Thursday, October 13, 2011

WACHEZAJI YANGA WALETA MGOMO KUTOKANA NA UKATA KLABUNI



Hali mbaya ya ukata ndani ya klabu bingwa ya Tanzania na Afrika Mashariki na kati, jana asubuhi ilisababisha mgomo wa wachezaji wa klabu hiyo wakitaka kugomea mazoezi huku wakishinikiza kulipwa mishahara yao kuanzia Septemba na kutafutiwa kambi sehemu nyingine, kwani klabuni kuna matatizo ya huduma ya maji.
Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema kwamba wachezaji hao waliamua kuendesha mgomo huo baada ya kupigwa danadana za mara kwa mara na viongozi wa klabu hiyo, kuhusiana na mustakabali mzima juu ya ulipwaji wa mishahara yao.
Habari hizo zilibainisha kuwa, kutokana na hali hiyo, uongozi wa Yanga ilibidi ukae kikao na wachezaji hao ili kufikia muafaka kuhusiana na mustakabali mzima wa mgomo huo, ambapo jioni walianza kulipwa huku mafundi pia wakijipanga kutatua tatizo hilo la miundombinu ya maji.
Alipotafutwa msemaji wa Yanga, Louis Sendeu, kuzungumzia kitendo hicho, alisema kuwa: “Hizo ni propaganda tu ambazo ni za kupuuzwa, si kweli leo wachezaji asubuhi hawakufanya mazoezi kwa sababu uwanja wetu ulijaa maji, lakini jioni walifanya mazoezi kama kawaida kabla ya kuingia kambini.”
Kuhusiana na kikao baina yao na wachezaji, Sendeu alisema kuwa kilikuwa cha kawaida katika kupeana mikakati ya kuelekea katika mechi ya kesho na michezo mingine iliyobaki.

No comments:

Post a Comment