipya Waziri wa Nishati na Madini atakuja nalo kuhusu kumaliza tatizo la mgawo wa Umeme nchini. Tangu mwaka 2006, Tanzania imekuwa ikipata tatizo hili kwa wastani wa kila mwaka isipokuwa mwaka 2007 na 2008 kipindi ambacho Shirika la Umeme nchini TANESCO lilikuwa linanunua umeme kutoka mitambo ya Kampuni za Aggreko na Dowans. Mwaka 2009 adha ya mgawo ilikuwa kubwa sana, ikaendelea mwaka 2010 na baadaye mwaka 2011. Mamlaka ya Mapato nchini walikadiria kupoteza zaidi ya shilingi 840 bilioni kama kodi kutokana na mgawo wa mwaka 2011 peke yake. Hakuna hesabu zilizowekwa wazi kuhusu mgawo wa mwaka 2009 na ule wa mwaka 2010. Pia wachumi wa Tanzania hawajaweza kutueleza katika kila mgawo unaotokea nchini ni kwa kiwango gani ukuaji wa Pato la Taifa unaathirika. Kwa mfano, ukuaji wa sekta ndogo ya Umeme ukiporomoka kwa nukta moja, ukuaji wa uchumi unaathirika kwa kiwango gani. Taarifa kama hizi zinaweza kusaidia sana watunga sera kuweza kujua umuhimu wa sekta ndogo ya Umeme katika juhudi za kukuza uchumi na kuondoa umasikini nchini.
Mwaka 2011 ulianza kwa Kamati za Bunge za Nishati na Madini na ile ya Mashirika ya Umma kuweka kipaumbele katika uzalishaji wa Nishati ya Umeme. Kamati ya Mashirika ya Umma ilijikita katika kuhakikisha Uzalishaji wa Umeme wa uhakika kutoka katika vyanzo vya Makaa ya Mawe (Mchuchuma, Ngaka na Kiwira).
Kamati ya Nishati na Madini Ilijikita katika kuhakikisha Wizara inasimamia vya kutosha sekta ndogo ya Umeme na kumaliza kabisa tatizo la Mgawo wa Umeme katika muda wa mfupi, wa kati na mrefu. Kutofanikiwa kwa juhudi hizi na hasa kutoonekana kwa Bajeti ya kutosha ya Sekta hii kulifanya Bunge likatae kupitisha Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini.
Hatimaye Serikali ilileta Mpango wa Dharura ulioitwa Mkakati wa kuondoa Mgawo wa Umeme na kuimarisha Sekta ndogo ya Umeme. Mkakati huu ni wa miezi 16, kuanzia Agosti 2011 mpaka Disemba 2012. Mkakati huu utakagharimu jumla ya Shilingi 1.2trilioni. Fedha nyingi sana lakini kwa matumizi muhimu sana ya kulihami Taifa. Kimsingi hii ni ‘stimulus package’ kwa Sekta ya Umeme!
Mkakati huu utaingiza jumla ya 882MW za Umeme katika gridi ya Taifa ifikapo mwezi Disemba mwaka 2012. Katika hizi 572MW zitaingia katika Gridi mwezi Disemba 2011. Jumla ya 422MW zitatokana na Mashine za kuzalisha Umeme za kukodisha kutoka Kampuni mbalimbali binafsi (37MW Symbion, 80MW IPTL, 100MW Aggreco, 205MW Symbion II ). Mradi pekee ambao tunaweza kusema ni wa ndani ni ule wa 150MW ambao utamilikiwa na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Shirika la NSSF liliomba Serikalini kuingia katika uzalishaji wa Umeme toka mwaka 2010 kufuatia maelekezo ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma. Juhudi zake zilikuwa zinagonga mwamba kutoka kwa watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini kwa sababu ambazo hazijaelezwa waziwazi. Kwa hatua ya sasa iliyo kwenye Mkakati, Tanzania italipa Kampuni binafsi za nje zaidi ya Shilingi 523 Bilioni kutokana na kununua Umeme kutoka katika mitambo yao. Ingewezekana kabisa NSSF wangeombwa kuwekeza zaidi na hata kuwaomba Mashirika mengine kama PSPF kuwekeza na kupunguza kulipa fedha za kigeni kwa kampuni za nje.
