Tuesday, August 19, 2014

APR,POLISI ZAFUZU NUSU FAINALI KOMBE LA KAGAME,AZAM FC,EL MERREIKH KIBARUANI LEO

 

Na Baraka Mpenja
HATUA ya Robo fainali ya michuano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na kati, Kombe la Kagame, imeanza kutimua vumbi alasiri ya jana na jioni mjini Kigali, Rwanda ambapo timu ya Polisi na APR (zote za Rwanda) zimetinga nusu fainali.
Robo fainali ya kwanza ilianza majira ya 9:00 alasiri kwa kuwakutanisha Wanyarwanda Polisi na dhidi ya Warundi, Atletico na kushuhudia dakika 90 zikimalizika kwa suluhu ya bila kufungana.
Sheria ya mikwaju ya penalti ikabidi itumike kuamua mshindi ambapo Polisi waliibuka na ushindi wa penalti 9 kwa 8.
Katika mchezo huo wachezaji wote 22 walipiga penalti, lakini Polisi ndio walikuwa na bahati zaidi.
Robo fainali ya pili ilipigwa jioni kwa kuzikutanisha timu mbili pinzani nchini Rwanda baina ya Rayon Sport na APR.
Dakika 90 za mechi hiyo zilimalizika kwa sare ya mabao 2-2 na APR wakashinda kwa penalti 4 kwa 3.
Katika mchezo huo zilipigwa penati 5 kwa kila timu tofauti na mechi ya mapema.
Kwa matokeo ya mechi za leo, nusu fainali ya kwanza itakuwa baina ya Polisi na APR.
Robo fainali nyingine zitapigwa leo ambapo mabingwa wa Tanzania Bara, Azam fc maarufu kama Wana Lambalamba watashuka dimbani kukabiliana na El Merreikh ya Sudan.
Kutokana na historia nzuri ya El Merreikh katika soka la Afrika mashariki na kati, hakika Azam wamekwaa kisiki ambacho wanahitaji maarifa makubwa kukivuka.

Mechi nyingine ya kesho jumatano itawakutanisha KCC ya Uganda dhidi ya Altabara ya Sudan Kusini.

No comments:

Post a Comment