Monday, November 7, 2011

DERRICK WALULYA KURUDI SIMBA, KUZIBA PENGO LA JERRY SANTO



SIMBA SPORTS CLUB
P.O.BOX 15318 | TEL+255 222183330 |FAX +255 222183330 |MSIMBAZI/MCHIKICHI STREET | DAR ES SALAAM | TANZANIA | EMAIL simbasportsclub@yahoo.com|
WEBSITE www.simba.co.tz| AFFILIATED TO TFF, DRFA and IDFA
07/11/2011
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Ndugu Wanahabari
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Kamati ya Utendaji ya Simba Sports Club ilikutana kujadili masuala anuai ya klabu na yafuatayo ni maazimio yaliyofikiwa mara baada ya mkutano huo.
Kuhusu Jerry Santo
Klabu ilikubaliana na ombi la mchezaji wake Jerry Santo aliyeomba aruhusiwe kwenda barani Asia kucheza soka la kulipwa mara baada ya kumalizika kwa mkataba wake wa sasa na Simba mwezi huu.
Simba inamtakia heri na fanaka mchezaji huyo kwenye maisha yake ya kisoka.
Nafasi ya Santo itajazwa na mchezaji kutoka nchini Uganda, Derick Walulya, ambaye kwa sasa anaichezea klabu ya Mamlaka ya Mapato Uganda (URA).
Moses Basena
Kamati ya Utendaji haikumjadili Moses Basena wala kuchukua maamuzi yoyote kumhusu. Hii inatokana na ukweli kwamba Simba SC ni klabu ya kistaarabu na inafahamu kuwa kocha wake huyo yuko kwenye msiba mzito wa mama yake mzazi.
Klabu ya Simba inapenda kutumia nafasi hii kukanusha habari zote kuhusu kusimamishwa au kufukuzwa kazi kwa Basena katika kipindi hiki kigumu kwake.
Wachezaji wa Timu ya Vijana ya Simba
Kama inavyofahamika, Simba imesajili wachezaji 26 kwa ajili ya Ligi Kuu ya Vodacom msimu huu ingawa Kanuni za TFF zinaruhusu timu kusajili wachezaji wasiozidi 30.
Kamati ya Utendaji imeamua kuwa nafasi nne zilizobaki (ili kufikia 30) zitajazwa na wachezaji kutoka timu za vijana za Simba.
Majina ya wachezaji hao yatapatikana baada ya Kamati ya Ufundi na Benchi la Ufundi kukutana na kujadiliana kuhusu wachezaji watakaofaa kwa ajili hiyo.
Simba ni timu ambayo falsafa yake ya soka inafahamika. Wachezaji ambao wamepikwa ndani ya timu (kama hao wa timu za vijana) wanafundishwa kwenye falsafa hiyo na wanatarajiwa kuwa mabalozi wazuri wa falsafa ya klabu.
Klabu maarufu na zenye mafanikio duniani kama vile Barcelona na Man United zimefanikiwa sana kwa kukuza vipaji kutoka kwenye timu zake za vijana.
Simba inaelekea kwenye njia hiyo.
Vurugu Viwanjani
Kamati ya Utendaji ya Simba imesikitishwa sana na vitendo vya vurugu vilivyofanywa na baadhi ya washabiki wake wakati wa mchezo wa mwisho wa raundi ya kwanza ya Ligi Kuu dhidi ya Moro United.
Washabiki hao wachache walikuwa wakitoa lugha ya matusi, vitisho na vurugu dhidi ya wachezaji na viongozi wa Simba waliokuwapo uwanjani.
Kamati iliazimia kuwa wakati umefika sasa kwa vyombo vya dola kushughulikia washabiki wanaofanya vitendo visivyo vya kiungwana katika viwanja vya soka nchini.
Kwa taarifa hii, Simba inawaomba washabiki wake waendelee kuwa alama ya uungwana na ustaarabu michezoni. Washabiki wa Simba wanafahamika kote duniani kwa sifa hii.
Simba SC haitatetea mpenzi au mwanachama wake yeyote atakayekutwa na hatia ya kufanya vitendo vya vurugu uwanjani.
Kufungwa na Yanga
Wajumbe wa Kamati ya Utendaji walieleza kusikitishwa kwao na kufungwa na Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu msimu huu.
Kamati inafahamu machungu ambayo wapenzi na wanachama wa Simba waliyapata baada ya kipigo hicho.
Hata hivyo, Kamati inasisisitiza kuwa ni vema wapenzi wa Simba wakaanza kuitazama ligi kwa mapana yake. Ligi haipo kwa ajili ya Simba kuifunga Yanga pekee bali kutwaa ubingwa wa Tanzania na kuwakilisha Taifa katika michuano ya kimataifa.
Pamoja na kufungwa na Yanga, Simba inaongoza ligi si kwa kuwa na pointi nyingi pekee bali pia kwa kuwa na idadi kubwa ya magoli ya kufunga na wastani mzuri wa magoli ya kufunga na kufungwa.
Hii ni ishara kuwa Simba ni timu bora Tanzania kwa sasa kwa vigezo vyovyote vile vya kimpira.
Kitendo cha washabiki kutuhumiana, kugombana na kutaka kufanya fujo kwa sababu ya kupoteza mechi moja na kusahau mazuri yote ambayo yamefanywa na timu ni kinyume cha uanamichezo.
Timu kubwa kama Man United ya England zimefungwa hadi mabao sita katika mechi ya watani wa jadi lakini hakuna aliyefanya fujo kwa wachezaji, benchi la ufundi au viongozi wa timu hiyo.
Kamati imehimiza umoja na mshikamano miongoni mwa wana Simba ndani na nje ya nchi. Hakuna sababu ya kuibua migogoro na migongano isiyo na sababu kwa sababu ya timu kupoteza mechi moja.
Naomba kuwasilisha
Ezekiel Kamwaga
Msemaji
Simba Sports Club

No comments:

Post a Comment