Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Imechapishwa Agosti 8, 2014, saa 2:16 asubuhi
BAADA ya kutolewa kushiriki michuano ya klabu bingwa Afrika mashariki na kati maarufu kwa jina la kombe la Kagame, Yanga sc imesema maisha mengine yanatakiwa kuendelea kama kawaida.
Katibu mkuu wa Yanga, Beno Njovu alisema wamesikitishwa kutolewa Kombe la Kagame, lakini hali hiyo haiwafanyi washindwe kuendelea na mipango mingine ya kuiandaa timu kwa ajili ya michuano iliyopo mbele yao.
Njovu alisema wachezaji waliotakiwa kwenda Kagame wanaendelea na mazoezi kama kawaida na wale waliokuwa timu za taifa za nchi mbalimbali (Tanzani, Rwanda na Uganda) walipewa mapumziko na wataripoti kesho jumamosi kwenye mazoezi ya timu yanayoendelea uwanja wa shule ya sekondari Loyola, Mabibo, jijini Dar es salaam.
“Maisha yanatakiwa kuendelea kama kawaida. Wale wachezaji waliotakiwa kwenda Kagame, mnaona wanaendelea na mazoezi kama kawaida na wale waliokuwa timu ya taifa wamepewa mapumziko mpaka jumamosi.” Alisema Njovu.
“Jumamosi wachezaji watafanya mazoezi. Wachezaji wote waliokuwa na timu za taifa watakuwepo, halafu watakuwa na kikao na mwalimu kupanga mikakati ya michuano iliyopo mbele yetu”
“Michuano iliyopo mbele yetu ilikuwa Kagame, lakini kwasababu tumetolewa, sasa michuano iliyopo mbele yetu ni ligi kuu, wataanza kupanga mikakati mara moja na kuingia kambini”
Baraza la vyama vya soka ukanda wa Afrika mashariki na kati CECAFA iliwatoa Yanga kushiriki kombe la Kagame baada ya kukataa kutuma kikosi cha kwanza.
Awali Yanga ilituma kikosi cha pili cha wachezaji 20, lakini CECAFA ikakitaa na kuitaka klabu hiyo kuthibitisha kutuma kikosi cha kwanza, lakini wanajangwani hawakufanya hivyo na wakatupwa nje ya michuano.
Baada ya tukio hilo, CECAFA waliwasiliana na TFF na kulitaka Shikirikisho hilo kuchagua timu nyingine na zali likawaangua Azam fc.
No comments:
Post a Comment