Monday, November 7, 2011

CANNAVARO: SUNZU KANIONDOA STARS...... KAPOMBE ARITHI NAFASI YAKE



Beki wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Nadir Haroub 'Cannavaro' amesema kuwa mechi dhidi ya mahasimu wao Simba ambayo walishinda 1-0 ndiyo iliyomtoa kwenye timu ya taifa kutokana na majeraha ya kuvimba enka.
Akizungumza jana, Cannavaro, alisema kuwa aliumia wakati akiwania mpira dhidi ya mshambuliaji wa Simba, Mzambia Felix Sunzu, na si kweli kwamba aliumia wakati wa mazoezi ya timu ya taifa, Taifa Stars inayojiandaa na mechi dhidi ya Chad ya kuwania kufuzu kwa Kombe la Dunia 2014.
Alisema kwamba kilichotokea juzi akiwa kwenye kikosi cha Stars ni kutonesha jeraha hilo ambalo litamweka nje ya uwanja kwa zaidi ya wiki moja.
"Sunzu ndiye aliyenipa maumivu haya, Stars nimejitonesha tu, mwanzo wa kuumia ilikuwa ni mechi yetu na Simba," alisema beki huyo tegemeo katika ngome ya Stars na klabu yake ya Yanga.
Maumivu hayo ya Cannavaro yamemfanya aondolewe Stars na pia hataweza kuambatana na timu yake ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes, ambayo inatarajia kuelekea Misri leo kwa ajili ya kujiandaa na mashindano ya Kombe la Chalenji yatakayofanyika kuanzia Novemba 25 jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, kocha mkuu wa Taifa Stars, Jan Poulsen, hajaita beki mwingine kwa ajili ya kuziba pengo la Cannavaro na badala yake huenda akamtumia mchezaji 'kiraka' Shomary Kapombe wa Simba katika nafasi hiyo.

No comments:

Post a Comment