Wednesday, November 16, 2011

Tanzania yapiga hatua katika upimaji wa ardhi

 Waziri wa Ardhi, Myumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka.
 Na Anna Nkinda – Maelezo.
Tanzania ni nchi ya kwanza Barani Afrika kwa kuwa na mtambo  mpya wa alama za upimaji wa ardhi ambapo jumla ya alama mia saba na arobaini  zimesimikwa nchi nzima kati ya hizo sita zinapima moja kwa moja kwa kutumia satellite.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na  Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani kutoka wizara ya Ardhi, Nyumba  na Maendeleo ya Makazi Dk. Selassie  Mayunga wakati   akiongea na mwandishi wa habari hizi kuhusiana na maandalizi ya mkutano wa kimataifa wa upimaji ardhi na ramani utakaofanyika mwishoni mwa wiki hii jijini Dar es Salaam.
Dk. Mayunga alisema kuwa Mtu akipima ardhi kwa kutumia alama sita ambazo ni za kisasa anapima kwa urahisi na haraka zaidi na zitarahisisha shughuli ya upimaji wa ardhi nchini  pia  zitapunguza gharama kwa kiasi kikubwa. Tayari mradi huo umeshakamilika na utazindiliwa tarehe 13/6/2012.
“Karibu Nchi zote za Afrika hazina  alama hivi za upimaji  hivi sasa Nchi za Uganda na Ghana zimeanza kuweka alama katika ardhi yao, sisi kama wizara mama inayoshughulika na masuala ya ardhi tutahakikisha kuwa  alama hizi zinafanya kazi vizuri.
 “Hivi sasa wizara yetu  ina mpango wa miaka mitano wa upimaji ardhi nchi nzima. Tutahakikisha  kuwa kila kipande cha ardhi kinachomilikiwa na mtu kinapimwa kwa njia ya kisasa na katika kutekeleza hili Serikali imekubali kuanzisha kituo cha kupokea picha kwa njia ya Satelite kitakachojengwa mjini Dodoma katika mwaka huu wa fedha wa 2011/12”, alisema Dk. Mayunga.
Aliendelea kusema kuwa kituo hicho kitasaidia kila kipande cha ardhi kupimwa na kujulikana mahali kilipo pamoja na mmiliki wake. Picha zitakazopingwa kwa kutumia satellite zitaonyesha kila kitu kilichopo juu ya ardhi kama ni uvuvi, elimu, madini na hivyo kurahisisha ukusanyaji wa kodi  ambazo zitasaidia kuendeleza sekta mbalimbali za maendeleo ya nchi.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa wameshafanya majaribio ya mradi huo katika wilaya ya Babati mkoani Manyara na Bariadi mkoani Shinyanga ambako mashamba zaidi ya laki moja yamepimwa na wamiliki wamepewa  hati za umiliki za kimila ambazo wanaweza kuzitumia  kukopa fedha Benki.
Alimalizia kwa kuwataka wananchi kulipia ardhi wanayoimiliki kila mwaka mwezi wa saba unapofika kwani   ni lazima kwa kila mtanzania kulipia ada ya viwanja bila kukumbushwa na kutolipa au kuendeleza ardhi uliyopewa na Serikali  kutakufanya unyang’anywe na radhi hiyo na  atapewa mtu mwingine ambaye atakiendeleza.
Serikali imepima jumla ya viwanja laki nane na sabini na mbili elfu na kuvimilikisha  kwa wananchi na Taasisi mbalimbali  tangu kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika mwaka 1961.

No comments:

Post a Comment