Tuesday, October 11, 2011

TAARIFA YA IKULU KWA UMMA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewataka watendaji wa Serikali yake kutambua kuwa nchi iko katika hali ya dharura kubwa ya upatikanaji wa nishati ya umeme, na hivyo wafanye maamuzi ya haraka, bila kigugumizi, kukabiliana na hali hiyo kwa manufaa ya wananchi.

“Tuko katika hali ya dharura na mimi sioni hisia za uharaka wa kuchukua maamuzi na hatua nyingine muhimu za kukabiliana na udharura wa upatikanaji wa umeme na nyenzo nyingi za kuzalisha umeme. Hatuwezi kuendeleza kuwa na kigugumizi katika kuchukua maamuzi ya kuitoa nchi katika changamoto kubwa hizi za upatikanaji wa nishati,” Rais Kikwete amewaambia watendaji hao wa Serikali yake wanaohusiana na sekta ya nishati.

“Ubwana mkubwa wa kila mmoja wetu utatambuliwa kutokana na mafanikio ambayo kila mmojawetu ataonyesha katika kuchangia katika kukabiliana na hali hii ya upatikanaji wa nishati,” amesema Rais Kikwete katika kikao cha watendaji hao kilichofanyika Ikulu, Dar es Salaam, jana, Jumatatu, Oktoba 10, 2011.

Rais Kikwete alikuwa anazungumza katika kikao alichokiitisha kuzungumzia ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam na upatikanaji wa gesi asilimia nchini kwa ajili ya kuzalisha umeme ambao umekuwa katika mgawo nchini tokea Novemba mwaka jana kutokana na ukame ulioathiri kina cha maji katika mabwawa yote ya kuzalisha umeme nchini.

Hali hiyo, imeilazimisha nchi kuchukua hatua nyingi za  kupatikana kwa umeme wa dharura mbali na hatua ambazo tayari Serikali ya Rais Kikwete ilikuwa imeanza kuchukua kuongeza kasi ya upatikanaji wa umeme kutokana na vyanzo vingine mbali na maji.

Miongoni mwa waliohudhuria kikao hicho cha kazi ni pamoja na Waziri wa Fedha Mustafa Mkullo, Waziri wa Sheria na Katiba Mheshimiwa Celina Kombani, Katibu Mkuu Kiongozi Phillemoni Luhanjo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Frederick Werema, na maofisa kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Benki Kuu ya Tanzania, Tume ya Mipango, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Kikao hicho kimejadili, miongoni mwa mambo mengine, ujenzi wa bomba kubwa zaidi la kusafirisha gesi asilia kutoka Mikoa ya Mtwara na Lindi kwenda Dar es salaam linalokusudiwa kujengwa na Serikali kwa fedha nyingi ili kuongeza kasi ya upatikanaji gesi kwa ajili ya matumizi ya kuzalishaji umeme na matumizi ya viwandani katika sehemu mbalimbali za nchi badala ya bomba la sasa ambalo ni dogo zaidi.

Shabaha na mipango ya Serikali ni kuhakikisha kuwa bomba hilo linakuwa limekamilika katika muda wa mwaka mmoja ujao tayari kuongeza uwezo wa Serikali kuwapatia wananchi umeme wa uhakika zaidi na kuongeza uzalishaji wa viwanda ambavyo vimeanza kutumia gesi kwa ajili ya uzalishaji badala ya mafuta.



Kikao hicho pia kimejadili upatikanaji wa gesi yenyewe na hatua zinazochukuliwa ili kuhakikisha kuwa inapatikana gesi zaidi ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka kila siku katika uzalishaji wa umeme na mahitaji ya viwandani.

Katika mjadala wa upatikanaji wa gesi zaidi, kikao hicho kimeangalia jinsi gani Tanzania inavyoweza kuongeza uzalishaji wa gesi hiyo kwa kuchimba visima zaidi na kukarabati visima vilivyoko kwa sasa ili kuongeza upatikanaji wa gesi hiyo asilia.

Kikao hicho pia kimejulishwa juu ya hali ya umeme nchini na jitihada zinachukuliwa na vyombo na taasisi mbalimbali nchini na hasa TANESCO katika kuitoa nchi katika hali ya sasa ya mgao wa umeme ambao umekuwa unaendelea kwa karibu mwaka mmoja.

Katika kikao hicho, Rais Kikwete amewataka watendaji hao kuelekeza nguvu zao katika kutambua na kufanya kazi kwa karibu zaidi na wawekezeji ambao wamethibitisha kuwa makini zaidi katika uzalishaji umeme kwa sababu inawezekana kuwa Serikali  isiwe na uwezo wa kutosha wa kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha za kutosha katika uzalishaji umeme katika miaka mitano ijayo ili kwenda sambamba na mahitaji makubwa na yanayoongezeka ya umeme nchini.

Mapema kabla ya hapo, Rais Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Ujerumani katika Tanzania, Mheshimiwa Klauu-Peter Brandes.

Katika mkutano huo ambao nao umefanyika Ikulu, Dar es Salaam, Rais Kikwete na Mheshimiwa Balozi Brandes wamezungumzia hali nzuri ya uhusiano kati ya Tanzania na Ujerumani.



Balozi wa Ujerumani amemshukuru Rais Kikwete na Serikali yake kwa kuandaa safari ya karibuni ya mabalozi wanaowakilisha nchi zao katika Tanzania kutembelea kijiji cha Butiama ikiwa sehemu ya kumbukumbu ya miaka 12 iliyopita.   

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

10 Oktoba, 2011

No comments:

Post a Comment