Shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na masuala ya afya, utafiti na kijamii la AMREF limetumia sh bilioni 7 katika kupunguza makali ya uhaba wa maji safi na salama katika vijiji 77 vilivyo kwenye mradi wa Maji, Afya na Usafi wa Mazingira wilayani Mkuranga.
Kaimu Meneja wa mradi huo, Bw. Saltiel Kimaro, amesema kuwa mradi huo uliotekelezwa kwa ushirikiano kati ya AMREF na Halmashauri ya wilaya ya Mkuranga umefanikiwa kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama kutoka asilimia 22 hadi kufikia asilimia 74 katika eneo la mradi ambapo kiwilaya umechangia ongezeko la upatikanaji wa maji hayo kwa asilimia 13.
Katika mkutano huo uliofanyika mwishoni mwa wiki katika hoteli ya Vigwaza huko Mkuranga, Bw. Kimaro, amesema kuwa Mradi huo wa miaka mitano uliofadhiliwa na Jumuiya za Nchi za Ulaya (EU) na washirika wengine wa AMREF kutoka Italia na Uingereza ulianza Septemba 2006 na kufanikiwa pia kupunguza magonjwa yasababishwayo na maji yasiyo safi na salama.
Akifungua mkutano wa kukabidhi mradi huo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga kufuatia kufikia kwa ukomo wa mradi huo, Mkuu wa wilaya hiyo Bw. Henry Clemens alisema kuwa pamoja na AMREF kufanikiwa kuchimba visima virefu 53, vifupi 152 na kujenga mabirika 71 ya maji ya mvua, bado asilimia 47 ya wananchi wake hawajafikiwa na huduma hii.
Bw. Clemens alisema kuwa kutokana na hali hiyo anashawishika kuiomba AMREF kufikiria na kuanzisha mradi mwingine wa miaka mitano ili kuongeza idadi ya watu wanaopata maji safi na salama bila kuyafuata maeneo ya mbali.
Mkuu huyo aliipongeza AMREF kwa ujenzi wa miundo mbinu vikiwemo vyoo vya mfano 68 na kuwapa mafunzo wananchi kupitia vikundi mbalimbali zikiwemo kamati za maji, afya, maendeleo za kata, vikundi vya sanaa, watumiaji maji, waelimishaji jamii, vilabu vya afya shuleni, mafundi wa vijiji, kamati tendaji ya wilaya, madiwani, timu ya usimamizi wa shughuli za maji na usafi wa mazingira.
“Pamoja na ukweli kwamba mradi ulianzishwa na AMREF, unabaki kuwa mali ya wananchi wa Mkuranga. Sisi ndio tunaofaidika nao. Kwa mantiki hii, ni wajibu wetu sisi wana Mkuranga kukaa na kufikiria hatma ya mradi huu uliotuletea mema pale AMREF watakapokuwa wameondoka,” alishauri Mkuu huyo.
Aidha alielezea kusikitishwa kwake na ripoti ya uchunguzi wa maendeleo ya mradi wa awamu ya kwanza wa mwaka 2001 – 2005 baada ya AMREF kuutekeleza kwa mafanikio na kuondoka na Halmashauri kuahidi kuuendeleza. “Inaonyesha mafanikio ya mradi yamepungua kwa kukosa ufuatiliaji,” alibainisha.
Mkuu wa wilaya alionya kwamba uzembe wa jinsi hii usiifanye wilaya irudi ilikotoka, “Katika enzi zile za kukosa maji safi na salama na kushambuliwa na magonjwa ya mlipuko,” alionya Mkuu wa wilaya.
Awali, Meneja Rasilimali Watu wa AMREF aliwataka wana Mkuranga kufahamu kwamba miradi hiyo ni mali yao hivyo wanawajibika kuitunza ili nayo iwatunze. Aidha aliwatoa hofu wana mkuranga kuhusu kufikia ukomo wa mradi huo kwa kusema kuwa pamoja na AMREF kukabidhi miradi hiyo kwa Halmashauri, itaendelea kuwa wilayani humo kwa mwaka mmoja likimalizia kazi ambayo haijakamilika.
Nao wajumbe wa mkutano huo wa makabidhiano kwa kauli moja waliazimia kuiomba AMREF ibaki Mkuranga na kuanzisha mradi mwingine ili kuweza kumaliza kabisa tatizo la uhaba wa maji safi na salama.
No comments:
Post a Comment