Wednesday, August 24, 2011

MBUNGE WA SINGIDA MJINI DEWJI ATOA UFAFANUZI JUU YA TUHUMA DHIDI YAKE


Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini, Mohammed Dewji, ametoa ufafanuzi juu ya tuhuma zilizotolewa na baadhi ya wakazi wa Singida za kwamba hajafanya chochote cha maendeleo katika jimbo lake tangu kuchaguliwa kwake .

Tuhuma na malalamiko hayo yaliyotolewa na baadhi ya wananchi wa Singida kupitia mtandao wa kijamii wa FACEBOOK, wakati wa kubadilishana mawazo na Mbunge huyo.

Wananchi hao ambao waliruhusiwa kutoa maoni na dukuduku zao kwa mheshimiwa DEWJI walidai kutoona maendeleo yoyote katika jimbo hilo kwa madai kwamba wananchi wa SINGIDA wamekuwa wakiteseka na maisha kwa kukosa maji, ajira na masuala ya maendeleo.

Katika ufafanuzi wake kuhusiana na Malalamiko hayo, Mheshimiwa Dewji amesema, Tangu kuchaguliwa kwake amekuwa mstari wa mbele katika kuleta mabadiliko ya kimaendeleo katika maeneo ya Kero za Maji ambapo amefanikisha uchimbaji wa  visima virefu zaidi ya 21, kwenye kata za Unyambwa, Mungu Maji, Unyamikumbi, Mwankoko, Mtamaa, Mandewa na Mtipa pamoja na baadhi ya kata za Mjini Kama Kindai, Mitunduruni na Utemini.

Aidha Mheshimiwa Dewji pia ameongeza kuwa  bado anaendelea na jitihada za kukabiliana na tatizo hilo kwa  kuibana Serikali itekeleze mradi Mkubwa wa Benki ya Dunia wa kuchimba visima 10 jimboni na anaendelea kuibana Serikali ifanye haraka kumalizia mradi mkubwa mwingine wa maji unaofadhiliwa na Benki ya BADEA na OPEC .

“Mradi huo ukikamilika ndio utakuwa ufumbuzi wa tatizo la maji katika manispaa ya Singida. Mradi huu utabadilisha miundombinu yote ya Maji safi ndani ya manispa yetu. Mradi huu unatarajia kukamilika 2013 na utagharimu takriban billion 20”.Amesema Mheshimiwa Mbunge Dewji.

Kuhusu ajira DEWJI ameeleza kuwa amekuwa mstari wa mbele katika kutoa  Ajira kwa vijana kupitia kampuni yake ya Mohamed Enterprises Limited(MeTL) sambamba na makampuni mengine mbalimbali.

Amefafanua  zaidi kuwa yuko mbioni kuwekeza katika jimbo lake kwa kufungua kiwanda  kitakachotoa fursa zaidi kwa vijana na wakazi wa Singida kujipatia maendeleo na ajira, na kwamba kwasasa  anaendelea kuwasiliana na wataalamu mbalimbali wa uwekezaji ili kuona kama kuna fursa za kuweza kuwekeza katika manispaa ya hiyo.

Amepongeza kupokelewa kwa wito wa kuhamasisha michezo katika Jimbo lake na kusisitiza kuwa ataendelea kunyanyua na kuibua vipaji  kupitia mashindano yake yajulikanayo kama Mohammed Dewji Cup yakiwa na takribani miaka SABA  na yamekuwa na mafanikio makubwa  kwa vijana wazaliwa wa Singida.

 “Kuhusiana na Suala la Ujenzi wa Uwanja wa Namfua nilishaanza ukarabati katika  eneo la Jukwaa kuu wewe mwenyewe ni shahidi kama ulikuwa unaufahamu uwanja ulivyokuwa mwanzo na wakati wa mashindano ya riadha Kitaifa niliweza kukarabati eneo la kukimbilia wanariadha  na bado nitaendelea kukarabati kwa awamu mpaka tutakapoukamilisha. Ukumbuke ahadi hii haikuwa yangu peke yangu. Ila nimeshanunua nyasi za bandia ambazo zimenigharimu million 250. Natarajia kuziweka hizo nyasi 2012/13.”

No comments:

Post a Comment