Sunday, October 16, 2011

Miss Tanzania 2011, Njia panda watoa msaada wodi maalum ya watoto Muhimbili

Miss Tanzania 2011,Salha Esrael akimtazama mtoto wa kike ambaye ameamua"kumuadapti" na kumpachika jina lake la Salha.
********************* 
Miss Tanzania 2011 Salha Esrael wakishirikiana na kipindi cha Njia Panda jioni ya leo wametoa msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo pampas,sabuni za maji,mashuka na vinginevyo ambavyo ni vitu muhimu kwa watoto wenye umri chini ya mwezi mmoja katika hospitali ya Taifa Muhimbili kwenye Wodi ya Watoto namba 36 (Neonatal Ward).
Mlimbwende huyo,Salha kwa hivi sasa ameamua kujikita kwenye harakati za kutetea haki za watoto wachanga walio chini ya umri wa mwezi mmoja ambao kitaalamu wanaitwa Neonates, "watoto hawa wamekuwa wakisahauliwa kwa kiasi kikubwa,watu wanawakumbuka kuwasaidia watoto kuanzia miaka mitano na kuendelea,wanakimbilia kutoa vyandalua na mambo mengine,lakini ukweli ni kwamba kundi la watoto hawa limesahaulika mno,kwa hiyo kupitia Miss Tanzania 2011 tukishirikiana na kipindi cha Njia Panda tumetoa msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo pampas,sabuni za maji,mashuka na vinginevyo ambavyo ni vitu muhimu kwa watoto hawa ambao wamekuwa wakisahaulika siku hadi siku",alisema Salha. 
Aidha Miss Tanzania 2011 Salha Esrael “amemuadapti” mtoto ambaye ni yatima mwenye umri wa chini ya mwezi mmoja na kumpa jina la Salha,mtoto huyo ambaye kwa sasa anaonekana kuendelea vyema kiafya alikutwa ametupwa vichakani na kuokotwa na wasamaria wema ambao walimfikisha haraka kwenye hospitali ya Taifa ya Muhimbili,wodi ya watoto namba 36 (Neonatal Ward).
Salha amebainisha wazi kuwa atahakikisha anamlea mtoto huyo katika maisha yake yote.  
Akizungumza kwenye hafla hiyo fupi ya kuvikabidhi vifaa hivyo mapema leo jioni kwa manesi wa wodi hiyo,Salha alisema kuwa yeye atajikita zaidi katika kutetea haki za watoto hao wachanga ambao wamekuwa wakisahaulika kwa asilimia kubwa,ilhali watoto wengi wanaanzia kwenye hatua hiyo, “huu ni mwanzo tu wa kampeni hii,lakini nitakaporudi kwenye mashindano ya Miss Word yanayotarajiwa kufanyika hapo baadaye mwaka huu,mimi pamoja na wadau wengine tutahakikisha tunafanya kampeni kubwa ya kuihamasisha na kuielimisha jamii katika suala zima la kuwasaidia watoto hawa,ambao baadhi yao hutelekezwa na wazazi wao kutokana na kuwa na matatizo mbalimbali wangali wachanga,” alisema  Salha.

No comments:

Post a Comment