TANZANIA imekataa masharti ya Uingereza inayotaka nchi zinazotaka misaada yake ziruhusu vitendo vya ushoga. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe alitoa msimamo huo jana Jijini Dar es Salaam akisema huko ni kwenda kinyume na sheria na utamaduni wa nchi yetu inayotambua ndoa ya mme na mke kama kiini cha familia. Membe alisema hayo alipokuwa akizungumzia mkutano wa Jumuia ya Madola uliofanyika wiki iliyopita Perth, Australia. Alitoa msimamo huo kufuatia kauli ya Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron kuwa wana mpango wa kusitisha misaada kwa nchi ambazo katiba na sheria zake hazitambui mashoga na ndoa zao.
"Nchi yetu inaheshimu sheria na utamaduni wake hivyo hatupo tayari nchi nyingine kutuwekea masharti kama hayo ya kuwa na uhusiano wa jinsi moja, hili ni tamko hatarishi linaloweza kuvunja uhusiano na nje", Waziri Membe aliwaambia waandishi wa habari. Alisema tamko hilo ni msimamo wa chama cha Conservative na kibaya zaidi linatoka Uingereza ambako ndio wenye Jumuia ya Madola hivyo linaweza kusababisha kuvunjika kwake na Cameroun na nchi hiyo ndio watawajibika jumuia hiyo ikivunjika.
Alisema miongoni mwa nchi 54 za Jumuia ya Madola kati yake nchi 13 ushoga ni sehemu ya katiba yao wakati 41 hazina utamaduni huo hivyo msimamo wa Tanzania ni kuwa na ndoa za jinsi mbili tofauti, kinyume na hapo unafungwa kifungo miaka 30. Alisema kuendelea kukumbatia ushoga si jambo zuri na si la kulishabikia hata kidogo vinginevyo wanaweza kujuta nchi ikijihusisha na ushoga na kuukubali kupata misaada ya maendeleo.
"Tanzania hatuwezi kuyumbishwa kwa masharti ya kipuuzi bora tuitunze nchi yetu. Tanzania ni nchi maskini lakini kamwe haturuhusu kuingiliwa na nchi nyingine. Kama ndio hivyo basi wakae na hela zao," alisema Waziri Membe wizarani kwake.
No comments:
Post a Comment