Wednesday, November 30, 2011

TAARIFA YA IKULU KUHUSU SALAMU ZA UHURU WA TANZANIA BARA


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Marekani Mheshimiwa Barak Obama ametuma salamu za pongezi na za kuitakia baraka Tanzania wakati inapoadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Tanzania Bara inatimiza miaka 50 ya Uhuru Ijumaa ya wiki ijayo, Desemba 9, 2011.

Aidha, Rais Obama ameihakikishia Tanzania kuwa Marekani itaendelea kubakia rafiki na mshirika wa kuaminika katika jitihada za kuhakikisha kuwa Watanzania kujiletea maisha bora na kwa njia za amani.

Katika salamu zake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais huyo wa Marekani ametumia lugha ya Kiswahili kuitakia baraka Tanzania akimwandikia Mheshimiwa Kikwete, “Mungu awabariki” na kufuatiwa na tafsiri ya maneno hayo hayo katika lugha ya Kiingereza.

Katika salamu zake, Rais Obama ameongeza kuwa umbali mkubwa wa kijiografia kati ya Tanzania unazidi kupungua kwa sababu ya uhusiano wa karibu kati ya Wamarekani na Watanzania.

Amesisitiza Rais Obama, “Hali ya kuwa anuwai ya taifa lako, kama ilivyo ya kwetu, ni chimbuko na msingi wa nguvu zitakazoipitisha Tanzania katika mabadiliko mengi na changamoto nyingi zinazokabili nchi yenye demokrasia inayopanuka.”

Imetolewa na:

Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

30 Novemba, 2001

No comments:

Post a Comment