Saturday, August 30, 2014

Manji amgeuzia kibao Okwi

 

  • Aipa TFF siku 7, apanga kwenda FIFA, CAS
  • Asema kama jeuri ni fedha, Simba haiwezi

Manji amgeuzia kibao OkwiSAKATA la Mshambuliaji wa Kimataifa Emmanuel Okwi kuikacha timu yake ya Yanga aliyojifunga nayo mkataba wa miaka miwili na kurejea Simba, limechukua sura mpya baada ya Yanga kumtaka awalipe fidia ya dola 500,000 za Marekani.
Yanga chini ya Mwenyekiti wake Yusuf Manji, imetaka kulipwa kiasi hicho kutokana na kitendo chake nyota huyo kuibukia Simba wakati akiwa na makata wa kuicheza Jangwani alikotua kwa kishindo msimu uliopita akitokea Sports Club Villa ya Uganda.

Nje ya hilo, wameliomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) chini ya Rais wake Jamal Malinzi, litoe uamuzi juu ya sakata la mchezaji huyo ndani ya siku saba kabla ya wao hawajaamua vinginevyo.
Juzi, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili Zacharia Hanspope, ilimtangaza Okwi kurejea Simba baada ya nyota huyo kuuomba uongozi wa Simba afanye hivyo kutokana na Yanga kumpa barua ya kuvunja naye mkataba.

Wakati Okwi akijinadi hivyo mbele ya waaandishi wa habari katika mkutano huo wa juzi, Yanga wamekanusha wakisema hakuna kitu kama hicho kwa sababu nyota huyo bado ana mkataba wao.
Mwenyekiti wa Yanga, Yusuph Manji alisema jana mbele ya waandishi wa habari kuwa, hadi kufikia juzi asubuhi, Okwi alitakiwa awalipe wao (Yanga) fidia ya dola 200,000 za Marekani sawa na sh mil 300.

Manji aliongeza kuwa, kwa kitendo cha mchezaji huyo kujitangaza mbele ya vyombo vya habari kwamba ameondoka Yanga na yu tayari kujiunga na Simba, fidia yake kwa Yanga imeongezeka hadi kufukia kiasi cha dola hizo 500,000.

Kiongozi huyo alisema, kwa vile mchezaji huyo wa kimataifa anafanya hivyo akitambua kuwa yumo katika mkataba halali na Yanga, kadri siku zinavyoendelea baada ya juzi, fidia hiyo inaweza kuzidi kupanda.

Hata hivyo, Manji alihoji ukimya wa TFF juu ya vitendo vya ukiukwaji wa mkataba vinavyofanywa na mchezaji huyo kwani tayari walishawasilisha barua kwa Shirikisho hilo ikiwemo kutoroka, kufungiwa na kuingarimu Yanga katika mbio za kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania bara.
Manji alisema kwa mazingira hayo, waliandika barua TFF kuomba mwongozo, lakini mpaka sasa hawajapata majibu, hivyo jana waliamua kuwasilisha barua nyingine ya malalamiko kutokana na nyota huyo kutimkia Simba.

Manji alisema ndio maana wameamua kuwapa TFF siku saba kutoa majibu juu ya mchezaji huyo, vinginevyo watalazimika kupeleka suala hilo katika ngazi za juu kwa maana ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) na ikiwezekana Mahakama ya Usuluhishi wa Masuala ya Michezo (Cas).
Alisema katika barua waliyowasilisha TFF tangu jana, wamelitaka shirikisho hilo kuishusha daraja klabu ya Simba na kumfungia Okwi kujihusisha na masuala ya soka katika maisha yake ili kuwa funzo kwa wengine.

“Mimi sina kinyongo wala tatizo na Simba, lakini naona wao wanafanya fujo sasa, mimi ninachotaka tushindane uwanjani na tunaiomba TFF itende haki katika hili. Simba wakishuka Daraja wasije wakanilaumu kabisa,” alisema Manji.

Manji alikwenda mbali zaidi na kusema tatizo haliko kwao wanachama moja kwa moja, bali ni kuchagua watu wasio wa michezo bali wapenda sifa sizizo na tija kwa maendeleo ya mchezo wenyewe.

Aliongeza kuwa, kama hoja ni jeuri ya fedha, Yanga chini ya uongozi wake hawashindwi kufanya lolote ikiwezekana kumhamisha Amisi Tambwe na Kocha Mkuu Mzambia Patrick Phiri, lakini hawaoni mantiki ya kufanya hivyo ikiwemo kuheshimu kanuni na sheria za mchezo huo.
“Mimi nawashangaa wenzetu (Simba), wao kila mwanamke anayepita wanaona anafaa kuoa, kama ni jeuri ya fedha, mimi sishindwi.

Ninao uwezo wa kuchukua timu nzima ya Simba na kuwalipa mshahara bila hata kucheza soka wakiishia kufanya mazoezi tu katika ufukwe wa Coco,” alisema.

Chanzo Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment