Tuesday, August 19, 2014

BUTIKU:KINACHOFANYIKA BUNGE KATIBA NI UTOTO

         Posted by Nasra Abdallah    

MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku

MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, amesema kitendo kinachoendelea sasa hivi katika Bunge la Katiba ni cha kitoto kutokana na ukweli kwamba katiba haiwezi kupatikana kwa kupitishwa vifungu na kundi la upande mmoja.
Butiku ambaye alikuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam, katika uzinduzi wa filamu na wimbo ya ‘Katiba ni yetu’, iliyoandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa kushirikiana  na wasanii mbalimbali.
Butiku alisema kuwa Watanzania kwa muda mrefu wamekuwa wakihitaji katiba mpya na sio viraka ambavyo anaamini ndicho kinachofanywa sasa na Bunge hilo ambalo kupitia Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisema watafanya marekebisho ya baadhi ya vifungu vya katiba ya sasa kwa ajili ya kutumika katika uchaguzi mkuu mwakani, iwapo wajumbe wakundi la UKAWA hawatakubali kurejea bungeni.
Alisema hatua hiyo haoni kama itazaa matunda, ikizingatiwa kwamba katiba ni maridhiano, hivyo kitendo cha pande moja kuendelea kupitia rasimu ya katiba ni kupoteza muda na kufuja fedha za wananchi.
Alilitaka Bunge hilo kuelewa kwamba katiba sio yao bali ni ya wananchi na ndio maana Rais alivyokubali kufanyika kwa mchakato huo aliunda Tume ambayo ilitumika kukusanya maoni ya wananchi ili kila mmoja aweze kushirika vilivyo katika kutoa dukuduku lake ya kipi angependa kiingizwe au kiondolewe.
“Lakini jambo la kushangaza leo tunaona mchakato huo umetekwa na kundi la watu fulani tena hawa si wenginebali ni wanachama wenzangu wa CCM na kujiona kuwa wao ndio wana haki ya kuamua kila kitu katika rasimu tuliwapelekea ambayo ni maoni ya wananchi.
“Wananchi tunaomba muelewe kwamba tulichokiandika ndicho mlichokisema na kama kuna uongo wowote tumeuweka basi tunaomba mtuhukumu kwa hilo kwa kuwa tulichokifanya ni kuweka mapendekezo yenu na wataalamu takribani 190 tulipewa kwa ajili ya kazi ya kuandika,”alisema.
Kuhusu mvutano wa Serikali mbili au tatu, Butiku alisema wao kama wazee hawako tayari kuona serikali mbili ikiundwa na wanaoendelea kuwaita wachochezi katika hilo waendelee kuwaita na kuahidi kutetea hilo hadi kufa huku akiwataka wale wenye kupendekeza hivyo wafanye wao wenyewe na wasihusishwe kamwe.
Hata hivyo, Butiku aliwataka wananchi kutoogopa vitisho vya mtu yoyote yule katika mchakato huu kutokana  na madaraka yake aliyonayo ndani ya serikali kwani katiba ni ya wote na kila mtu anapaswa kuhusika kuitengeneza.
Kwamba, majadiliano mbalimbali yanyoendelea kwa sasa kuhusu pande mbili zinazovutana bungeni, haoni kama kuna haja hiyo na kudai kuwa ni kupoteza muda kwa kuwa kila kitu kipo wazi.
Akizungumzia kuhusu filamu hiyo, Butiku alisema kilichochezwa na wasanii hao ndio maisha halisi ya Watanzania waliojionea wakati wanazunguka nchi nzima katika kukusanya maoni.
Kuhusu wimbo huo ambao ulionekena kumvutia, Butiku alisema mashairi yaliyotumika ya ‘Katiba ni yetu, Taifa ni Letu, Sote Tuhusike’, yamebeba ujumbe unaotakiwa na kuwataka wananchi kutekeleza hayo kivitendo badala ya kuwaachia wanasiasa na makundi mengine.
Naye Mkurugenzi wa LHRC, Dk. Hellen Kijo Bisimba, alisema uandaaji wa filamu hiyo ambayo yeye ni mmoja wa washiriki unalenga kuendelea kutoa elimu kuhusu mchakato huo.
Dk. Bisimba alisema awamu hii katika kampeni hiyo ya kuendelea kutoa elimu kwa wananchi, wanaiita Kampeni Gogota namba 2 kwani wanaamini katiba ni maisha ya kila siku ya mwananchi, hivyo kila mtu anayo haki ya kushiriki vilivyo katika kujitengenezea maisha yake ya sasa na ya baadaye.
Katika kampeni hiyo wanatarajia kuzunguka mikoa 20 nchini ambako mbali na kuonesha filamu hiyo pia watakuwa wakigawa machapisho mbalimbali yaliyoandikwa kwa lugha rahisi kuhusu rasimu hiyo ya katiba.
Katika hatua nyingine mkutano wa mazungumzo ya maridhiano baina ya Baraza la Vyama vya Siasa nchini na vyama vya siasa umeahirishwa kwa muda usiojulikana.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Peter Mziray alisema kuwa kongamano hilo la mazungumzo limeahirishwa kutokana hudhuru ya viongozi.
Kongamano hilo, ambalo lilikuwa liwahusishe marais wastaafu ambao ni Benjamin Mkapa, Ali Hassan Mwinyi, Amani Abed Karume na wanasiasa wengine, limehairishwa kutokana na viongozi hao kupata hudhuru

Chanzo Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment