Na:-Marzuku Khamis Maelezo Pemba
Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba Meja Mstaafu Juma Kassim Tindwa amesema kuwa Serikali haitosita kumchukulia hatua kiongozi yeyote atakayebainika kujihusisha na Magendo ya Karafuu.
Hayo ameeleza jana huko katika Ukumbi wa Kiwanda cha Makonyo Wawi Chake Chake Pemba katika Warsha ya Uhamasishaji wa Uchumaji na Uanikaji wa Karafuu pamoja na Uwekaji wa Amana iliowashirikisha Masheha,Watendaji Wakuu wa Mkoa na Wilaya wa Mkoa wa Kusini Pemba.
Amesema kuwa zao la Karafuu ndio Uchumi wa Taifa kwa hivyo Serikali haitokubali kuona zao hilo linauzwa visivyo halali kwa kutumia njia za Magendo.
Meja Tindwa amesema kuwa Vikosi vya Ulinzi na Usalama vimejipanga vizuri kulinda Usalama wa Raia na Mali zao ambapo amewashauri Wakulima wa zao hilo kutoweka Karafuu zao Majumbani na badala yake wazipeleke ZSTC kwa kuziuza mara baada ya kukauka.
Nae Naibu Meneja wa Fedha wa Shirika la ZSTC Ismail Omar amesema hadi kufikia sasa Shirika hilo limeshanunuwa Karafuu zaidi ya Tani Mia mbili na Arobaini zenye thamani ya zaidi ya shillingi Billioni Tatu.
Aidha amewataka Wakulima kuziweka Fedha wanazopata Benki ili kuweza kuhifadhi na kujiwekea Amana.
Warsha hiyo imeendeshwa na Shirika la ZSTC na Benki ya Watu wa Zanzibar kwa ajili ya kutoa muongozo mzuri kwa wauzaji na wazalishaji wa zao hilo la Karafuu.
No comments:
Post a Comment