Monday, November 21, 2011

WATOTO 43,000 WANAOISHI MAZINGIRA HATARISHI WAFIKIWA NA WAMA,FHI



Na Anna Nkinda – Maelezo

Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) kwa kushirikiana na Family Health International (FHI) Pamoja Tuwalee wameweza kuwafikia watoto zaidi ya elfu arobaini na tatu wanaoishi katika mazingira hatarishi katika mikoa ya Dar es Salaam , Pwani, Morogoro na Zanzibar.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Mkurugenzi wa Mradi wa FHI Pamoja Tuwalee Priskila Gobba wakati akiongea na wawakilishi wa Sekta binafsi katika mkutano uliojadili jinsi ya kuwasaidia watoto hao uliofanyika katika viwanja vya WAMA jijini Dar es Salaam.

Gobba alisema kuwa mchakato wa kuwafikia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi ulianza mwaka jana mwishoni na kwa kipindi cha mwaka mmoja wameweza kuzitambua familia zao na mahali wanapoishi na hivyo kuanza kutoa huduma mbalimbali.

“Baada ya kuwafikia watoto wote hao, watoto 25,198 wameweza kupata huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwapatia ushauri nasaha ili waweze kujitambua kuwa wao ni watoto wa jamii na wanatakiwa kupata huduma muhimu kama watoto wengine, wameweza kupata vyeti vya kuzaliwa na huduma ya afya”, alisema Gobba.

Aliendelea kusema kuwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi wako wengi mjini na vijijini hivyo basi jamii nzima inatakiwa kuwasaidia watoto hawa jambo wanalolifanya hivi sasa ni kushirikiana na mashirika mengine ili waweze kufahamu sababu zinazowafanya wakimbie majumbani kwao ili waweze kutatua tatizo hilo lisiweze kutokea tena kwa vizazi vijavyo.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Taasisi ya WAMA Daud Nasibu alisema kuwa wameamua kuishirikisha Sekta binafsi katika mradi huo kwani huwa wanafanya kazi ya kuwalea watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi pia kutokana na shughuli wanazozifanya wanaifikia jamii iliyopo vijijini kirahisi zaidi.

Nasibu alisema kuwa wataandaa mkakati wa mawasiliano kuhusiana na mradi huo ambao utawezesha kuishirikisha jamii nzima ndani ya wilaya na vijijini ili jamii hiyo iweze kuwatambua na kuwaangalia watoto yatima wanaoishi katika maeneo yanayowazunguka.

“Jamii ya watanzania imejaliwa kuwa na moyo wa upendo na kujitolea lakini inahitaji kusisitizwa na kuhimizwa ili iweze kuona umuhimu wa kuwasaidia watoto hawa.

Kama kila Mtanzania ataweza kumsaidia mtoto yatima mmoja, kila mtoto ataweza kupata huduma na kwa miaka ijayo hakutakuwa na mtoto anayeishi katika mazingira hatarishi, hakutakuwa na mtoto atakayeshindwa kwenda shule kwa kukosa ada na vifaa, hakuna mtoto atakayelala na njaa kwa kukosa chakula”, alisema Nasibu.

Aidha alisema kuwa mradi huo unalenga kuwafikia watoto wengi na kuwapatia mahitaji yao kwa kutumia jamii , watoto hawataishi katika vituo vya kulelea watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi bali jamii inayowazunguka itaweza kuwasaidia watoto hawa huku wakiwa katika mikono ya wazazi na walezi wao.

Akizungumza kwa niaba ya wawakilishi kutoa Sekta Binafsi Richard Kasesela Mwenyekiti wa Shirikisho la Sekta Binafsi (Biashara) Afrika alisema kuwa makampuni mengi yanatoa msaada kwa watoto yatima kwani Sekta binafsi iko kila mahali hivyo ni rahisi kwao kuwafikisha watoto ukilinganisha na sekta zingine.

Kasesela alisema, “Kutokana na shughuli zinazofanywa na Sekta binafsi kuwepo hadi vijijini tumekuwa tukitoa misaada mbalimbali kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi walioko mijini na vijijini ukilinganisha na Sekta zingine hivyo basi tukiunganisha nguvu zetu kwa pamoja tunaweza kuwafikia watoto wengi zaidi na kwa haraka”.

Aliendelea kusema kuwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi wakiendelea kuwepo wanaweza kuleta janga kubwa hapo baadaye kwani kuna kipindi jamii iliacha kuwaangalia watoto ndiyo maana wameongezeka kwa kasi huku wengi wakiwa wamekosa malezi na misaada.

FHI Pamoja Tuwalee ni mradi wa miaka mitano unafadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia ofisi ya shirika lao la Maendeleo hapa nchini (USAID Mission/Tanzania) mradi huo unafanya kazi kazi katika mikoa ya Dar es Salaam wilaya tatu, Pwani wilaya sita, Morogoro wilaya sita na Zanzibar wilaya 10.

No comments:

Post a Comment