Serikali itatoa dhamana (guarantee) kuiwezesha TANESCO kuchukua mkopo wa 408 bilioni tshs kutoka katika Mabenki ya ndani. Sekta Fedha nchini itabidi iandae ‘syndicated’ mkopo mwingine kwa TANESCO zaidi ya ule wa mwanzo wa mwaka 2007 wa tshs 300 bilioni ambazo ninaamini unalipwa bila ya mashaka. Hivi Serikali isingeweza kuuza Bond ya thamani hiyo? Wataalamu wa fedha wataweza kulijuza Taifa njia bora zaidi ya kupata fedha hizi. Hata hivyo Sekta ya Fedha ni moja ya sekta zitakazo faidi Mkakati huu, ikiwemo Sekta ndogo ya Mafuta (kwa kuuza mafuta ya kuendesha mitambo). Sekta ndogo ya Usafiri pia nayo itafaidika kwa kusafirisha mafuta kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda kwenye mikoa ambayo Mitambo ya kuzalisha umeme itawekwa kama Tanga, Dodoma, Mwanza na Arusha.
Ifikapo Mwezi Disemba 2012 Tanzania itakuwa imeongeza 310MW za Umeme ambazo zote zitakuwa zinamilikiwa na Shirika la Umeme au 150MW kati ya hizo Shirika la NSSF. Kwa maana hii ni kwamba katika jumla ya Uzalishaji wa Umeme wa 882MW  tunaotarajia kuongeza katika Gridi ya Taifa, utakaobakia nchini baada ya Mashine za kukodi kuondoka ni 460MW peke yake. Tutatumia  tshs 1.2tr kuingiza katika Gridi wa umeme wa kudumu wa 460MW tu. Hii inatokana na ukweli kwamba baada ya Disemba 2012 jumla ya 422MW zitakuwa zimeondoka kwenye Gridi baada ya mikataba ya kukodisha kumalizika.
Jambo moja zuri  ni kwamba Serikali imefikiri kimkakati kwamba tuwe hatuna mitambo ya kukodi ifikapo Disemba 2012 (kwa maana ya symbion na Aggreco). Huku ni kufikiri vizuri, kwamba Serikali itakuwa  imejenga uwezo wa Taifa kupitia TANESCO na NSSF kuwa na uwezo wa kuzalisha umeme wake. Imefanya ‘sequencing’ kwamba itatumia umeme wa kukodi wakati inajenga uwezo wa kununua mitambo yake yenyewe. Wakati Mikataba ya kukodi inakwisha, ndani ya miezi 16 Serikali kupitia TANESCO na NSSF itakuwa inazalisha 460MW. Hatua ya kupongeza.
Hata hivyo, Serikali na wananchi wanapaswa kujiuliza katika hiki kipindi cha mpito jambo gani litakuwa linafanyika? Ifikapo Disemba mwaka 2012 kutakuwa na mahitaji zaidi ya Umeme kwa ziada ya 200MW au zaidi. Hii inatokana na ukweli kwamba mahitaji ya umeme yaliyopo hivi sasa ni ‘suppressed’ licha ya ukuaji wa asilimia 15 kila mwaka. Vile vile inatarajiwa  kuwa kuwepo kwa umeme kutaongeza uzalishaji ambao utaongeza mahitaji zaidi. Hapa Serikali ilifikia ukomo wa kufikiri (ilichoka). Kunapaswa kuwa na kazi inayofanyika ambayo inafikiri zaidi ya 2012 (Thinking Beyond Dec 2012). Kunahitajika mradi wa angalau 200MW kuanza kutekelezwa kati ya sasa na Disemba 2012 ili mitambo ya kukodisha ikiondoka kuwepo na uwezo wa angalau 600MW. Hapa ndipo Mradi wa Kiwira I unaingia.
Mkakati wa Serikali kwa KIWIRA una makosa ya kifikra. Serikali inataka kukopa Uchina ili kujenga Kiwira. Mchakato wa mkopo utachukua zaidi ya miaka 2. Taifa haliwezi kusubiri. Serikali iharakishe utwaaji wa Hisa za Kampuni ya TanPower Resources na kukabidhi hisa hizo kwa Shirika la Umma. Shirika litangaze Zabuni kupata ‘strategic investor’ kwa utaratibu wa PPP ambao utazingatia kwamba mara baada ya Mwekezaji kujilipa gharama zake na faida kidogo umiliki uwe sawa kwa sawa (50/50).
Licha ya Mkakati kuendeshwa na zaidi na fedha za mikopo kutoka katika Mabenki, bado umepangwa vizuri mpaka 2012. Hata hivyo, Mkakati wa kuondoa mgawo wa Umeme na kuimarisha sekta ndogo ya Umeme nchini haukufikiriwa vya kutosha (inadequate thinking) na hasa kwa mbele ya 2012. Bado kuna fursa ya kuboresha. Kamati za Bunge za Nishati na Madini na Mashirika ya Umma zinapaswa kufuatilia kwa karibu sana utekelezaji wa Mkakati huu.
Written by zittokabwe
August 13, 2011 at 7:19 PM

No comments:

Post a Comment