Friday, October 14, 2011

MBUNGE MANGUNGU AWASHA MOTO KWA JAN POULSEN

MBUNGE wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu (CCM), amemtaka Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Sunday Kayuni, kuangalia upya mwenendo mbaya wa soka, hasa ufanyaji kazi wa kocha wa timu ya Taifa, Mdenmark, Jan Borge Poulsen.
Stars imezidi kupata matokeo mabaya yaliyopelekea kuondolewa kwenye mbio za kuwania kufuzu Kombe la Mataifa, baada ya kupigwa mabao 3-1 na morocco, mechi ambayo Poulsen alitabiria kufungwa kabla ya kusafiri, kuelekea nchini humo.

Kwa siku kadhaa sasa, TFF imekuwa kwenye presha kubwa kutokana na wadau mbalimbali wa michezo kuhoji mwenendo huo mbaya, licha ya Katibu Mkuu wake, Angetile Osiah, mara kwa mara kuonekana kumbeba mgongoni kocha huyo kwa kumtetea na kutetea pia utendaji kazi wa Shirikisho lake.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka mkoani Morogoro, Mangungu alisema ni wakati wa TFF, ikiwa chini ya Kayuni kuzionea huruma pesa za Watanzania kwa kulipa mshara usiokuwa na manufaa na Taifa.
Alisema Kayuni ndio jukumu lake la kuangalia ufundi unavyokwenda katika Shirikisho hilo, kwa kufuta ajira ya kocha huyo aliyeshindwa kabisa kulitetea soka la Tanzania, licha ya kuwa na ramani nzuri katika uwepo wa Marcio Maximo, kocha wa zamani wa timu hiyo.
“Suluhisho ni kutafutwa kocha mwingine baada ya huyu kuonekana kama ni mzigo kwa Tanzania na anayetumia gharama kubwa bila mafanikio yoyote kupatikana na kuhuzunisha wadau wa michezo.


“Pesa zetu zinakwenda sehemu isiyostahili, hivyo ni jukumu la Kayuni kuangalia namna ya utendaji kazi wao, ukizingatia kuwa hata yeye ana uwezo mkubwa kuliko huyo mwajiriwa wake, ndio maana mambo yamekuwa mabaya,” alisema.


Kwa mujibu wa Mangungu, tayari Poulsen ameshavunja mkataba wake na Stars baada ya kushindwa kuipatia mafanikio timu hiyo, licha ya kuingia makubaliano ya kuifundisha Stars kwa mafanikio katika ujio wake.


Wakati Tanzania ni tofauti kidogo, nchi za wengine kocha anaposhindwa kuipatia mafanikio timu yake huondoka mwenyewe kabla ya kuondoshwa, kitu kinachotakiwa kuwaingia vilivyo wadau, mashabiki na viongozi wa soka nchini.

No comments:

Post a Comment