Monday, November 21, 2011

HOTUBA YA RAIS KIKWETE KWA WAZEE WA DAR ES SALAAM,NOVEMBA 18,2011

HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE,
KWA WANANCHI KUHUSU HALI YA UCHUMI NCHINI NA MCHAKATO WA KATIBA MPYA, TAREHE 18 NOVEMBA, 2011

Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa,
Mstahiki Meya,
Viongozi wa Serikali,
Wazee wangu,
Ndugu Wananchi,

Nakushukuru Mkuu wa Mkoa na viongozi wenzako wa Jiji la Dar es Salaam kwa kuniandalia fursa hii ya kukutana na Wazee wa Dar es Salaam.  Nawashukuru sana wazee wangu kwa kuitikia wito wangu huu wa kukutana nanyi.  Nimefarijika sana kwa mahudhurio yenu makubwa pamoja na taarifa kuwa ya muda mfupi.
          Nimewaiteni wazee wangu nizungumze nanyi na kupitia kwenu nizungumze na wananchi wote wa Tanzania.  Mwisho wa mwezi uliopita sikuweza kufanya hivyo kupitia utaratibu wetu wa kawaida kwa sababu nilikuwa kwenye Mkutano wa Jumuiya ya Madola nchini Australia.  Mwisho wa Mwezi  huu nitakuwa Bujumbura kuhudhuria  Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, hivyo sitaweza kuongea na wananchi wakati huo. Lakini, yapo masuala kadhaa ambayo ni muhimu watu kupata ufafanuzi kutoka kwangu.  Kwa ajili hiyo nimeona nitumie fursa hii kuzungumza nanyi siku ya leo.   Leo nataka kuzungumzia hali ya uchumi na mchakato wa kupata Katiba Mpya.
Hali ya Uchumi
Ndugu Wananchi;
          Katika kuelezea hali uchumi nchini, naomba nianze kwa kuelezea hali ya uchumi duniani kwani yanayotokea nchini yana uhusiano mkubwa na yanayotokea duniani.  Hali ya uchumi duniani siyo shwari.  Ukweli ni kwamba hali katika uchumi wa mataifa ya Marekani, Ulaya Magharibi na Japan haijatengemaa kufuatia machafuko ya masoko ya fedha na mdororo wa uchumi wa miaka miwili iliyopita.  Hivi sasa uchumi wa mataifa tajiri ya Ulaya , wanachama wa Umoja wa Ulaya na hasa wanachama wa Umoja wa Sarafu ya Euro unapita katika kipindi kigumu na mashaka.  Thamani ya sarafu hiyo inashuka na hata kuaminika kwake ni kwa mashaka. Mfumuko wa bei umepanda, ukosefu wa ajira umeongezeka na ipo hofu kubwa ya uchumi wa nchi hizo kudorora tena.  Lakini nchi hizi ndiyo masoko makubwa ya bidhaa zetu, watalii na bidhaa za viwandani.  Hivyo, athari zao zinatugusa na sisi.  Kuongezeka kwa mfumuko wa bei kunaongeza bei ya bidhaa tunazonunua kutoka kwao.  Aidha, kutetereka kwa uchumi wao nako kumepunguza masoko ya bidhaa zetu.
          Lakini kulegalega kwa sarafu ya Euro kumesaidia kuimarika kwa sarafu ya dola ambayo kabla ya hapo ilikuwa imepungua nguvu.  Kwa sababu hiyo thamani ya sarafu ya dola imepanda duniani ikilinganishwa karibu na sarafu nyingine zote pamoja na yetu.  Wakati huo huo bei ya mafuta imeendelea kupanda duniani kutoka dola 76.1 kwa pipa Septemba,, 2010 hadi dola 100.5 Septemba, 2011.  Jumla ya yote haya ni kuongezeka kwa mfumuko wa bei kutoka asilimia 4.2 Oktoba, 2010 hadi asilimia 17.9 Oktoba, 2011.
Ndugu Wananchi;
Serikali na vyombo husika vimekuwa vinachukua hatua mbalimbali kukabiliana na matatizo ya kushuka kwa thamani ya shilingi, bei ya mafuta, bei ya sukari na matatizo ya umeme.  Kuhusu kushuka kwa thamani ya shilingi Benki Kuu imeendelea kuchukua hatua zilizopo ndani ya mamlaka yake hususan kubana ulanguzi wa fedha za kigeni, kudhibiti matumizi ya fedha kigeni kufanyia malipo hapa nchini na kuongeza fedha za kigeni katika masoko ya fedha.  Kwa kweli uwezo wao una ukomo.  Jawabu la uhakika lipo kwenye uchumi wa mataifa makubwa kuchukua hatua thabiti kuimarisha uchumi wao ili thamani ya dola irejee mahali pake stahiki na bidhaa zetu zipate masoko ya uhakika na bei nzuri ili mapato yetu ya fedha za kigeni yaongezeke.
Kwa upande wa mfumuko wa bei, ni vyema tukatambua kuwa Asilimia 75 ya ongezeko hili imetokana na kupanda kwa bei ya chakula na mafuta.   Asilimia 25 iliyobaki imechangiwa na sera za fedha.  Kwa upande wa mafuta, tunaamini utaratibu wa kuagiza mafuta kwa pamoja utasaidia kudhibiti bei za ndani za bidhaa hiyo.  Aidha, itsaidia kupunguza makali ya athari ya bei za dunia zinazopanda.  Kwa upande wa bei za vyakula, tatizo kubwa ni uhaba wa chakula katika nchi jirani unaosababisha wote kututegema sisi na hivyo kupandisha bei nchini.  Tunaendelea kudhibiti magendo ya chakula na wakati huo kutengeneza taratibu rasmi za kuziuzia chakula nchi jirani.
Kwa upande wa sukari tumeamua kuruhusu tani 120,000 ziagizwe ili kupunguza uhaba wa bidhaa hiyo na kushusha bei yake.

No comments:

Post a Comment