Thursday, November 24, 2011

Matukio mbalimbali ya ajali na mafuriko Monduli

WATU wawili wamekufa na wengine watatu kunusurika baada ya lori walilokuwa wakisafiria kusombwa na maji katika daraja la Mto Loobuko kati ya Makuyuni na Mto wa Mbu wilayani Monduli.

Ajali hiyo ilitokea jana saa 12 alfajiri wakati lori hilo namba T190 AKW likiwa limebeba mitambo ya kutengeneza barabara likitoka Engaruka kwenda Arusha, kukumbwa na dhahama hiyo.


Maafa hayo yametokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika milima ya Monduli.


Mfanyakazi wa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR), Augustino Masige, akiendesha gari namba T573 AHW, akitoka Arusha kwenda Musoma ni miongoni mwa watu walionusurika katika maafa hayo baada ya gari lake aina ya Toyota kusombwa na maji eneo hilo.


Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Jowika Kasunga, aliwataja watu waliokufa kuwa ni dereva wa lori hilo aliyetambuliwa kwa jina moja tu la Shekman (38) na msaidizi wa mitambo ya kutengeza barabara, Samwel Julius (28).


Kasunga alisema watu hao walisombwa na maji umbali wa kilometa moja huku msaidizi wa opareta wa mitambo, alikutwa amenasa kwenye miti huku amekufa.


Dereva alikutwa amekufa umbali wa kilometa moja baada ya kugunduliwa na wanafunzi wa shule za msingi waliokuwa wakirejea nyumbani kutoka shuleni.


Aidha, Mkuu wa Wilaya aliwataja walionusurika katika ajali hiyo, kuwa ni Somara Minja (28), Basil Joseph (27) na William Martin (27) Mwili wa Julius umehifadhiwa katika chumba cha maiti cha Hospitali ya Wilaya ya Karatu, wakati wa Shekman umehifadhiwa katika chumba cha maiti katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru.


Akihojiwa eneo la tukio, mfanyakazi wa ICTR, Masige, alisema katika gari hilo alikuwa peke yake na alikuwa safarini kwenda kwao Musoma likizo na alipofika eneo hilo saa 11 alfajiri gari lake lilisombwa na maji.


Alisema hata hivyo jitihada za kulinasua gari hilo katika tope zinaendelea na kazi ikikamilika atarejea Arusha.


Aidha, abiria zaidi ya 45 waliokuwa wakisafiri na basi la Lakrome aina ya Fuso namba T946 ARX likitoka Rombo kwenda Karatu ni miongoni mwa walionusurika katika eneo hilo.


“Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika milima ya Monduli na Simingoli zimesababisha kingo za madaraja matano kati ya Mto wa Mbu na Makuyuni kukatika, ambapo daraja lililosababisha maafa limekatika nusu,” alisema Kasunga akiwa eneo la tukio Makuyuni jana.


Kutokana na tukio hilo, abiria zaidi ya 250 na magari 40 yakiwamo ya watalii wanaokwenda katika hifadhi za Serengeti, Ngorongoro na Manyara, walikwama kwa zaidi ya saa sita katika eneo hilo.


Kasunga akiwa na wajumbe wa kamati yake, alisema mvua hizo zilianza kunyesha kwa nguvu kati ya Novemba 17, 18, 23 na 24 na kusababisha madaraja matano likiwamo moja kubwa kuathirika.


Alisema hatua za haraka zisipochukuliwa, hali ya utalii na usafiri kwenda katika hifadhi za Kanda ya Kaskazini mwa Arusha na abiria wanaosafiri kwenda mikoa ya Mara, Mwanza na Shinyanga itakuwa ngumu.


Sylvia Kombe anaripoti kutoka Mwanga, kwamba Anna Keshi (20) na mwanawe Ester Shukuru mwenye umri wa miezi minane, wamekufa baada ya kuangukiwa na gema usiku wakiwa wamelala kutokana na mvua nyingi zilizonyesha usiku.


Akithibitisha ajali hiyo jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Absalom Mwakyoma alisema tukio hilo lilitokea juzi usiku katika kijiji cha Mamba, Ugweno.


Mwakyoma alisema siku ya tukio, mvua kubwa zilinyesha katika kijiji hicho na kusababisha maporomoko ya udongo kutoka mlimani na kuangukia ukuta wa nyumba walimokuwa wamelala na kufunikwa na udongo.


Alisema uchunguzi wa miili ya marehemu hao wote wawili umefanyika na kukabidhiwa kwa ndugu zao kwa ajili ya mazishi.


Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Athumani Mdoe akisoma taarifa ya maafa hayo kwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, alisema mvua kubwa zilizonyesha usiku wa kuamkia Novemba 23, zikiambatana na radi, zilisababisha maafa katika maeneo ya ukanda wa milimani na tambarare ambapo upande wa Mashariki zilisababisha vifo, kubomoka kwa nyumba na kukatika kwa mawasiliano ya barabara.


Mdoe alisema katika kijiji cha Lambo, kata ya Shigatini, nyumba mbili ziliangukiwa na gema na kubomoa kuta na katika kijiji cha Mamba, nyumba nne ziliangukiwa na gema na moja ni ya Issa Mruma iliyosababisha kifo cha Anna na Esther.


Alisema katika Tarafa ya Usangi Kata ya Kighare, nyumba 30 ziliangukiwa na gema na kubomoka kuta na nyingine 15 zilifunikwa na udongo na kwamba katika upande wa mawasiliano barabara ya Usangi -Mwanga na kusababisha kusimama kwa huduma za usafiri wa abiria na mizigo.
Basi la abiria la Mali ya kampuni ya Lakrome aina ya Fuso namba T946 ARX likiwa na abiria zaidi ya 40 likitoka Karatu kwenda Rombo nalo ni miongoni mwa mwa vyombo vya usafiri vilivyonusurika katika ajali.
Mfanyakazi wa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR), Augustino Masige, aliyekuwa akiendesha gari namba T573 AHW, akitoka Arusha kwenda Musoma, akisimama kando ya gari lake lilosukumwa na maji umbali wa mita 50 toka barabarani.
Mwili wa marehemu Samweli Julius ambaye alikuwa ni msaidizi wa mitambo ya kutengeza barabara, ukiwa umenasa juu ya mti.
.
Lori la mizigo namba T190 AKW likiwa limebeba mitambo ya kutengeneza barabara likitoka Engaruka kwenda Arusha.
 
 Polisi walifika eneo la tukio na kufanya ugaguzi wa matukio hayo ya ajali.
 Polisi wakatoa idhini sasa ya mwili wa Samweli kutolewa katika eneo ulipopatikana.
 Njia hii ikafungwa nusu kuepusha maafa kutokea baada ya kipande cha barabara hiyo kumegwa na maji katika daraja la Mto Loobuko.
 Hivi ndivyo kipande hicho cha barabara kilivyomegeka na maji.
 Ukarabati wa haraka unahitajika katika eneo hili kabla ya mawasiliano kukatika.
 Wakazi wa eneo la Loobuko wakiangalia athari hizo za mvua.
Hakika maafa yatokeapo hukumba kila kiumbe hai katika jamii. Mbwa huyu si kuwa aliathirika na mafuriko hayo bali alionesha uzalendo wake wa kweli na kufika katika eneo la tukio na kuangalia mwenyewe kilichojiri

No comments:

Post a Comment