Saturday, August 27, 2011

VODACOM MISS TANZANIA KUCHUANA KATIKA MICHEZO LEO

Warembo wanaowania taji la Vodacom Miss Tanzania 2011, leo wanatarajia kuchuana katika kuonyesha vipaji vyao katika michezo, kwenye ufukwe wa Jangwani Sea Breeze, Dar es Salaam.
Tukio hilo litakaloanza saa 3:00, ni miongoni mwa vipengele (fast tracks) vitano vya awali vya kinyang’anyiro hicho ambapo washindi hutinga moja kwa moja katika hatua ya nusu fainali.
Tayari warembo wawili wameshapata tiketi ya kuingia nusu fainali ya mashindano hayo ambao ni Mwajabu Juma aliyeshinda taji la Top Model na Tracy Sospeter aliyeshinda taji la Miss Photogenic.
Mbali ya vipengele hivyo, vingine vilivyobaki ni Kipaji (Talent) na Mvuto (Personality) ambapo mshindi wake hutangazwa kila wiki kabla ya fainali za taifa zilizopangwa kufanayika Septemba 10, mwaka huu katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Lino International Agency, waandaaji wa shindano hilo, Hashim Lundenga, michezo itakayohusishwa leo ni riadha, mbio za magunia, kuogelea, kuruka chini, mpira wa miguu, mpira wa pete, kuvuta kamba na mingineyo.
Shindano la Vodacom Miss Tanzania 2011, limedhaminiwa na Vodacom, Redd’s Original, New Habari (2006) Ltd, Star TV, Giraffe Hotel na Papa Zee Entertainment.

No comments:

Post a Comment