Monday, November 7, 2011

KOCHA TIMBE AONDOKA BONGO



Hatimaye aliyekuwa Kocha Mkuu wa mabingwa wa soka Tanzania Bara, Sam Timbe, ametimka jana jijini Dar es Salaam kuelekea nchini Uganda, baada ya kulipwa stahiki zake alizokuwa akiudai uongozi wa klabu hiyo baada kusitisha naye mkataba wa kuinoa timu hiyo.
Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu, alisema jana kuwa tayari wameshamlipa stahiki zake Timbe ambaye alisitishiwa ghafla mkataba na uongozi wa klabu hiyo hivi karibuni na kumrejesha kocha wake wa zamani Mserbia Kostadin Papic.
“Tumeshamalizana na Timbe kwa kumlipa kilicho chake na ameondoka jana kwenda kwao tayari kwa masuala yake binafsi,” alisema Sendeu.
Kabla ya kuondoka, juzi Timbe alikaririwa kwenye vyombo vya habari akiapa kutoondoka mpaka atakapolipwa fedha zake baada ya kuona akizungushwa kulipwa malipo yake ambayo ni mishahara ya miezi saba na fidia ya kuvunja naye mkataba, ambao ulikuwa unatarajiwa kumalizika Mei mwakani.
Hata hivyo, Sendeu hakuwa tayari kuweka wazi kiasi alicholipwa kocha huyo kwa madai kuwa ni siri baina ya uongozi na kocha huyo mwenye rekodi ya mafanikio ya kufundisha soka katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Chanzo cha habari cha kuaminika kutoka ndani ya uongozi wa mabingwa hao wa TZ Bara na Afrika mashariki na kati kimesema kuwa, Timbe amelipwa shilingi milioni 36 ambazo zimejumuisha mishahara yake na fidia ya kuvunjiwa mkataba wake.

No comments:

Post a Comment